Tuesday, July 15, 2014
UNDER THE SAME SUN YAWASHUKIA WAAGUZI WA HOSPITALI ZA OCEAN ROAD NA MUHIMBILI KWA KUKATAA KUMTIBU MLEMAVU WA NGOZI MWENYE SARATANI.
RUKIA KASEMBE MICHENGA (55)
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
IMETOLEWA NA UNDER
THE SAME SUN (UTSS)
TAREHE: 14 JULAI
2014
Shirika la Under The Same Sun
limesikitishwa na kitendo kilichofanywa na baadhi ya wauguzi na madaktari wa
hospitali za Ocean Road na ile ya Rufaa ya Muhimbili cha kumkatisha tamaa
mgonjwa wa saratani ya ngozi RUKIA KASEMBE MICHENGA (55) na kukataa kuendelea
kumtibu huku akiwa na maumivu makali.
Michenga amekuja katika ofisi za
UTSS akiomba msaada wa matibabu huku akilalamika kwamba madaktari wamemwambia
kuwa saratani aliyonayo haitibiki na hivyo asirejee tena katika hospitali hizo.
Japokuwa shirika letu halihusiki na
matibabu yoyote yale, tuna haki na tunao wajibu wa kulifikisha suala hili kwa
idara na viongozi husika kupitia vyombo vya habari.
Kwanza tunaona kwamba wafanyakazi
hao wa hospitali wamekiuka maadili yao ya kazi ya utabibu ambapo hawapaswi
kumkatisha tamaa mgonjwa.
Pili, ikiwa katika hospitali hizi
kuu wagonjwa kama Rukia wanapoambiwa kuwa hawawezi kutibiwa, watu wengi wenye
albinism wanaosumbuliwa na saratani ya ngozi wakimbilie wapi?
Wakati wa maadhimisho ya Tisa ya
Siku ya Watu wenye Albinism nchini Tanzania Mei 4 mwaka huu, kundi hili la watu
wenye ulemavu wa kurithi waliiambia serikali kwamba asilimia 80 ya watu wenye
ulemavu huo hufariki dunia majumbani kwao kwa kukosa matibabu ya saratani ya
ngozi.
Wakati huo huo asilimia 78 ya wagonjwa wanaofika
hospitali kwa matibabu hawapati huduma hiyo kwa wakati kutokana na urasimu
uliokithiri katika kliniki na hospitali za wilayani kabla ya kupewa rufaa
kwenda hospitali kuu, kama vile Ocean Road, Muhimbili na KCMC katika kitengo
cha RDTC.
Matokeo yake ni kwamba watu wengi
wenye albinism wanafika katika hospitali hizo wakati saratani ya ngozi
imeathiri sehemu kubwa ya mwili wao.
Michenga
ni mwenyeji wa Masasi,Alikuja Dar es Salaam kufuata matibabu wakati saratani ya
ngozi ikiwa imesambaa katika eneo kubwa la uso wake.
Amepoteza
jicho la kushoto ambalo limeliwa na saratani hiyo; na pia jicho lake la kulia
limepoteza uoni kabisa. Hivi sasa
Michenga haoni kabisa.
Ahadi
nyingi zinazotolewa na viongozi mbali mbali wa serikali za kutoa huduma bora
kwa watu wenye albinism hazizai matunda.
Badala yake ndugu zetu kama huyu Michenga wanaendelea kuteseka.
Tunatoa
rai kwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dr Seif Rashid kuliangalia suala
hili kwa makini zaidi ili kuokoa maisha ya Michenga na Watanzania wenzetu wengine
wenye albinism wanaosumbuliwa na saratani ya ngozi, ugonjwa ambao unaweza
kutibika endapo madaktari watagundua dalili mapema na kutoa matibabu bora na
haraka.
Mama huyu aruhusiwe kuendelea
kupata matibabu haraka iwezekanavyo tena bila malipo kwa kuwa serikali
imeidhinisha wagonjwa wenye albinism wenye saratani watibiwe bila kutozwa gharama
zozote.
RUKIA KASEMBE MICHENGA (55)
Tunamwomba
Mheshimiwa Waziri achunguze malalamiko haya ya Michenga ili hali kama hiyo
isijitokeze tena kwa mgonjwa yeyote yule.
