HOME
Warioba: Msikurupuke kupitisha Katiba Mpya
Bunda. Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amewataka Watanzania
kutokurupuka kuipitisha Katiba Inayopendekezwa kwa kuwa imeyaacha kando
maoni yao mengi na akawataka waisome kwa makini kabla ya kuikubali au
kuikataa.
Akiwa katika likizo ya wiki moja nyumbani kwake
Bunda, Mkoa wa Mara, Jaji Warioba alialikwa na vijana wa mji huo kupitia
Jukwaa lao la Uwazi na Fikra Yakinifu, wakiomba azungumze nao kuhusu
masuala mbalimbali hasa mchakato wa Katiba Mpya.
Katika mkutano huo uliofanyika katika Hoteli ya
Harrieth, Jaji Warioba aliulizwa na kujibu maswali; anaionaje Katiba
Inayopendekezwa na iwapo CCM imemgeuka kwa nini asihame chama?
Akijibu maswali hayo, Jaji Warioba alisema Katiba
hiyo haina maoni yote ya wananchi kama Bunge Maalumu lilivyojinadi, bali
yamewekwa machache ambayo hata hivyo yamo hata katika Katiba ya sasa.
Mathalan, alisema wananchi wengi walipendekeza
kiwepo kipengele cha maadili ya viongozi ili kuwadhibiti dhidi ya
vitendo viovu wanavyovifanya kwa sasa kama ufisadi, rushwa na matumizi
mabaya ya madaraka, lakini wajumbe wa Bunge walikirekebishana hadi
kikapoteza maana.
Kwa kufanya hivyo, alisema wajumbe hao walionyesha
wanafurahishwa na hali iliyopo ya viongozi kukosa uzalendo, uadilifu na
kukosa uwajibikaji hata kuwasababishia Watanzania maisha magumu ambayo
kupitia maoni yao, walikuwa wameyatafutia dawa kwa kupendekeza maadili
yatambulike kikatiba.
Alisema wananchi walipendekeza muundo wa muungano
wa serikali tatu ili kuondoa matatizo yaliyopo, kupatiwa madaraka ya
kuwawajibisha wabunge wao pamoja na rais kupunguziwa madaraka, mambo
ambayo yameondolewa na Bunge hilo Maalumu.
“Kazi yetu kama Tume ya kuandaa Katiba ya
Watanzania tuliimaliza. Bunge nalo limemaliza kazi yake japo ina
upungufu. Sasa kazi imebaki kwenu wenye Katiba; kuisoma iliyopendekezwa
kwa makini kabla ya kuipigia kura,” alisema Warioba.
Jaji Warioba alieleza kusikitishwa na taarifa
iliyotolewa na Mwenyekiti wa lililokuwa Bunge la Katiba, Samuel Sitta
siku ya kukabidhi Katiba Inayopendekezwa kwa Rais, kwamba Bunge hilo
limeweka ndani ya katiba hiyo asilimia 81 ya maoni ya Tume, akisema huo
ni uongo mkubwa.
“Ukweli ni kwamba wamechukua asilimia 20 tu na
kutupa nje asilimia iliyobaki na kubandika yaliyomo katika Katiba ya
sasa ambayo hayawezi kuleta mabadiliko yoyote,” alisema Jaji Warioba.
Hivyo, Jaji Warioba aliwataka Watanzania kwa umoja
wao bila kujali tofauti zao za kisiasa, dini, rangi, kabila kuhakikisha
kuwa wanapata Katiba Inayopendekezwa na kutumia muda mwingi kuisoma
kabla ya kuipigia kura na kuwa wakikurupuka watajuta siku za usoni.
Akizungumzia hatima ya Muungano wa serikali mbili
uliopo kwa sasa, Warioba alisema hachelei kusema kwamba huenda
ukakumbana na changamoto nyingi siku za usoni iwapo wananchi watauridhia
kupitia kura yao kwa vile asilimia kubwa ya Wazanzibari hawaukubali.
“Hapa napo kuna tatizo, Mpaka mgogoro uliopo miongoni mwa
Wazanzibari umalizwe. Wao wenyewe wanataka kuendeleza tamaduni zao ndani
ya Zanzibar wanayoitambua kama nchi huru. Sidhani kama watakubaliana,”
alisema Warioba.
Kuhusu kujitoa CCM, Jaji Warioba alisema hawezi
kufanya hivyo, bali ataendelea kuwa mwanaCCM daima kwani anaamini katika
chama hicho lakini akawaponda wanachama wenzake aliosema wanaweka
masilahi binafsi mbele badala yale ya wananchi.
“Mimi ni mwanaCCM na nitadumu hivyo daima kwani
ndicho chama ninachokiamini. Mimi siyo mwanachama masilahi ambaye
akikosa kitu fulani au akiguswa kidogo tu anahamia chama kingine,”
alisema Jaji Warioba.
Unataka niwe nakujuza kila kinachonifikia?usijali mimi niko tayari lakini kama haujalike page zetu za facebook na twitter nakuomba like kwa kubonyeza hapa>>>Facebook>>>Twitter
Unataka niwe nakujuza kila kinachonifikia?usijali mimi niko tayari lakini kama haujalike page zetu za facebook na twitter nakuomba like kwa kubonyeza hapa>>>Facebook>>>Twitter
Chapisha Maoni