HOME
IMEANDIKWA NA MAULID AHMED
IMEANDIKWA NA MAULID AHMED
Baada ya baadhi ya wafanyabiashara kuficha sukari kwa lengo la kuhujumu uchumi, Serikali imeazimia kuagiza sukari na kuwachukulia hatua wafanyabiashara wote wanaoficha sukari kwa lengo la kuhujumu uchumi kama Mwandishi Wetu MAULID AHMED anavyoeleza katika makala haya.
“SERIKALI ya Magufuli haiwezi kushindwa kununua sukari kutoka nje....imeweza kugharimia elimu watoto wasome bure kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne haiwezi kushindwa kununua sukari,” amesema Rais John Magufuli. Rais Magufuli ametoa kauli hiyo hivi karibuni eneo la Katesh mkoani Manyara wakati akizungumzia uhaba wa sukari uliojitokeza baada ya wafanyabiashara kuficha sukari kwa lengo la kuhujumu uchumi. Rais Magufuli amewaonya wafanyabiashara hao na kuwataka kutoa sukari hiyo na kuisambaza kabla ya serikali haijatumia vikosi vyake kuisambaza na kuigawa bure.
“Kuna mfanyabiashara mmoja amenunua sukari tani 3,000 kiwanda cha sukari Kilombero akaacha kuichukua , mwingine kwenye ghala Mbagala ana tani 4,000 hataki kuzitoa kusudi wananchi wakose sukari…nawahimiza waitoe mara moja,” anasema Magufuli. Anaendelea kusema, “niwaambie sukari huwezi kuificha kama sindano, nimeshaagiza vyombo vya dola vifuatilie wafanyabiashara wote walioficha sukari, hao ni wahujumu uchumi... tutachukua sukari na tutaigawa bure kwa wananchi.”
Rais anawaonya wafanyabiashara wanaoficha sukari kwamba hawatapata fursa ya kufanya biashara nchini Tanzania na kusisitiza kuwa kila mfanyabiashara anayejaribu kucheza na serikali yake wajue kuwa wanacheza na maisha yao wenyewe. Rais Magufuli anatoa salamu kwa wafanyabiashara wasio waaminifu walioamua kuficha bidhaa hiyo kwa lengo la kupandisha bei na kuifanya bidhaa hiyo iwe adimu hasa baada ya kuona serikali imechukua hatua za kudhibiti sukari kutoka nje, ambayo si salama na pia inavifanya viwanda vya ndani vikose soko la sukari.
Hasira hizi za wafanyabiashara ziliibuka baada ya serikali mwezi uliopita kutoa bei elekezi ambayo kwa rejereja kilo moja inatakiwa kuuzwa Sh 1,800. Hapo ndipo Watanzania walipoanza kuonja chungu ya maisha kwani sukari imeadimika na inapopatikana bei ipo juu kuanzia Sh 2,500 hadi 4,000. Hata pale Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipotangaza kuwa kutokana na upungufu wa sukari wa tani 120,000 ya matumizi ya kawaida, serikali itaagiza bidhaa nje ya nchi bado wafanyabiashara wameonesha kiburi na kuendelea kuificha sukari hiyo.
Inawezekana wanafaidika zaidi na sukari ya nje kwani inayoingia nchini inatokea zaidi Brazil ambapo wafanyabiashara wasio waaminifu wanakwenda huko kuchukua sukari inayokaribia kuisha muda wake wa matumizi na kuiweka kwenye mifuko na kuwauzia Watanzania. Kwa kawaida Serikali ya Brazil hutupa baharini sukari inayoisha muda wake. Sukari hiyo kutoka Brazil imekuwa ikiingizwa nchini kupitia bandari bubu kwa majahazi kama Mbweni, Bagamoyo, Zanzibar, Tanga na njia nyingine zinatotumika kuigiza bidhaa za magendo.
Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli imeamua kuwabana wafanyabiashara wasio waaminifu wanaoingiza sukari hiyo inayodaiwa kuhatarisha afya na kudhoofisha viwanda ya sukari vya ndani. Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba wakati anawasilisha bungeni Makadirio ya Mapato na Matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2016/2017 hivi karibuni, ametaja hatua zinazochukulia na serikali kuwabana wafanyabiashara hao wa sukari wasiokuwa waaminifu.
Hatua mojawapo ni kuundwa kwa kikosi kazi kinachoratibiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kujumuisha Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari(TPA) na vyombo vya ulinzi na usalama ili kudhibiti magendo ya sukari. Nchemba anasema katika kudhibiti sukari inayoagizwa kutoka nje, Serikali imeanzisha utaratibu wa kuwatoza kodi kwa asilimia 15 zaidi tofauti na kodi ya kawaida ya asilimia 10.
