HOME
Kama tutauenzi Muungano hatuna budi kusema kweli kuulinda
Katiba inayopendekezwa kwa mujibu wa maelekezo
na matakwa ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Sura ya 83 imekwisha
kabidhiwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano Jakaya Kikwete pamoja na Rais
wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) Dk. Ali Mohamed Shein. Sote
tu mashuhuda, wale waliokuwa uwanja wa Jamhuri pale Mji Mkuu Dodoma na
wale tuliokuwa mbele ya runinga zetu, tukifuatilia hatua kwa hatua
katika ratiba ya makabidhiano hayo. Ni kwa hakika tuna Katiba
Inayopendekezwa, nadhani nikianza hivi sitaonekana mbishi, kweli mimi
siyo mbishi, ninafuata sheria, ninatii mamlaka ya nchi na ninawaheshimu
viongozi wangu.
Baada ya kusema hayo nikiri kwamba, ninaipenda
nchi yetu Tanzania, sijaota ndoto ya nchi nyingine bora kuliko Tanzania,
nimezunguka dunia yote, kote kuzuri na kule kwenye changamoto bado
nikiwa kote huko natamani siku ziende nirudi kwetu nyumbani. Ninasema
haya kumaanisha niyafanyayo, sisukumwi na mihemko ya wakati, sisukumwi
na itikadi za vyama vya siasa tena ambavyo kwa kiasi kikubwa ambavyo
vinaendelea kutukwaza Watanzania kwa kuweka mbele maslahi yao na kuacha
nyuma maslahi ya Taifa. Hata kwenye chama ambacho mimi ni mwanachama
wanajua sikubaliani na maelekezo yanayokwenda kinyume na maslahi ya
wananchi. Nifanyacho hakipati maelekezo ya taasisi yoyote, wala mtu
yeyote bali sauti za Watanzania ambao naendelea kuwakumbuka wakitoa
maoni yao. Siamini kwamba tulikwenda kuwahadaa ili tuhalalishe letu,
unajua ugumu ninaoupata hausimuliki, napitia kipindi kigumu na
kinachoambatana na msongo mkubwa wa mawazo.
Kwa kawaida mimi huwa si mtu wa mawazo,
nastahimili majaribu ya wakati lakini kipindi hiki najihoji, ilikuwaje
nikapata bahati mbaya hii? Hili nitaendelea kulisema moyoni mwangu na
kwa watu wangu wa karibu, “aliposema nenda ukajifunze” na akarudia mara
kadhaa tena “unajifunza lakini?” nikajibu kwa woga nikitoa uhakika
kwamba ninafanya kila lililo ndani ya uwezo wangu wa kibinadamu kuelewa
mambo, kuuliza, kusoma, kuongea na kila ambaye anaweza kuwa chanzo na
msingi wa taarifa sahihi, taarifa ziletazo maarifa ya kweli. Ningesema
nizungumze kwa kiingereza kuonyesha msisitizo ningesema “I did all
that”.
Nilikuwa katika kila majadiliano katika Tume ya
Katiba, na siyo vibaya nikisema nilikuwa Katibu wa Kamati ya Muungano,
nilijua taarifa zote za wazi na za siri, nakumbuka maoni yote ya
viongozi walioko madarakani na waliostaafu, nakumbuka sana. Nilikuwa
Katibu wa Kamati ya Wenyeviti wa Kamati zote za Tume ya Katiba,
nakumbuka kazi kubwa walifanya, nakumbuka vikao vyao virefu, vilivyokuwa
vimejaa uzalendo mkubwa wa kutoa mapendekezo ya kutupatia Tanzania Mpya
sasa na kwa miaka 50 ijayo.
Nayasema haya nikiwa mtu mwenye kifua, nayasema
kwa jumla jumla tu ili kujaribu kuonyesha nikisemacho sijaokota kwenye
mkutano wa hadhara, au kongamano la Azaki au kutoka kwa mtu fulani au
taasisi fulani na kwa maslahi fulani. Nikisemacho ni kweli, na ni kweli
tupu, sikufanya mzaha nilipokula kiapo, niliapa kweli mbele ya Mkuu wa
Nchi na Mbele ya Mungu wangu ninayemuamini, na ukijumlisha na kuaswa na
kila mtu wa kila rika, wakiwemo wazazi wangu, pamoja na “maneno yake”.
