HOME
Historia ya Serikali za Mitaa- 3
Wiki iliyopita katika kona hii tulikuwa na
sehemu ya pili ya historia ya Serikali za Mitaa Tanzania. Leo
tunaendelea na mfululizo wa makala ile.
Tatizo la pili kubwa lililokuwa linazikabili
Serikali za Mitaa ni ukosefu wa uongozi imara na watendaji wenye uwezo.
Baada tu ya uhuru.
Serikali ya wananchi ilikuja na mfumo wa
“Africanisation” yaani Waafrika kupewa madaraka serikalini. Kwa baadhi
ilikuwa kama “Asante” kwa kushiriki katika harakati za kupigania uhuru.
Hii ilimaanisha kwamba maofisa tawala waliokuwa na
uzoefu katika masuala ya Serikali za Mitaa tangu wakati wa mkoloni,
walihamishiwa katika Serikali Kuu.
Dosari nyingine ilikuwa ya kuwapa wanasiasa
madaraka ya watendaji. Kwa mfano, katika Halmashauri za Wilaya,
wenyeviti wa Tanu walikuwa vilevile wenyeviti wa halmashauri zao na kwa
halmashauri za miji na manispaa walikuwa ndiyo mameya.
Walikuwepo madiwani wa kuteuliwa
Hii ina maana kwamba wengi kati ya hao walikuwa
wakithamini zaidi nafasi zao katika chama tawala. Katika hali hii baadhi
yao hawakuweza kuwa viongozi imara wa kuwawakilisha vizuri wananchi
katika halmashauri.
Mambo yafuatayo yalijitokeza kudhihirisha udhaifu wa madiwani wengi wa wakati huo:
Madiwani hawakuwa tayari kutekeleza kikamilifu
majukumu yao, hasa kusimamia ukusanyi wa kodi, kwa kuhofia kutochaguliwa
katika uchaguzi ujao.
Walijiongezea vikao ili waweze kujipatia
marupurupu zaidi; wengi wao walipenda kuingilia kazi za watendaji bila
ya kufuata taratibu na kanuni zilizowekwa.
Wenyeviti wa halmashauri, ambao walikuwa na kofia
mbili, walikuwa wakitaka wapewe marupurupu maalumu kama vile ofisi,
gari, mhudumu mambo ambayo yalikuwa kinyume na utaratibu.
Tenda zilikuwa zinatolewa kwa kuzingatia zaidi masilahi binafsi
ya madiwani na watendaji na wengi wao wengi walikuwa wakila njama na
baadhi ya watendaji kwa nia ya kulinda na kutetea masilahi yao binafsi
wakati wa vikao halali.
Kwa ujumla madiwani wengi hawakuelewa majukumu yao wakati wanaingia marakani.
Serikali Kuu haikusimamia kwa umakini ukaguzi na
udhibiti wa shughuli za Serikali za Mitaa. Suala muhimu zaidi katika
kipengele hiki ni kuvunjwa kwa Serikali za Mitaa mwaka 1972.
Juni 30, 1972 halmashauri 60 za wilaya zilivunjwa
na zile za miji zilivunjwa mwaka mmoja baadaye. Sababu kuu tano
zilisabisha Serikali Kuu kuamua kuzivunja Serikali za Mitaa.
Halmashauri hazikuwa na uwezo wa kifedha
kugharamia majukumu yake kwa ufanisi na Serikali Kuu ilishindwa kukagua
na kudhibiti kwa ukamilifu Serikali za Mitaa.
Kwa ujumla utendaji katika halmashauri haukuwa wa
kuridhisha kwani vitendo vya rushwa vilishamiri na baada ya Serikali Kuu
kuchukua baadhi ya majukumu yaliyokuwa mikononi mwa Serikali za Mitaa,
ilionekana kwamba hazikuwa muhimu.
Madaraka mikoani
Baada ya kuzifufua Serikali za Mitaa mwaka 1972, Serikali Kuu ilianzisha utaratibu wa madaraka mikoani.
Madaraka mikoani ilikuwa na maana ya uhamishaji wa
mamlaka kutoka makao makuu ya Serikali na kuwapa maofisa wake katika
ofisi za mikoani.
Sababu ya utaratibu huo ilikuwa kuongeza
ushirikishwaji wa wananchi katika uamuzi pia kuongeza nguvu na madaraka
ya wawakilishi wao.
Utaratibu huu ulipokewa kwa hisia tofauti. Kwanza,
haikuwa rahisi kuona uwezekano wa nguvu na madaraka ya wawakilishi wa
wananchi yakiongezeka juu ya watendaji wao ambao hawakuwa na uwezo wa
kuwaajiri. Baadhi ya maofisa walikuwa na madaraka makubwa pia mishahara
mikubwa.
Kwa mfano Mkurugenzi wa Mkoa (RDD) alilinganishwa
na Katibu Mkuu wa Wizara, Ofisa Mipango, Ofisa Utumishi na Mdhibiti wa
Fedha nao walipewa mishahara mikubwa. Hali hii ilisababisha manung’uniko
kwa baadhi ya watendaji wa mikoani na wilayani.
Kutokana na maandalizi hafifu, watendaji waliteuliwa haraka
haraka bila ya kuzingatia sifa zao kwa makini. Wengi waliandaliwa
kupitia semina fupi za wiki moja au mbili.
Kwa bahati mbaya wengi wa watendaji wa halmashauri
zilizovunjwa hawakuajiriwa katika utaratibu wa madaraka mikoani. Dosari
katika utendaji zilionekana tangu awali.
Kwa mfano, katika sehemu nyingi hati za
makabidhiano hazikutayarishwa na pale zilipotayarishwa, watendaji wa
madaraka mikoani hawakuzifuatilia. Hali hii ilisababisha upotevu wa mali
na fedha nyingi za Serikali.
Kwa sababu madaraka yalibakia zaidi mikononi mwa watendaji wakuu, hali ya utoaji huduma za jamii ilizorota.
Utekelezaji wa Mpango wa Vijiji vya Ujamaa
uliotekelezwa kati ya mwaka 1972 na 1975 chini ya madaraka mikoani
ulikuwa na kasoro nyingi.
Itaendelea Jumatano ijayo
Chapisha Maoni