HOME
Sumu ya rasimu
‘Aisee, mimi napenda sana polisi wanavyofanya kazi siku hizi?’
‘Hawakudai rushwa tena?’
‘Achana na wale. Juzi kuna wezi walitaka kuvunja
nyumba yangu usiku. Basi tulipoona hali mbaya, mke wangu akapiga simu
polisi wakati mimi natafuta sime. Majibu kama kawaida … ‘Oh hatuna
petroli, huwezi kutuletea M-pesa kidogo tununue na majibu mengi ya
kukera, hadi mke wangu akakata simu kwa hasira. ‘
‘Hapa kuna nini cha ajabu? Yaleyale.’
‘Ngoja Bwana. Mbona kiherehere kama mheshimiwa
mbele ya posho? Wakati nasikia wezi bado wanatafuta jinsi ya kupenya na
mimi nilipiga simu polisi. ‘Jamani eee, kuna vijana wamejikusanya hapa,
eti wanajiandaa kuandamana kupinga Bunge letu tukufu la Katiba.’
‘Wacha wewe’
‘Ndiyo. Nakuambia hata dakika kumi hazikupita,
polisi hao! Tena walikuja na kasi ya ajabu na magari matano na deraya na
mabomu ya machozi na maji ya kuwasha hadi wale wezi hawakufurukuta
tena. Nadhani bado wanajikuna huko selo. Sisi tu tulibaki ni athari
kidogo ya mabomu yale, lakini angalau sisi tulikuwa salama na wezi sasa
wameswekwa ndani bila kuona ndani.’
‘Duh!’
‘Kabisa. Kwa hiyo, mambo yamebadilika. Eti utoe
taarifa ya wizi au uhalifu wowote, umepitwa na wakati. Ukiona jambo
lolote siku hizi, piga simu na ongelea maandamano. Hapo magari yao
yanafufuka na petroli inajitokeza kama miujiza. Udumu mchakato wa
kutibua.’
Basi wacha watu wacheke. Na wengine waliongeza.
‘Siku hizi ya nini kuandamana ili uandamwe.
Tangaza maandamano na polisi watafanya maandamano kwa niaba yenu. Kaa
pembeni na waangalie tu na wakimaliza maandamano yao, tangaza maandamano
mengine sehemu nyingine, ili mradi wazunguke mji mzima wakiandamana
siku nzima. Senema ya bure nakuambia.’
Ndiyo maana nawapenda sana Wabongo. Si tu kwamba kila mtu ana
wazo lake tofauti na mwenzie (na sijui wangapi wako tayari kweli
kuwasikiliza wengine na kupima iwapo wana hoja au la), lakini wanajua
kugeuza hata hali mbaya ili hali ya kuwafaidi wao.
Lakini siyo wote waliokubali. Mwingine alikasirika sana.
‘Huu ni upumbavu kabisa, eti kuvuja kwa pakacha. Ukiwa umebeba samaki na wameanza kuoza, unapata nini pakacha ikivuja?’
‘Una maana gani?’
‘Sasa kodi zetu wananchi zinatumika kutuzuia sisi wananchi tusiweze kupinga matumizi mabaya ya kodi zetu wananchi.’
Watu wakacheka.
‘Mnacheka nini? Miaka yote hii tunaambiwa kwamba
hakuna fedha za kuboresha jeshi la ndani. Hawawezi kujengewa nyumba
bora, hakuna hata fedha za kununua karatasi za kuandika maelezo sembuse
gari linalofanya kazi na petroli ya kutosha. Ghafla vitu vyote hivi
vipo, tueleweje? Hakuna fedha za kuwakamata wezi na mafisadi, lakini za
kutupiga kichwani zipo za kutosha. Mwisho tutaanza kupigwa kwa kukataa
kutoa rushwa, eti ni kutotii amri halali bila shuruti.’
Watu wakacheka hata kama yule alinuna. Mwingine aliamua kubadili mada.
‘Lakini tusiwalaumu sana ndugu zetu wenye rungu ya
dola. Hayo yote ni matokeo ya kuchakachua mchakato laivu. Kwa kuwa
wameanza kuburuta, lazima waburute hadi mwisho.’
