Serikali Yajibu hoja ya Ukosefu wa Ajira Nchini.Yatumia Mawaziri wanne kujibu Mapigo, yawataka wapinzani kuacha Uchonganishi
SERIKALI imetoa ufafanuzi kuhusu tatizo la ajira nchini, huku wanasiasa waliozungumzia tatizo hilo kuwa ni bomu, wakitakiwa kutoa ushauri wa namna ya kulitegua au kupunguza athari zake kama likilipuka.
Mbali
na ushauri huo, Serikali pia imewataka wanasiasa wanaotumia tatizo hilo
kisiasa, kuonesha mfano wa kusaidia vijana katika majimbo yao kwanza,
badala ya kusubiri siku wakipewa nchi.
Mawaziri
wanne walitumia muda wao jana kujibu hoja hiyo, ambayo ni hoja lulu
kisiasa, kutokana na hali halisi kuwa sehemu kubwa ya Watanzania ni
vijana, hivyo inatazamwa na wanasiasa wengi kuwa ndio watakuwa sehemu
kubwa ya wapiga kura.
Kutokana
na umuhimu wa ajira katika siasa za leo, Naibu Spika, Job Ndugai hivi
karibuni alisema Mtanzania mwenye nia ya kugombea urais mwaka 2015, ili
aeleweke kwa wananchi, ni lazima aeleze mikakati ya kuwasaidia vijana
kupata ajira.
“Ajira
ni tatizo kubwa na lazima lishughulikiwe. Kuna vijana hawaendi shule,
lazima watazamwe. Kuna wanaomaliza darasa la saba, kidato cha nne, cha
sita na vyuo vikuu.
"Nazungumza
kutoka moyoni kabisa. Hizi ni dakika za mwisho za Serikali ya Awamu ya
Nne, wale wanaojipanga kwa Awamu ya Tano kama hawataongelea ajira, basi
waandike wameumia,” alisema Ndugai.
Alianza
Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudentia Kabaka, ambaye alikiri kuwa ajira ni
tatizo, lakini akafafanua kuwa si la Tanzania tu, bali pia ni tatizo la
kimataifa.
Alisema
katika utafiti uliofanyika mwaka 2012, ilionekana ajira ya muda mrefu,
inayompa mwajiriwa hifadhi kuwa imeongezeka kwa asilimia 13.5. Ongezeko
hilo limetolewa katika sekta ya umma, ambayo imetoa asilimia 35.8 ya
ajira huku sekta binafsi ikitoa asilimia 64.2 ya ajira.
Kutokana
na mchango mkubwa wa sekta binafsi katika ajira, Kabaka alisema
Serikali imekuwa ikiweka mazingira rafiki kwa wawekezaji, ikiwemo ujenzi
wa barabara, kuboresha upatikanaji wa nishati ya umeme na mawasiliano.
Alisema
wakati wanasiasa wanasema Tanzania kuna tatizo kubwa la ajira, ambalo
kitakwimu ni asilimia 11.7, nchini Afrika Kusini ni asilimia 24.9.
“Sasa
kabla ya kusema ukipewa nchi utatoa ajira, tuoneshe kwanza katika jimbo
lako. Umefanyaje kuongeza ajira katika sekta isiyo rasmi…msidanganye
wananchi na kuwachonganisha na Serikali,” alisema.
Kuhusu
fursa ya kufanya mafunzo kwa vitendo, Serikali imezungumza na Chama cha
Waajiri (ATE) ili watoe fursa hizo kwa wanafunzi wanaotoka katika vyuo
mbalimbali.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Asiye na Wizara Maalumu, Profesa Mark Mwandosya, aliamua kuonesha mfano kwa kuanza kutoa ushauri.
Alitoa
hatua kumi, alizotaka waajiriwa watarajiwa walio katika soko ambao
hawajapata ajira na walio vyuoni na wanaojiandaa kujiunga na vyuo
mbalimbali, ili wapate ajira.
Kwanza aliwataka wanafunzi wanaojiunga na vyuo, kama wanataka kuajiriwa, wachukue fani za sayansi, teknolojia na uhandisi.
Pili, aliwataka wanaosomea uhandisi na sayansi, wachanganye fani hiyo na fani ya usimamizi wa biashara.
Tatu, aliwataka wanaochukua fani za sanaa, pia kuchukua fani za usimamizi, kwa maana ya Shahada ya Uzamili ya Usimamizi (MBA).
Tatu, aliwataka wanaochukua fani za sanaa, pia kuchukua fani za usimamizi, kwa maana ya Shahada ya Uzamili ya Usimamizi (MBA).
Profesa
Mwandosya pia aliwataka waajiriwa watarajiwa, wasidharau lugha za
Kiswahili na Kiingereza ;na wazizungumze kwa ufasaha, lakini akawataka
pia kuchukua lugha moja katika ya Kifaransa, Kihispania, Kireno na
Kichina.
Hatua
nyingine waliyoshauriwa kuchukua ni kutoogopa kushindana katika soka la
nje, ikiwemo soko la Afrika Mashariki, Afrika na sehemu nyingine
duniani. Kwa mujibu wa Profesa Mwandosya, katika soko hilo la ajira kuna
Wakenya, Warwanda na Waganda.
Aliwataka
wanafunzi vyuoni kuanza kujijengea kichwani dhana ya kujiajiri, kwa
kuwa ni jambo zuri ili wasingoje kupata ajira za Serikali.
Wasomi
hao pia walitakiwa waache kuchagua kazi wala ngazi ya kuanzia kazi, kwa
kuwa hata aliyesomea uhandisi akianzia kazi ya fundi mchundo, atapanda
haraka. Pia, aliwataka wajiamini, wawe wabunifu na kujiunga katika
vikundi ili wawezeshwe.
Chapisha Maoni