HOME
Aibu ya samaki wa Magufuli iwe funzo gani kwetu
Wakati Waziri wa Mifugo na Uvuvi (wakati ule),
Dk John Magufuli alipokamata meli yenye jina la Tawaliq 1 mwaka 2009,
ilionekana kama vile tumepiga hatua kubwa katika kulinda rasilimali
zetu. Iikuwa ni kazi nzuri aliyoifanya Dk Magufuli (sasa Waziri wa
Ujenzi) mara baada tu ya kuhamishiwa wizara ile ya vitoweo, lakini sasa
kesi hiyo imetupwa na Serikali inatakiwa iwarejeshee Wachina hao pasi
zao za kusafiria na meli yao inayokadiriwa kuwa na thamani ya Sh3.3
bilioni.
Meli hiyo iliyokuwa na tani 293 za samaki aina ya
jodari waliovuliwa katika ukanda wa kiuchumi wa Tanzania bila kibali,
sasa imeshazama baada kukatwa mabati yake na kuibwa vifaa huku Serikali
ikigawa bure shehena ya samaki hao.
Hapa ndiyo najiuliza naomba wanasheria wanisaidie.
Ilikuwaje watu waliovua samaki kwenye eneo la Tanzania bila kibali, leo
hawana kesi ya kujibu?
Miaka yote mitano waliyokamatwa, wanasheria wa Serikali hawakujua kwamba hakuna kesi?
Hayo tisa, kumi ni ile meli waliyokamatwa nayo iko
wapi? Maana yake ni kwamba sasa Serikali imepoteza kesi, halafu ilipe
Sh3.3 bilioni? Hii ni kashfa kubwa mno kwa Serikali na inaniwia vigumu
mno kuamini umakini wa Serikali yetu.
Hii siyo kesi ya kwanza ya Serikali kupoteza,
kwani ni mwaka huu tu Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato (TRA) ilipoteza
kesi dhidi ya Kampuni ya Atom Red Met Zoloto (ARMZ) ya Urusi
inayokusudia kuchimba madini ya urani nchini siku za usoni.
Baada ya kupoteza katika kesi hiyo, TRA walikosa
Sh340 bilioni za kodi ya ongezeko la mtaji. Yaani, kama nchi tumepoteza
kiasi hicho cha fedha wakati madini ni yetu, na yalishagunduliwa na
Serikali tangu miaka ya 1970, kisha leseni ya ugunduzi wa madini hayo
ikapewa kampuni ya kigeni kwa bei ya kutupa.
Hapohapo kuna zaidi ya Sh200 bilioni zimepotelea
kwenye sakata jingine la IPTL ambapo viongozi wetu wanadai siyo za
Serikali huku upande mwingine ukidai ni za Serikali.
Ilimradi tu kila siku Serikali inapoteza mabilioni ya fedha, iwe ni kwenye kesi au wizi. Yaani, nchi hii imekuwa ya wapiga dili.
Watendaji wengi wa Serikali siyo waaminifu, kibaya
zaidi hakuna wa kuwawajibisha. Kwa upande mwingine wapo watendaji
wengine waaminifu, ila hata wakitoa ushauri kwa Serikali haufuatwi.
Hata ukifuatilia miradi mingi ya maendeleo utakuta
fedha zinazotumiwa ni za wafadhili, siyo fedha za Serikali, wakati kuna
uwezekano mkubwa tu wa kuzalisha fedha nyingi na zikaingizwa kwenye
miradi ya maendeleo.
Kwa ufupi, nchi yetu inaelekea kubaya. Tunaweza
kujifariji tu kwa maendeleo kidogo tunayoyaona tena kwa fedha za
misaada, lakini uhalisia ni kwamba hali tuliyonayo kama Taifa ni mbaya
na inatia aibu.
Yote haya yanasababishwa na kukosekana kwa uadilifu hasa kwa watendaji wa Serikali.
Viongozi walio wengi wanapopata fursa badala ya
kuangalia masilahi ya Taifa, wanaangalia manufaa yao na kuhakikisha
wanabadili maisha yao na siyo ya wananchi.
Ni jukumu la watendaji wa Serikali sasa kurejesha uadilifu huu, vinginevyo nchi yetu inazama na kupotea kabisa.
Chapisha Maoni