“Katika utaratibu huu kila kiwanda kinawajibika kuthibitisha kwa TRA matumizi halisi ya sukari waliyoagiza na kutumia kabla ya kurejeshewa asilima 15,”anafafanua Nchemba. Nchemba anataja hatua nyingine iliyochukuliwa na serikali ni kuunda kikosi kazi kinachoratibiwa na TRA ili kusimamia udhibiti wa sukari inayopita nchini kwenda nchi jirani . Kikosi kazi hicho kinajumuisha pia vyombo vya ulinzi na usalama na TPA.
Kikosi kazi hicho kinafuatilia sukari kuanzia inapoingia kwenye maghala ya forodha hadi sukari hiyo inapovuka mipaka ya Tanzania. TRA imeanzisha mfumo wa kielektroniki wa kufuatilia shehena za sukari hadi zinapovuka mipaka ya Tanzania. TRA inasimamia utekelezaji wa malipo ya Hati Fungani au malipo ya fedha taslimu ya asilimia 100 ya thamani ya sukari inayopita nchini kwenda nchi jirani .
Hati fungani au malipo taslimu hurejeshwa kwa wahusika baada ya TRA kuthibitisha kuwa shehena ya sukari imevuka mipaka. Pia mwaka 2015 serikali ilifanya marekebisho ya Kanuni za sukari za mwaka 2010 kwa kurekebisha muundo na majukumu ya Kamati ya Ufundi na Ushauri ya uagizaji sukari ili iwe na uhuru wa kutoingiliwa ili iongoze ufanisi katika utendaji wake wa kazi.
Pia kuipa Bodi ya Sukari mamlaka ya kisheria ya kukagua sukari kabla haijaruhusiwa kutoka bandarini na kuipa mamlaka ya kushirikishwa na TRA katika kudhibiti sukari inayopita nchini kwenda nchi jirani na kuanzisha kisheria mfumo wa kuagiza sukari wa pamoja kwa kutumia chombo kitakachoanzishwa na wazalishaji na wafanyabiashara wa sukari. Nchemba anataja hatua nyingine ni Serikali imeanzisha utaratibu maalumu kwa kufanya ukaguzi maalumu wa viwanda vinavyotumia sukari ili kupata takwimu za mahitaji halisi ya sukari ya vi- wandani.
Ukaguzi huo unahusisha pia uhakiki wa kutambua kiasi cha sukari kilichopo . Takwimu hizi ndizo zinazotumika kama msingi wa Bodi ya Sukari kutoa leseni kwa waagizaji sukari ya viwandani. “Serikali kupitia Bodi ya Sukari, Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Jeshi la Polisi zimeanzisha utaratibu wa ukaguzi wa kushtukiza kwenye maghala ya sukari na maduka hapa nchini ili kubaini sukari inayoingizwa kinyume cha sheria na kuchukua hatua stahiki,” Nchemba anabainisha.
Anasema serikali inahamasisha uzalishaji wa sukari kupitia wawekezaji katika mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) imeainisha eneo la hekta 294,000 kwa ajili ya uzalishaji wa sukari katika mikoa ya Kagera, Kigoma, Morogoro, Mara, Mtwara, Pwani na Tanga. Mashamba hayo ni kwa ajili ya uwekezaji na yanamilikishwa kupitia utaratibu wa zabuni chini ya Kituo cha Uwekezaji (TIC).
Katika kuthibitisha hilo, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amesema Kiwanda cha Sukari cha Kigoma kitaanzishwa mkoani Kigoma na tayari kimeshapewa eneo la hekta 47,000 kwa ajili ya kuzalisha sukari. Mwijage anasema kiwanda hicho kitakapoanza uzalishaji, kitakuwa kinazalisha tani 120,000 za sukari kwa mwaka. Bila shaka uzalishaji huo utakidhi upungufu wa sukari uliopo sasa wa tani hizo 120,000 za matumizi ya kawaida.
Kwa sasa mahitaji ya sukari ni wastani wa tani 420,000 kwa matumizi ya kawaida na tani 170,000 kwa ma- tumizi ya viwandani . Uzalishaji wa sukari kwa mwaka ni wastani wa tani 300,000 ambazo zote ni kwa matumizi ya kawaida hivyo takribani tani 290,000 huagizwa kutoka nje ikiwa ni kufidia upungufu wa tani 120,000 za matumizi ya kawaida na tani 170,000 kwa matumizi ya viwandani.
Kutokana na upungufu huo mdogo, wafanyabiashara wasio waaminifu wamekuwa wakiingiza sukari kutoka nje ambayo muda wake karibia unamalizika kwa njia za bandari bubu, wanauza nchini sukari inayosafirishwa nje na wanauza sukari ya matumizi ya viwandani kwa ajili ya matumizi ya kawaida. Hali hiyo imesababisha kuyumba kwa soko la sukari ya ndani na yote hii ni kutaka faida kubwa kuamua kuingiza tone la shubiri kwenye tamu ya sukari, hali ambayo sasa serikali imeshtukia na kuanza hatua ya kuondoa shubiri kwenye utamu wa sukari.
SORCE HABARI LEO
Chapisha Maoni