Shuhuda asimulia mwenzao alivyouawa kwa bomu Zanzibar
Siku moja baada ya mlipuko wa kitu kinachosadikiwa kuwa ni bomu na kusababisha kifo na kujeruhi watu saba eneo la Darajani mjini Unguja, mmoja wa majeruhi ameelezea jinsi mwenzao alivyouawa wakati wakisubiri daladala baada ya kutoka kuswali msikitini.
Shuhuda
huyo, Khalid Ahmed amesema mwenzao alipigwa kwa kitu kinachosadikiwa ni
bomu kilichorushwa na kutua mwilini na kufa papo hapo huku wengine
wakijeruhiwa.
Tukio
hilo limethibitishwa na Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya
Jinai, Kamishna Yussuf Ilembo na kumtaja marehemu kuwa ni Muhammad
Khatib Mkombalaguha (26), Msambaa na mkazi wa Tanga ambaye alikufa papo
hapo.
Aidha,
kutokana na tukio hilo, Jeshi la Polisi limewatangazia hali ya hatari
wahusika, huku uchunguzi ukianzia kwenye mabaki ya vitu vilivyokutwa
katika eneo la tukio.
Akielezea
tukio hilo, Ilembo alisema mtu aliyekufa na wengine waliojeruhiwa,
walikuwa wametoka Msikiti wa Darajani baada ya Ibada ya Swala ya Isha
inayoswaliwa kuanzia saa 1:45 usiku na kuendelea, lakini huishia kabla
ya swala ya alfajiri. Mbali ya Ibada, pia walitoa mawaidha msikitini.
Alisema
mara baada ya kumaliza ibada hiyo walitoka msikitini na kufika eneo la
Darajani wakisubiri gari na ndipo mlipuko mkubwa uliposikika ambao
unasadikiwa kuwa ni bomu na kuwajeruhi saba na wanane kufa papo hapo.
“Jeshi
la Polisi linaendelea na uchunguzi zaidi wa tukio hilo ambalo limezusha
taharuki kubwa kwa wananchi wa Zanzibar katika kipindi hiki kumekuwepo
na ugeni wa watu mbalimbali,” alisema.
Katika
hatua za kwanza za upelelezi, Ilembo alisema wamekusanya baadhi ya
vielelezo ikiwemo vipande vya mabaki ya gundi ya karatasi (solar tape)
na vitu vingine ambavyo vinasadikiwa vimetumika kwa ajili ya kutengeneza
bomu hilo.
Pia
katika mlipuko huo, magari mawili, moja aina ya Toyota Land Cruiser
lenye namba za usajili Z 675 na jingine aina ya Toyota IST lenye namba
za usajili Z 268 yaliharibiwa kwa kuvunjwa vioo na matairi yake
kupasuka.
Katika
ajali hiyo waliojeruhiwa na kulazwa katika hospitali ni Hamad Nassor
Kassim (46), ambaye ameumia kichwa, Khalid Ahmed Haidar (16), Ahmed
Haidar Jabir Alfarsy (47) ambao wamelazwa katika Hospitali ya Al-Rahma.
Wengine ni Suleiman Ali Juma (21) amelazwa katika Hospitali ya Al-Rahma
huku Kassim Issa Muhammad akiruhusiwa baada ya kupata matibabu.
Naye
Ahmed ambaye ni mmoja ya mashuhuda wa ajali hiyo, alisema kitu hicho
kinachosadikiwa kuwa ni bomu kilirushwa kwa mkono na kumpata moja kwa
moja Mkombalaguha na baadaye kuwajeruhi watu wengine.
“Bomu
lile linaonekana moja kwa moja kuwa ni la kurushwa kwa mkono kwa sababu
lilimfikia mwilini marehemu na baadaye kutuathiri wengine,” alisema.
Mji
wa Zanzibar wiki hii umekuwa na ugeni mkubwa kutoka nchi mbali mbali za
Afrika ya Mashariki wakihudhuria ibada ya Kiislamu ya Ijitimai
inayofanyika huko Fuoni.
Aidha,
wageni mbalimbali wanahudhuria Tamasha la Filamu la Kimataifa la
Zanzibar (ZIFF) ambalo huwakutanisha wageni kutoka sehemu mbalimbali
duniani.
Chapisha Maoni