HOME
HATIMAYE ahadi za Rais John Magufuli alizozitoa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana zimeanza kuzaa matunda.
Miongoni mwa ahadi hizo ni zile za kutoa Sh milioni 50 kwa kila kijiji ili kuwawezesha kiuchumi, lakini pia ahadi ya kuzijengea uwezo halmashauri za wilaya ili ziweze kutekeleza miradi ya maendeleo ipasavyo. Katika makala haya, Mwandishi Wetu OSCAR MBUZA anaelezea mikakati ya serikali kukamilisha ahadi hizo za Rais Magufuli.
Katika mikutano ya kampeni za uchaguzi mkuu mwaka jana, Rais Magufuli wakati huo akiwa mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), aliahidi mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutoa Sh milioni 50 kwa kila kijiji na mtaa ili kusaidia katika kukuza shughuli za ujasiriamali.
Si hilo tu, Dk Magufuli pia aliwaahidi wananchi kujenga uwezo wa kiuchumi kwa makundi ya kijamii ikiwemo mikopo kwa wanawake na vijana kwa kuzijengea uwezo wa kifedha na uamuzi kwenye halmashauri. Kuhusu Sh milioni 50 kwa kila kijiji, Rais Magufuli alisema mpango wake huo wa kugawa fedha hizo ungeanza mara tu baada ya Watanzania kumchagua kuwa Rais wao. Miezi michache baada ya kuingia Ikulu, ahadi ya Rais Magufuli imeanza kuleta matumaini kwa Watanzania, hasa kutokana na kukamilika kwa mpango huo.
Kupitia Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, tayari mikakati na mpango wa usambazaji wa fedha hizo kwa wananchi na hasa masikini wa vijijini, umekamilika na kielelezo kinajidhihirisha wazi katika Bajeti ya Kwanza ya Uongozi wa Rais Magufuli inayoendelea kujadiliwa mjini Dodoma.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa analieza Bunge namna serikali ilivyojipanga kuhakikisha kuwa utoaji wa fedha hizo kwa wananchi unaanza. Majaliwa anasema, katika mwaka ujao wa fedha, Serikali imetenga Sh bilioni 59 ili kuweza kutekeleza ahadi hiyo ya Rais kwa kuanza kugawa fedha hizoi. Anasema, ili kuhakikisha kuwa zinakuwa na manufaa, zitatolewa kwa kikundi cha kifedha kilichosajiliwa kutoa huduma hiyo na kilicho na Katiba na inayotambulika katika mamlaka za serikali.
Anataja sifa nyingine kuwa ni kikundi hicho kuwa chini ya asasi ya kiraia, kiwe na uzoefu wa utoaji wa mikopo usiopungua mwaka mmoja, hesabu zake zikionesha kulipwa kwa mikopo iliyokuwa inatolewa kwa wanachama wake katika mikopo iliyotangulia. Ukiondoa fedha zitakazogawanywa kupitia vikundi, Waziri Mkuu anasema kwa upande wa vyama vya akiba na mikopo (SACCOS), fedha hizo zitatolewa kwa kuzingatia Sheria ya Ushirika ya Mwaka 2013.
Kuzijengea uwezo halmashauri Waziri Mkuu anasema serikali imeamua mara moja kubadili mfumo wa awali uliokuwa unazipa halmashauri hizo mamlaka ya kuidhinisha mikataba isiyozidi thamani ya Sh milioni 50 na ile inayozidi ikilazimika kupelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG). Anasema katika mfumo wa sasa unaolenga katika kuondoa urasimu wa kurundikana kwa mikataba katika ofisi ya AG na kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo, sasa thamani itakayoidhinishwa na halmashauri hizo itafikia thamani ya Sh bilioni moja.
Hata hivyo pamoja na ruhusu hiyo kwa halmashauri, Waziri Mkuu anasema serikali itakuwa macho kuhakikisha halmashauri zinazingatia sheria ya manunuzi na sheria zinazowahusu wanasheria wanaohusika na uidhinishaji lakini pia weledi wa utumishi wa umma na watakaokiuka watakumbana na meno ya serikali.