Tunaiomba Wizara ya Afya ichukue hatua kali dhidi ya wauguzi na
madaktari wenye kauli za kuwakatisha tamaa wagonjwa na kuwarejesha nyumbani
huku wakijua kuwa hali zao hazitapata nafuu wakiwa mbali na hospitali.
Rukia
Kasembe Michenga kama wagonjwa wengine wa saratani anapata maumivu makali kwa
hiyo anahitaji dawa za kutuliza maumivu hayo na pia Tiba Shufaa (Palliative Care).
Tunawaomba wabunge wenye albinism katika Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Al Shaymaar Kweygir na
Mheshimiwa Bar’wani Khalfan wahakikishe kwamba suala la matibabu kwa watu wenye
albinism linashughulikiwa haraka iwezekanavyo.
Ahadi zao ziishie kwenye majukwa ya kisiasa na wakati wa kuomba kura tu. Wabunge hawa wanajua uchungu wa kuishi na
saratani ya ngozi kwa kuwa wao wenyewe wana ulemavu huo wa kurithi.
Tunatoa wito kwa wajumbe wa Bunge la Katiba
kuhakikisha kwamba suala hili la matibabu bure na haraka kwa watu wenye albinism wanapopatwa na
maradhi ya saratani linaingizwa kwenye Katika Mpya!
Hatma ya watu wenye albinism nchini Tanzania
ipo mikononi mwa Bunge la Katiba na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kila mnaporumbana kisiasa na kila
mnapojiongezea posho na marupurupu mengine, mnayaweka rehani maisha ya watu
wenye albinism!
Tunamwomba Mheshimwa Rais Dk. Jakaya Mrisho
Kikwete kutimiza ahadi yake ya kuhakikisha kwamba maisha bora kwa kila
Mtanzania yananawezekana pia kwa watu wenye albinism ikiwa atahakikisha kuwa
wanapata huduma bora ya afya mara dalili za awali za saratani
zinapogundulika!
Pamoja na kuwa
Michenga hakupata matibabu mapema, bado Rais wetu una nguvu za kuhakikisha kuwa
anapata matibabu sasa bila ya kuwepo na urasimu wa aina yoyote ile na pia
anapatiwa Tiba Shufaa haraka iwezekanavyo endapo itahitajika.
Afya na maisha ya Michenga yapo mikononi mwenu
ninyi mliopo madarakani na bungeni!
Tunatoa wito na
msisitizo kwa watu wenye albinism kujikinga dhidi ya mionzi ya jua kwa kuvaa
nguo zenye mikono mirefu na zinazofunika sehemu zote za mwili ikiwa ni pamoja
na miguu; kichwani ni muhimu kuvaa kofia pana ili kukinga sehemu za kichwa
usoni, shingoni na mabegani.
Tunaomba wawe wepesi
kufika hospitali au katika kituo cha afya karibu na makazi hao mara tu
wanapogundua vipele, mfano wa chunusi na / au malengelenge yamejitokeza katika
ngozi yao.
Hiyo ni dalili za awali za
saratani ambazo zisipotibiwa haraka zinaweza kuendelea na kuwa saratani kubwa
zaidi.
Watu wenye albinism
wasikubali wanapoambiwa na baadhi ya matabibu au wauguzi kuwa hivyo ndivyo
walivyo.
Washinikize kupewa
matibabu! Hakuna anayezaliwa na vipele,
vidonda au malengelenge!
Tunaziomba halmashauri
zote ziwajibike katika kuwasaidia watu wenye albinism pale wanapohitaji
matibabu ya saratani ya ngozi. Vingozi
wasiotekeleza haya ni lazima wawajibishwe na wizara husika!
MWISHO
Kwa maelezo zaidi
tafadhali wasiliana na:
Gamariel Mboya – Meneja
Uendeshaji: 0684968114 / 0754968114
Vicky Ntetema –
Mkurugenzi Mtendaji: 0787600136 / 0753177752
PS: TAFADHALI REJEA NUKUU ZA HANSARD (KWENYE
KARATASI NYINGINE) ZA MKUTANO WA 20: KIKAO CHA BUNGE CHA PILI – TAREHE 9 JUNI
2010 ZA MAJIBU YALIYOTOLEWA NA NAIBU WAZIRI WA AFYA NA USTAWI JAMII KUHUSU
MATIBABU YA WATU WENYE ALBINISM.
