HOME
Mahakama ya Kadhi yalitafuna Bunge
Wakati Waislamu wakishikilia msimamo huo, wajumbe
ambao ni Wakristo nao wamejipanga kupiga kura ya hapana endapo Mahakama
ya Kadhi itaingizwa katika Katiba inayopendekezwa.
Dalili za mpasuko huo zilianza kujitokeza jana
asubuhi baada ya mjumbe mmoja, Jaku Ayub Hashim kuwasha kipaza sauti
akitaka kuzungumza akisema ana jambo muhimu.
“Mheshimiwa tangu jana (juzi) ulisema utanipa
nafasi ya mwanzo nizungumze,” alisema Jaku, lakini Makamu Mwenyekiti,
Samia Suluhu alimtaka aketi chini na suala lake limesikika.
Suluhu akaendelea kuwapa wajumbe wengine kuendelea
kuchangia na baadaye alimpa Jaku muda wa dakika saba ili kuwasilisha
kile alichotaka kukizungumza ndani ya Bunge hilo.
Jaku alisema walipendekeza kifungu kinachotaka
uamuzi unaohusu ndoa, talaka na mirathi iliyoamuliwa kwa misingi ya dini
ingizwe kwenye Katiba inayopendekeza lakini hakimo.
“Ni kitu kidogo kabisa tuliomba kiongezwe lakini
cha kusikitisha kikundi cha sanaa kimeingizwa. Mimi binafsi yangu
sitaunga mkono wala mguu wala sitaipigia kura hii,” alisema Jaku.
Suluhu akamweleza kuwa angalizo lake
limechukuliwa, na uongozi wa Bunge pamoja na kamati ya Uandishi
wanajitahidi kuingiza kila kitu kinachowezekana, lakini kwa misingi na
sheria za nchi.
Baadaye Sheikh Masoud Jongo alipopewa nafasi ya
kuchangia, naye alitahadharisha kuwa mambo yaliyopendekezwa na Waislamu
yasipoingizwa kama ilivyo kwa sasa, hawatakuwa tayari kwa lolote.
“Msimamo wetu sisi Waislamu kama mambo yetu
tuliyoleta katika mapendekezo hayataingizwa, basi yatabomokea hapa na
hatutakuwa tayari tena,” alisema Sheikh Jongo, kauli iliyowashtua
wajumbe.
Akihitimisha majadiliano hayo, Mwenyekiti wa
Kamati ya Uandishi, Andrew Chenge alisema kamati yake imefanya kazi kwa
uadilifu mkubwa na kwa masilahi ya Watanzania. Akiahirisha Bunge, Suluhu
alisema kesho Bunge litaanza kwa kupitia baadhi ya mambo yaliyoibuka
katika uhakiki kisha kupitisha azimio la upigaji wa kura. Kura zitapigwa
kati ya kesho hadi Oktoba 2.
Baada ya kuahirishwa kwa Bunge, Sheikh mwingine,
Hamid Jongo alimwendea Askofu mstaafu Donald Mtetemela na kumkumbatia,
kisha kumvuta pembeni na kisha kuteta kwa dakika tano.
Katika viwanja vya Bunge, hali ilikuwa tete kwani kulikuwa na
makundi tofauti tofauti ya Wakristo na Waislamu kila moja likijadili na
kutafakari suala la Mahakama ya Kadhi kuingizwa kwenye Katiba.
Mjumbe wa kundi la 201 Dk Aley Nassoro alisema
kuwa suala la Mahakama ya Kadhi lisipoingizwa katika Katiba
inayopendekezwa, atakuwa wa kwanza kuhamasisha wenzake ili wagome kupiga
kura.
Dk Nassoro alisema Waislamu wamechoka kudanganywa
kwani tangu kipindi cha kampeni za mwaka 2010, waliahidiwa kuwa jambo
hilo lingeshughulikiwa mapema lakini watawala wamekuwa kimya.
“Hii Katiba itakuwa ni mbovu kuliko ile ya mwaka
1977 na italeta migongano baada ya miezi sita tu tangu kuzinduliwa. Bora
iachwe kwani mambo mengi ya msingi kwa Wazanzibari yameachwa,”alisema.