“Tumefikia hatua hiyo baada ya kutathmini mfumo wa sasa na kuona kuwa unasababisha ucheleweshaji wa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, hasa kutokana na kasi iliyopo katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika kupitisha Mikataba hiyo kuwa ndogo,” anasema Majaliwa. Anasema, katika kuhakikisha mfumo wa sasa unatekelezwa kwa ufanisi, halmashauri zinaruhusiwa kuomba ushauri wa kisheria kutoka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika maeneo ambayo yanaweza kusababisha matatizo.
Wabunge wanapongeza uamuzi wa kutenga kwa Sh milioni 50 kwa kila kijiji katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha na hatua ya Serikali Kuu kuendelea kugatua madaraka kwa serikali za mitaa kwa kuziongezea ukomo wa fedha za miradi ya maendeleo. Mbunge wa Mkuranga, Abdallah Ulega (CCM) anasema kutengwa kwa fedha hizo, kumeibua matumaini kwa wananchi wanaoamini kuwa zitakuwa ni chachu ya kusukuma mbele miradi ya ujasiriamali.
Mbunge wa Viti Maalum, Ritha Kabati (CCM) anasema, mpango wa serikali wa kugatua madaraka kwa kuziongezea halmashauri za wilaya nguvu kuamua matumizi ya fedha kwenye miradi ya maendeleo, kutaharakisha maendeleo kwa kasi kubwa katika serikali za mitaa. Anasema ukomo wa awali uliokuwa unazipa halmashauri kupitisha manunuzi yasiyozidi Sh milioni 50 tu ulikuwa unachelewesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa vile mfumo wa kupeleka mikataba ya zaidi ya Sh milioni 50 kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ulikuwa unasababisha urasimu na kuchelewesha maendeleo.
Kabati anasema, jukumu kubwa linabaki mikononi mwa wabunge ambao ni wajumbe wa Baraza la Madiwani katika kusimamia ili kuhakikisha kuwa watendaji wa halmashauri wasio waaminifu hawatumii mwanya huo kuiingiza serikali hasara kwa kuidhinisha fedha nyingi katika mikataba isiyo na tija. Mbunge wa Viti Maalumu, Kunti Majala (Chadema) anasema serikali inapaswa kuwasilisha bungeni baadhi ya mikataba ambayo itaonekana ina ulazima wa kufika hapo ili wabunge waijadili kwa niaba ya wananchi.
Aituhumu Serikali kuwa imekuwa ikipitisha mikataba hiyo bila kufanya hivyo hivyo kukiuka matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoagiza mikataba kufikishwa bungeni ili kujadiliwa. Anasema pamoja na madhara mengine, nchi pia imekuwa inapata hasara kwa kuwa baadhi ya watendaji wanapitisha mikataba hiyo kwa kushawishika na rushwa, hivyo kusababisha kushamiri kwa vitendo vya ufisadi.
Waziri Mkuu anakiri kuwa ni kweli Bunge lina wajibu wa kuisimamia serikali lakini yapo maeneo ambapo limetoa mamlaka ya kisheria kwa serikali kutekeleza majukumu ili kuharakisha maendeleo. Anasema moja ya eneo ambalo wabunge kupitia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wametoa mamlaka kwa serikali kutekeleza majukumu yake ni mikataba. Katiba inatoa nguvu ya kisheria kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia na kupitisha mikataba hiyo.
“Mwanasheria Mkuu anafanya kazi hii ya kupitia mikataba kwa niaba ya serikali na Bunge, kama mikataba yote ingekuwa inakuja hapa bungeni ili kujadiliwa na wabunge basi Bunge lisingekuwa na kazi nyingine zaidi ya kupitia mikataba,” anasema Waziri Mkuu. Anasema, hakuna ubaya endapo wabunge watapendekeza kuwasilishwa bungeni kwa mikataba ya kiwango au aina fulani ili waijadili kwa niaba ya wananchi kulinda maslahi ya taifa.
Kuhusu ufisadi katika mikataba, Majaliwa anasema pamoja na mikataba kupitishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, inapobainika kuna ukiukaji wa maadili na sheria za nchi, hatu zimekuwa zinachukuliwa kwa wahusika wa suala hilo. Anasema katika kuhakikisha kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali anapunguziwa mzigo wa kupitia mikataba yote Serikali imeamua kubadili mfumo katika halmashauri za wilaya ili mamlaka zao zipitie na kuidhisha mikataba yenye thamani isiyozidi Sh bilioni moja kutoka ukomo wa zamani wa Sh milioni 50.
SOURCE:HABARI LEO
Chapisha Maoni