HOME
“TUMEANZA kuifanyia kazi kauli ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein ya kutumia vizuri rasilimali zetu na kuimarisha uchumi bila kutegemea washirika wa maendeleo,” anasema Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk Halid Salum.
Dk Salum anasema katika kipindi cha uongozi wa miaka mitano Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itafanya kazi kwa kuzingatia hotuba ya Rais Dk Shein ambayo ni kama dira kwa ajili ya kuimarisha uchumi na kupambana na umasikini. Anasema watendaji wa Wizara ya Fedha na Uchumi wamejipanga kuhakikisha kwamba Zanzibar inajitegemea kwa kuweka kipaumbele katika suala zima la kutumia vizuri rasilimali ziliopo na ukusanyaji wa mapato katika vyanzo mbalimbali.
Katika suala la ukusanyaji mapato, anasema taasisi mbili zilizokabidhiwa jukumu hilo ni Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) pamoja na Bodi ya Mapato nchini (ZRB) kuhakikisha kwamba zinafanya kazi ya kubuni ya kukusanya mapato katika vyanzo vyote vikiwemo vipya. Anasema katika kipindi cha miaka mitano Serikali itatoa kila aina ya ushirikiano kwa taasisi hizo ikiwemo wafanyakazi wake kuona wanatekeleza malengo yaliyowekwa kwa mujibu wa sheria.
Katika suala la ukusanyaji wa mapato anasema malengo ni kuhakikisha hadi kufikia 2020-2021 taasisi za ukusanyaji wa kodi zinafikia malengo ya Sh bilioni 800 kutoka Sh bilioni 362.8 katika mwaka 2014-2015. Anasema matarajio makubwa zaidi yapo baada ya kukamilika kwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amaan Karume katika jengo la abiria ambalo litakuwa na uwezo wa kuchukua abiria milioni 220 kwa mwaka.
Aidha anasema ujenzi wa bandari mpya kwa Mpiga Duri itakuwa moja ya kichocheo kikubwa cha kukua na kuimarika kwa uchumi wa Zanzibar sambamba na kuongeza ajira kwa vijana. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ipo katika hatua za mwisho za makubaliano na Benki ya Exim kutoka China kwa ajili kutia saini ujenzi wa bandari hiyo kwa awamu tofauti.
Anasema eneo la bandari ya sasa ya Malindi ni dogo sana huku likiwa limezidiwa na wingi wa makontena kiasi ya wakati mwingine meli kushindwa kushusha bidhaa kwa ajili ya kusubiri kuondoshwa kwa makontena mengine na hivyo kusababisha kuzorota kwa shughuli za uzalishaji katika bandari hiyo.
Amesema kwamba Serikali imeweka mikakati ya kutekeleza vipaumbele vichache katika mwaka wa fedha 2015-2016 ikiwemo miradi ambayo itashirikisha sekta binafsi ya ujenzi wa hoteli za kitalii zenye hadhi ya nyota tano pamoja na ujenzi wa nyumba za kuishi wananchi na wageni. Miradi hiyo inayotazamiwa kuwashirikisha wafanyabiashara maarufu akiwemo Said Bakhresa itatekelezwa katika mji wa maeneo huru ya uchumi huko Fumba mkoa wa Mjini Magharibi Unguja pamoja na Mtoni.
Anasema eneo la uchumi la Fumba tayari limeanza kutumika vizuri kwa ujenzi wa kiwanda cha kisasa cha Maziwa ambacho tayari kimeanza kazi ya uzalishaji wa bidhaa na kuingia katika Soko la Afrika ya Mashariki. Kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuhamasisha wawekezaji mbalimbali kuwekeza Pemba ambapo mazingira ya uwekezaji yameimarika kwa kiwango kikubwa ikiwemo miundombinu ya barabara kutoka mjini hadi vijijini pamoja na nishati ya umeme wa uhakika.
Anasema eneo la uwekezaji wa maeneo huru ya Micheweni huko Pemba likitumiwa vizuri linaweza kuleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi kwa ujenzi wa viwanda mbalimbali ambapo kwa sasa miundombinu imeanza kuimarika kidogo kidogo. “Tumepanga kutekeleza miradi michache ikiwa ni sehemu ya vipaumbele vyetu kwa mwaka wa fedha 2015-2016 ambapo baadhi yake ni miradi itakayoishirikisha sekta binafsi imeanza kufanya kazi ikiwemo kiwanda cha Maziwa cha Bakhresa kiliopo Fumba mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, “ anasema Dk Salum.
Dk Salum anasema Serikali imeweka mikakati ya kukuza pato la mtu binafsi kutoka dola za Kimarekani 939 na kufikia dola za Kimarekani 1,046 sambamba na kukua kwa uchumi kwa asilimia 8.10 kutoka 6.6 katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Waziri wa Habari, Utangazaji, Utalii na Michezo, Rashid Ali Juma, anasema sekta ya utalii ndiyo tegemeo la kuingiza mapato katika vianzio mbali mbali kwa hivyo watafanyakazi kwa kuweka kipaumbele katika kuboresha sekta hiyo.
Juma anasema sekta ya utalii inachangia pato la taifa kwa asilimia 60 na kutoa ajira kwa asilimia 47. Juma ameyataja maeneo ambayo yataimarishwa kuwa ni pamoja na ubora wa utoaji wa huduma kwa wageni kama njia mojawapo ya kuwavutia watalii wengi zaidi kuja Zanzibar. Katika kufanikisha hatua hiyo Serikali ipo katika hatua za kuimarisha Chuo cha Utalii kiliopo Maruhubi kuweza kutoa wanafunzi zaidi katika sekta mbalimbali.
“Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejizatiti kuhakikisha kwamba sekta ya Utalii inaimarishwa na kukuzwa kwa kiwango cha utoaji wa huduma kwa wageni pamoja na kuitangaza Zanzibar katika maonesho ya kimataifa yanayofanyika ulimwenguni kote,” anasema Juma. Kwa mujibu wa takwimu ziliopo zinaonesha kwamba katika mwaka 2010 jumla ya watalii wapatao 132,836 wakitembelea Zanzibar ambapo hadi kufikia mwaka 2014 idadi ya watalii iliongezeka na kufikia 311,89, ambapo kwa ujumla wageni waliotembelea Zanzibar hadi kufikia mwaka jana 2015 walikuwa 294,243.
Juma anasema malengo yamewekwa hadi kufikia mwaka 2020 Zanzibar itakuwa na uwezo wa kupokea jumla ya watalii 500,000 kwa mwaka huku idadi ya hoteli zenye hadhi ya nyota tano zikiongezeka. “Hayo ndiyo malengo yetu tuliyojipangia kuhakikisha tunaongeza idadi ya watalii mwaka hadi mwaka kwa kutumia fursa ya kutangaza sekta hiyo nje ya nchi ikiwemo kushiriki katika maonesho ya kimataifa yanayofanyika nchi mbalimbali kuanzia Afrika Arabuni na Ulaya,’’ anasema.
Zanzibar imefanikiwa kufungua ofisi ndogo kwa ajili ya matangazo ya utalii huko Mumbai India ikiwa ni sehemu ya kutangaza soko la utalii liliopo visiwani. Juma alisema kwamba Zanzibar kwa sasa imeweka mikakati zaidi kwa ajili ya kuingia soko la Asia lenye idadi kubwa ya watu wenye uwezo wa kifedha. Kwa sasa Zanzibar inategemea kupokea watalii wengi kutoka nchi za Ulaya ikiwemo Italia, Uingereza pamoja na Afrika
SOURCE:HABARI LEO
Chapisha Maoni