‘Kweli kabisa. Lakini ni wajanja pia, maana naona
katiba sasa imekuwa dili ya uchaguzi. Wakati wa uchafuzi mkuu, watu
wanaahidi hili au lile, badala ya kuongelea sera kiasi kwamba imebidi
kuweka watu kukusanya ahadi zote zinazotolewa kila mahali. Sasa ni
katiba. Hawa wa bangi maalumu ambao walichaguliwa hapo awali kwa
kutotaka katiba, sasa wanasikiliza kila kikundi na kuweka maneno matamu
yanayowahusu ili mradi wajenge uhalali wa kubomoa rasimu na kuweka ya
kwao.’
‘Kabisa. Bado nauliza ni wajenzi wa aina gani
wanaohangaika kurembesha paa wakati misingi haina nguvu. Hawajaona
yaliyotokea huko Nigeria. Kupandisha jengo, hata likiwa jengo zuri namna
gani, juu ya misingi mibovu ni kukaribisha janga, mporomoko na vifo vya
watu. Hata ukiwa mtabiri namna gani au ukiwa umevimbiwa na kutawala
miaka yote hii, jengo ni jengo na misingi yake haiwezi kupuuzwa.’
‘Na ahadi hizi za kutuhadaa ni duni kabisa, maana wamebomoa misingi kwa hiyo nakshi za juu ni sura tu ya kutudanganya.
Hapo kijana mmoja alibisha.
‘Si kweli. Sisi vijana tunashukuru. Hii rasumu mpya …’
‘Rasimu Bwana …’
‘Sumu … simu yote hali moja. Rasumu hii ni kiboko. Unaona hatimaye tumepata hata baraza la vijana.’
‘Ohoo mwenzangu, unaona unavyodanganyika kirahisi.
Suala si kuona kama hiki au kile kimepachikwa. Yale mambo ya msingi
mbona yameondolewa.’
‘Lakini wameweka na ardhi pia.’
‘Kwani ardhi isingekuwepo? Chini ya mapendekezo ya Serikali tatu, ardhi ingekuwepo kwenye Katiba ya Tanganyika.’
Mama mmoja naye aliingia.
‘Hapana, lazima tushukuru,maana hata mambo ya jinsia yameingia.’
‘Mmh, nyinyi kinamama mmeshasahau wakati wa
mapambano ya Sera na Sheria ya Ardhi. Wengine walipigania kwanza ardhi
ibaki mali ya Watanzania, wakati wengine walitaka tu kuhakikisha kwamba
mwanamke ana haki ya ardhi. Tukawauliza, haki ya ardhi ya nini iwapo
ardhi imechukuliwa na wawekezaji. Si mwanamume, si mwanamke atapata
kitu. Linda mambo ya msingi kwanza. Na watu wakajenga umoja sana hadi
Serikali ikaona kuna hatari ya kushindwa, ndiyo maana walibadilisha
sheria kusema kwamba wanawake wanaweza kumiliki ardhi. Basi wanawake
wengi walihamia upande wa Serikali na ardhi yetu ikazidi kuchukuliwa na
wawekezaji. Angalia huko Loliondo, angalia mashamba ya jatropha.’
‘Lakini hii rasumu mpya sasa inalinda ardhi …’
‘Naona hunielewi kabisa. Sawa wamesema. Lakini
hayo yote ni kutufanya kukubali rasumu yao kama unavyoiita. Vijana
wafurahie baraza lao, wanawake wafurahie kwamba jinsia ipo ili mradi
kila mtu akubali kwamba yale ya msingi si ya msingi tena. ‘
‘Lakini ni mapendekezo mazuri.’
‘Nani anabisha. Suala ni kwamba bila kuangalia
yale ya msingi wa uhusiano wetu kitaifa na uwezo wa kuwajibisha viongozi
wetu na mamlaka yetu sisi wananchi, hayo mengine ni pipi tu.’
‘Duh, we angalia Bwana maana unavyowashwa na hii
rasumu, mwisho utakuta unajikuna selo sasa. Hujui kwamba sasa
tunatawaliwa kimabavu kabisa. Hatuna hiari tena, ni shuruti tu.’
Wakati anaongea hivi, tukasikia ving’ora kwa mbali. Kila mtu alisambaratika bila kuangalia nyuma.
Chapisha Maoni