Tafadhali jiulize na
waulize viongozi wa Wizara husika na serikali kwa ujumla endapo haya
yaliyoahidiwa miaka minne iliyopita yametekelezwa.
Ruzuku kwa Dawa za Walemavu wa Ngozi (Albino)
MHE. MOHAMED RISHED ABDALLAH (K.n.y. MHE. AL-SHAYMAA
JOHN KWEGYIR)
aliuliza:- Nchi yetu inawajali sana watu wa makundi mbalimbali ya walemavu
nchini:- Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa ruzuku ya dawa za bure kwa ajili
ya kundi la walemavu wa ngozi (Albino) nchini ili wapate dawa ya
kujikinga na saratani ya ngozi?
NAIBU WAZIRI WA AFYA NA USTAWI WA JAMII alijibu:- Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Al-Shaymaa
John Kwegyir, Mbunge wa Kuteuliwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Wizara
inaandaa utaratibu wa kununua dawa na kuzisambaza kwa ajili ya walemavu ngozi (Albino),
kujikinga na Saratani ya ngozi katika mwaka wa fedha wa 2010/2011.
Kwa kuanzia, dawa hizo
zitasambazwa hadi Hospitali za Mikoa, Hospitali za Wilaya na Hospitali Teule
kupitia Bohari ya Dawa.
Mpango wa kuzifikisha dawa hizo hadi ngazi ya zahanati
na vituo vya afya utafuata.
Mheshimiwa Spika,
taarifa itatolewa kwa wananchi kuhusu namna ya kuzipata dawa hizi mara
zitakaposambazwa katika Hospitali za Mikoa, Wilaya na Hospitali Teule ili
waweze kuzitumia. Aidha, dawa hizi zitatolewa bila malipo kwa walemavu wa
ngozi.
MHE. MOHAMED RISHED ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Napenda kumuuliza
Mheshimiwa Naibu Waziri, maswali mawili madogo ya nyongeza.
(i) Pamoja na hizi dawa
lakini tunaona kwamba walemavu wa ngozi wana matatizo wakati wanapoingia juani
na macho yao kuyakunja kutokana na mwanga mkali wa jua. Je, Serikali ina
utaratibu wa kuona kwamba kila mwenye ulemavu huu anapata miwani; chombo
ambacho siyo ghali ili iweze kumsaidia?
(ii) Kwa faida ya Bunge hili na nchi yetu;
sijui Mheshimiwa Waziri anaweza
akatuambia kuna walemavu
wa ngozi wangapi Nchini Tanzania?
SPIKA: La
pili naona ni la takwimu, sijui linastahili wakati huu, lakini
inategemea. Mheshimiwa
Waziri majibu tafadhali.
NAIBU WAZIRI WA AFYA NA USTAWI WA JAMII: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali
ya nyongeza ya Mheshimiwa Rished kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni
kweli kabisa wenzetu wenye ulemavu wa ngozi pia wanapata matatizo sana
wanapopata mwanga machoni.
Ninakubaliana kwamba,
wanahitaji kabisa kupewa miwani, lakini vilevile kupatiwa kofia za kuwakinga
ili jua lisiweze kuwapata. Kwa hiyo, sisi kama Wizara tunalichukua hili ili
tuweze kuona kwamba ni namna gani wakati tunatoa dawa za ngozi, tuweze
kuwapatia miwani ambazo wataweza kuzipata japo kwa bei rahisi.
Mheshimiwa Spika, kuhusu
swali la idadi ya watu wenye ulemavu wa ngozi, Wizara sasa hivi kwa kweli haina
taarifa ambayo ni ya uhakika. Tumefanya Sensa Maalum ambayo itatuwezesha kujua
idadi ya albino ambao wapo kuanzia ngazi ya Mikoa, Wilaya mpaka katika
Vitongoji.
Chapisha Maoni