Suala ni kwamba nasema hayo yote nikiendelea na
tafakuri yangu, kama nikionacho sicho, je, nikae kimya kwasababu kazi
imeshaisha ilhali nikiona dhahiri shahiri imeisha ndivyo sivyo? Unajua
kupitia runinga pale jukwani nilikuwa nawangalia baadhi ya waheshimiwa
ambao walitoa maoni, nayakumbuka maoni yao, na baadaye walibadili
msimamo na wakaunga mkono mambo tofauti na maoni yao. Nikajiuliza,
waheshimiwa wale, furaha yao iko wapi, amani yao iko wapi, uaminifu wao
uko wapi? Nikaendelea kujiuliza au ndiyo uongozi ulivyo? na kudhihirisha
ule usemi usemao “kua uyaone”?
Nakumbuka katika mojawapo ya vikao vya Tume ya
Katiba vya mwishoni kabla ya Tume kuvunjwa, tulikuwa na mjadala mzito,
wajumbe walikuwa wakitafakuri kwa pamoja mapokeo mabaya ya Rasimu Toleo
la Pili hasa miongoni mwa watawala. Kwa uchungu nilisimama na kusema
“kama tumesema uongo katika kazi ya Tume, basi tunapaswa kuhukumiwa
daima, sasa na vizazi vijavyo, na kama tumefanya kazi ambayo wananchi
wametutuma kwa mujibu wa sheria basi tunapaswa kuisimamia, na kusema
ukweli daima”. Nitasema kweli daima juu ya ninachokijua kuhusiana na
Mchakato wa kuandika Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Nitakaa kimya nikisaidiwa majibu ambayo yamejengwa katika hoja na
sababu, kwasababu huo ndiyo ulikuwa msingi wa mjadala wa kupata Katiba
Mpya.
Tofauti ya Rasimu ya Warioba na Katiba Inayopendekezwa
Nijielekeze kwenye maeneo matatu ili kuonyesha tofauti hizi kubwa:
(1) Tunu za Taifa
Rasimu ya Warioba ilipendekeza kuwa Jamhuri ya
Muungano iwe na Tunu zifuatazo (a) utu; (b) uzalendo; (c) uadilifu; (d)
umoja; (e) uwazi; (f) uwajibikaji; na (g) lugha ya Taifa, ambazo sisi
sote kama Taifa tutazienzi na kuzizingatia. Tunu hizi au kwa kiingereza
huitwa “national societal core values” ndiyo ambazo kila Mtanzania
angefanya awezavyo kuzienzi ili kuwa na jamii ya Kitanzania yenye
maadili. Wamefuta yote na kubakisha utu na lugha ya Kiswahili. Najiuliza
hivi kuna utu pasina uadilifu, uwajibukaji, umoja na uzalendo?
(2) Maadili na Miiko ya Viongozi na Watumishi wa Umma
Ibara Mahususi zifuatavyo zimetupiliwa mbali, Zawadi katika
Utumishi wa Umma. Akaunti nje ya nchi na mikopo. Wajibu wa kutangaza
mali na madeni. Mgongano wa maslahi na Matumizi ya mali ya umma kwa
uchache katika eneo la Maadili na Miiko ya viongozi na watumishi kwa
kigezo cha kutungiwa sheria ya Bunge.
Kifungu cha Utii wa Miiko ya Uongozi wa Umma
ambacho kilisema “21(1) bila ya kuathiri masharti ya Katiba hii,
kiongozi wa Umma atapaswa kuheshimu na kutii maadili ya viongozi wa
umma, ikiwemo Miiko ya Uongozi.
