Polisi Yatangaza Msako Mkali kwa watu waliomuu Sista wa Kanisa Katoliki....Msako huo utahusisha Traffiki Wote,Askari wa doria, Wapelelezi na Askari wa kawaida
POLISI Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imeanzisha msako mkali, kuwatafuta watu waliohusika na mauaji ya Mhasibu wa Kanisa Katoliki Parokia ya Makoka jijini Dar es Salaam, Sista Cresencia Kapuri (50), ambao utahusisha vikosi vyote vya Polisi. Vikosi hivyo ni Usalama Barabarani, askari wa doria wanaotumia pikipiki na magari, wapelelezi na askari Polisi wa kawaida.
Mauaji
ya mtawa huyo, yalitokea juzi mchana katika eneo la Ubungo Riverside,
jijini humo, ambapo alipigwa risasi na watu wanaodaiwa kuwa ni majambazi
na kumpora Sh milioni 20 pamoja na nyaraka mbalimbali za ofisi.
Kamanda
wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Mkoa wa Dar es Salaam, Suleiman Kova,
aliwaambia waandishi wa habari ofisi kwake jana kuwa Sista Cresencia
wakati anapigwa risasi, alikuwa ameongozana na wenzake, ambao ni Sista
Brigita Mbaga (32) na dereva wao Mark Mwarabu, aliyekuwa akiendesha gari
aina ya Toyota Hilux Pick-Up, yenye namba T213 CJZ.
Kova
alisema wakati watawa hao, wakitoka katika Benki ya CRDB Tawi la
Mlimani City, walipofika Ubungo Riverside kulipa deni la chakula katika
duka la Thomas Francis, ndipo walitokea watu hao wawili wanaodaiwa kuwa
ni majambazi wakiwa na pikipiki, ambayo haikusomeka namba, huku mmoja
akiwa na bunduki aina ya SMG.
“Yule
dereva wa gari la masista walimpiga risasi katika kidole gumba cha
mkono wa kulia na kisha kumpiga mtawa huyo risasi ya kifuani na kupora
kiasi hicho cha fedha na nyaraka hizo,” alisema Kova.
Alisema
kuwa jambo kubwa walilogundua ni kuwa matukio mengi ya ujambazi, hasa
unaohusisha wananchi kuporwa kiasi kikubwa cha fedha, yanaanzia katika
mabenki, hivyo kuna uwezekano wa watu ambao si waaminifu, wanafanya
uhalifu huo.
Alisema kuwa katika matukio ya aina hiyo, majambazi huwafuatilia wateja wanapoingia au kutoka katika benki mbalimbali.
Alisema
imeonekana kwamba mara nyingi benki, zinapohitaji kusafirisha pesa
nyingi, hutumia askari au taasisi nyingine za usalama kusafirisha fedha
zao.
“Tunawaomba
mameneja wa benki zote, kuhakikisha wanawahimiza wateja wake kutumia
njia mbadala za kusafirisha pesa nyingi, kama vile matumizi ya hundi,
kufanya miamala bila kadi, matumizi ya kadi za kutolea fedha (ATM) na
njia nyingine ambazo ni salama.
“Matukio
kama haya, yanaonesha ni wazi huu utaratibu wa watu kutoa pesa nyingi
kutoka benki na kwenda kufanya malipo si salama. Kuna baadhi ya huduma,
kwa mfano kuna baadhi ya nchi ambazo ni sheria mtu haruhusiwi kutembea
na fedha nyingi, kwa hiyo ni muhimu kwa sisi wenyewe tukajielewa
kwanza,” alisema Kova.
Alisema
pia wanaomba mameneja wa benki, kuhakikisha benki zao zinakuwa na
kitengo maalumu cha ushauri wa masuala ya usalama kwa wateja wao.
Alifafanua
kuwa kama mteja atafika katika benki zao na akahitaji kutoa fedha
nyingi ni vyema wakamshauri ;na kama atakaidi, benki ichukue hatua ya
kutaarifu Polisi.
Aidha,
alitaka wafanyabiashara na taasisi mbalimbali, zisitumie njia za mkato
katika usafirishaji na uhifadhi wa pesa zao kwa faida ya usalama wa
maisha na mali zao.
Aidha,
Kova alisema katika kukabiliana na uhalifu wa aina hiyo wa kutumia
pikipiki, wamezikamata pikipiki 668, ambazo wanazitilia shaka na
wanazifanyia ukaguzi zaidi. Pia, zipo ambazo zimekamatwa kuhusiana na
makosa mengine ya barabarani.
Chapisha Maoni