HOME
Kura ya Meghji yazua utata mpya
Dar es Salaam. Suala la Mjumbe
wa lililokuwa Bunge Maalumu la Katiba, Zakia Meghji kupiga kura upande
wa Zanzibar wakati wa kupitisha Katiba Inayopendekezwa, limechukua sura
mpya baada ya uliokuwa uongozi wa Bunge hilo kusema, “hakuna sehemu
yoyote iliyobainisha kwamba alikuwa mjumbe kutoka Bara.”
Utata wa kura ya Meghji uliibuliwa na Mwenyekiti
wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Deus Kibamba ambaye alisema
mjumbe huyo alitakiwa kupiga kura upande wa Bara kutokana na Tangazo la
Gazeti la Serikali namba 29 la Februari 7, mwaka huu lililomtambulisha
Meghji kama mjumbe kutoka Tanzania Bara lakini katika upigaji kura
alipiga upande wa Zanzibar.
Hatua ya mjumbe huyo kupiga kura upande huo wa
muungano inachukuliwa na baadhi ya wanaopinga mchakato wa Katiba Mpya
kama moja ya mbinu zilizotumiwa na uongozi wa Bunge Maalumu kulazimisha
upatikanaji wa theluthi mbili ya kura kutoka visiwani ili kupitisha
Katiba.
Hata hivyo, Naibu Katibu wa Bunge hilo, Dk Thomas
Kashililah alisema jana kuwa: “Mnajichanganya tu, katika hilo tangazo la
Serikali halikubainisha kwamba Meghji ni mjumbe wa Bara sisi
tulichoangalia ni originality (asili) yake ni wapi hata kama anaishi
Bara,” alisema Dk Kashililah na kuongeza: “Kama ndiyo hivyo, mbona Hamad
Rashid anaishi Bara lakini asili yake ni Zanzibar? Mbona hilo
hamuulizi? Hapo hakuna hoja kama wanatafuta kitu hicho hakipo.
“Katika Bunge hilo kulikuwa na wajumbe wa Baraza
la Wawakilishi, wajumbe 201 na wajumbe kutoka Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania... ieleweke kwamba mjumbe wa Baraza la Wawakilishi
anaweza kuingia Bunge la Jamhuri lakini wa Jamhuri hawezi kuingia Baraza
la Wawakilishi.”
Muda mrefu ambao Meghji amekaa Bara anaweza
kufananishwa na ule ambao Mbunge wa Dole (CCM), Sylivester Maselle
Mabumba ameishi Zanzibar lakini wakati akipiga kura kupitisha Katiba,
asili ya Mabumba ambayo ni Bara haikuzingatiwa.
Taarifa katika tovuti ya Bunge zinaonyesha kuwa
Mabumba alihitimu elimu yake ya msingi katika Shule ya Langoni, Dole –
Zanzibar mwaka 1983 na mpaka sasa amekuwa akiishi Visiwani humo licha ya
kwamba ni mzaliwa wa Kahama, Shinyanga.
Meghji alipopigiwa simu kuzungumzia suala hili,
baada ya mwandishi kujitambulisha kwake alisema: “Unasema unaitwa nani,
unasemaje”, kisha simu ikakatika na alipopigiwa tena alipokea lakini
ilisikika sauti ikisema hasikii na alipotumiwa ujumbe wa maandishi
hakujibu.
Asili yake
Mjumbe huyo ni mmoja wa wabunge wa kuteuliwa na
Rais katika Bunge la Jamhuri ya Muungano na hakuna taarifa zozote
zilizoambatana na uteuzi wake kuhusu ni upande upi wa muungano
anakotoka. Taarifa rasmi zinaonyesha kuwa amekuwa akiishi mkoani
Kilimanjaro ambako 1990 alikuwa mkuu wa mkoa huo, nafasi ambayo aliipata
baada ya kuwa Mkuu wa Wilaya ya Moshi mwishoni mwa miaka ya 1980.
Meghji pia amewahi kushika nyadhifa mbalimbali za
uwaziri akiongoza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa miaka tisa, Wizara
ya Afya kwa miaka minne na Wizara ya Fedha kwa miaka miwili.
Wizara hizo mara kadhaa zimekuwa zikiongozwa na
mawaziri kutoka pande zote mbili za muungano, lakini pia ni nadra kwa
kiongozi kutoka Zanzibar kushika wadhifa wa mkuu wa mkoa na mkuu wa
wilaya upande wa Bara.
Wasemacho wengine
Mratibu wa Mtandao wa Wanaopigania Haki za
Binadamu, Onesmo Ole Ngurumwa alisema kitendo kilichofanywa ni
kuhalalisha uchakachuaji wa Katiba hiyo.
“Kama mtu ameteuliwa kutoka Bara hata kama ni
Mzanzibari atatakiwa kupiga kura kama mtu wa Bara kwani kulikuwa na
maana yake kuteuliwa upande mmoja.”
Mwanasheria Mwandamizi wa Kituo cha Sheria na Haki
za Binadamu (LHRC), Harold Sungusia alisema kuna vitu viwili vinatakiwa
kutazamwa kwa makini; mosi ni uteuzi wake ulikuwa kutoka wapi na
alipiga kura kama mjumbe wa wapi.
“Kama aliteuliwa kama mjumbe wa Tanzania Bara
alitakiwa kupiga kura kama mjumbe wa Bara na kama aliteuliwa mjumbe wa
Zanzibar angepiga kura kama Mzanzibari na si kuangalia asili yake na
hili halina hata haja ya kuumiza kichwa kwani linaeleweka alipoteuliwa
ndipo huko atapigia kura,” alisema Sungusia.
Chapisha Maoni