(2) Miiko ya Uongozi inayorejewa katika ibara
ndogo ya (1), itakuwa kama ifuatavyo: (a) Kiongozi wa umma hatopaswa -
(i) kuvunja au kukiuka masharti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano; (ii)
kutoa au kupokea rushwa; (iii) kujilimbikizia mali kinyume cha sheria;
(iv) kusema uongo au kutoa taarifa zisizo za ukweli; (v) kutoa siri za
Serikali kinyume cha sheria; (vi) kutumia wadhifa, nafasi au cheo chake
kwa manufaa yake binafsi, familia yake, ndugu, jamaa au marafiki zake au
mtu yeyote aliye na uhusiano naye wa karibu; (vii) kufanya vitendo vya
uzembe, uvivu, ubaguzi, kiburi, dharau au unyanyasaji wa kijinsia.
(b) Kiongozi wa umma atapaswa kuheshimu na
kuendeleza - (i) dhana ya uwajibikaji wa pamoja kwa viongozi
wanaohusika; na (ii) maadili na Miiko ya Uongozi wa Umma, ikijumuisha:
(aa) kuwa na tabia na mienendo inayokubalika katika jamii; (bb)
kuheshimu, kutunza na kulinda mali za umma; na (cc) kutambua, kuheshimu
na kuzingatia Kanuni za Maadili na Mienendo ya Watumishi wa Umma, Kanuni
za Kudumu za Watumishi wa Umma, nyaraka za umma na miongozo mbalimbali
ya Serikali kuhusu viongozi na watumishi wa umma. (iii) kutenganisha
biashara na shughuli binafsi na masuala yanayohusiana na uongozi.
(3) Kiongozi wa umma ambaye anatuhumiwa kwa makosa
ya: (a) kimaadili; (b) udhalilishaji wa mtu au wa kijinsia; au (c) wizi
au ubadhirifu wa mali za umma, atasimamishwa kazi hadi suala lake
litakapoamuliwa kwa mujibu wa sheria za nchi au taratibu nyingine
zinazowahusu viongozi wa umma.” Ibara hii Mahususi imebaki kwenye
historia kwamba imebaki katika Rasimu ya Warioba lakini Bunge Maalumu
katika kuiboresha imeifutilia mbali.
(3) Mapato ya Jamhuri ya Muungano
Hili ni eneo ambalo litatuletea shida muda si
mrefu kwa jinsi lilivyo katika Katiba Inayopendekezwa. Tunasema vyanzo
vya Jamhuri ya Muungano ni Kodi ya Mapato, ushuru wa Bidhaa na Ushuru wa
Forodha. Pendekezo hili limebaki kama lilivyo katika Katiba ya Mwaka
1977. Kimsingi na kwa ufupi, pendekezo hili halijawahi kutekelezeka
tangu mwaka 1984, viongozi tujiulize kulirejesha kama lilivyo pasina ya
kutoa hoja na sababu zinakubalika katika pande zote za Jamhuri ni ubabe
au ni kupanga kushindwa? Au kiingereza tunasema “planning to fail”.
Nimejifunza kitu kuhusu Watanzania waishio
Zanzibar, wewe walazimishe na kwa shinikizo kubwa, watakukubalia katika
misingi ya “funika kombe mwanaharamu apite” na kwa hakika wakirudi
Zanzibar hawatatekeleza na itakuwa historia nyingine inayojirudia.
Ninasema kwa ushahidi kwamba pendekezo hili
litaendelea kuleta mzigo Tanzania Bara na litawaumiza Wazanzibari.
Nijielekeze kwenye mapato ya Zanzibar, kwa takwimu za makusanyo kutoka
Zanzibar kupitia Bodi ya Mapato ya Zanzibar (ZRB) pamoja na Mamlaka ya
Mapato ya Tanzania (TRA), kodi ya Mapato kwa Mwaka 2010/2011 kwa
Zanzibar ni Bilioni 65.5 sawa na asilimia 36.1 ya Makusanyo yote ya
Zanzibar ambayo yalikuwa Bilioni 180.
Naomba mchumi daraja la kwanza anisaidie kuelewa,
kama Wazanzibari wamechukua mambo yao yote ya kiuchumi, je, mambo hayo
watayaendesha kwa mapato yepi kama zaidi ya asilimia 36 ya mapato yao
yamechukuliwa na Jamhuri ya Muungano?
Itaendelea wiki ijayo
Chapisha Maoni