Akiwa viwanja vya Bunge Askofu Mtetemela
alionekana akishauriana na wajumbe mbalimbali na baadaye alisema
analaani kauli hizo na kusema kuwa hazilengi kujenga nchi badala yake
zinabomoa.
“Kinachotakiwa ni amani, sasa tukianza kutishiana
mambo hayatakwenda maana na sisi Wakristo tutataka mambo yetu yaingizwe
humo, tunachohitaji ni amani na si vinginevyo,” alisema Mtetemela.
Askofu Mtetemela alisema kikubwa kinachotakiwa kwa
wajumbe ni maridhiano na isiwe vitisho kwa kuwa walianza pamoja hivyo
wanapaswa kumaliza pamoja.
Aliitaka Kamati ya Uandishi kutoingiza kabisa
jambo hilo katika Katiba na akasema hali ikifikia hapo itasababisha
mgogoro wa kimasilahi kwa kila mtu kudai haki yake ndani ya Katiba.
Hata hivyo, aliitaka Serikali kutunga sheria za
kutambua uamuzi wa Waislamu wa ndoa, mirathi na umiliki wa rasilimali
kwa Waislamu ili yakubaliwe kwenye sheria siyo kwenye Katiba.
Mjumbe mwingine wa Bunge hilo, John Cheyo, alitaka
Watanzania kuendelea kuheshimu Katiba ambayo imeweka wazi kuwa Serikali
haina dini bali wananchi wake ndiyo wenye dini.
“Kwa sababu ukienda njia hiyo hakuna
atakayeshinda. Na sisi Wakristo tuseme bila ‘Canon Law’ (Sheria za
Kanisa) hakuna hatupigi kura, tutafika wapi? Ndiyo maana
tuliyatenganisha haya mambo,”alisema.
Wakati makundi hayo yakiwa na msimamo tofauti,
jana katika viwanja hivyo vya Bunge walisikika Waislamu wakihamasishana
kwamba kama ikifika kesho hakuna Mahakama ya Kadhi wasusie Bunge.
Suala la Mahakama ya Kadhi, linaonekana kuwapasua kichwa wajumbe
wa Kamati ya Uongozi ambayo juzi na jana zilikutana kutafuta njia ya
kulinusuru Bunge hilo na mpasuko huo mkubwa.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho, zilieleza kuwa
baadhi ya wajumbe walipendekeza kuitishwa kwa Kamati ya Maridhiano ili
kutafuta njia bora itakayonusuru Katiba Mpya kukwama kesho.
CUF watuhumu mbinu chafu
Wakati hayo yakijiri Dodoma, Chama cha Wananchi
(CUF) kimesema kuwa kimebaini mbinu zitakazotumiwa kuongeza idadi ya
kura zinazotarajiwa kupigwa Jumatatu kwa njia ya mtandao kuunga mkono
Katiba iliyopendekezwa.
Bunge Maalumu hivi karibuni lilizifanyia
marekebisho kanuni zake ili kuwaruhusu wajumbe watakaokuwa nje ya Ukumbi
wa Bunge wakiwamo wanaokwenda Hijja kuipigia kura Katiba
inayopendekezwa. Chini ya marekebisho hayo, mjumbe aliye nje ya Bunge,
ataruhusiwa kupiga kura ya wazi au ya siri kwa njia ya nukushi (Faksi)
au barua pepe kama itakavyoelekezwa na katibu kwa kushauriana na
mwenyekiti.
Akizungumza jana katika ofisi za CUF, Mkurugenzi
wa Ulinzi na Usalama, Yusuf Salim Hussein, alizitaja mbinu hizo kuwa ni
pamoja na kuingiza majina ya wabunge wa chama hicho na Chadema kwenye
orodha ya waliopiga kura.
“Taarifa tulizo nazo sisi kutoka huko Dodoma ni
kwamba yatawekwa majina yasiyopungua 10 ya chama chetu na 10 ya Chadema
kwamba wamepiga kura katika njia ya mtandao,” alisema Hussein.
Alisema Jumatano wiki iliyopita wabunge na
wawakilishi wa chama cha CUF walikuwa na kikao cha pamoja na kukubaliana
kwamba hakuna mjumbe yeyote atakayepiga kura kwa njia ya mtandao.
Chapisha Maoni