HOME
Watoa ahadi ‘hewa’ nao waadhibiwe
Tunapokea ahadi nyingi sana kutoka vyanzo
mbalimbali. Kutoka kwa wenzetu katika ndoa, wazazi na watoto wetu,
viongozi wetu wa dini, serikali, vyama n.k. Ahadi hizi hutupa matumaini
ya nini tukitarajiacho baadaye na kutufanya tupange utekelezaji wa mambo
kadha wa kadha ambayo tunaamini yatawezeshwa na ahadi zilizotolewa.
Zipo zile ahadi ambazo zinaathiri mtu mmojammoja, hizi tuziweke kando.
Zipo zile ambazo hutolewa kwa jamii ambazo kutotekelezwa kwake
kunaathiri idadi kubwa ya watu; hizi ndizo tuzimulike wiki hii.
Tuziangalie ahadi hizi hewa kama bidhaa zisizofaa
waziletazo wafanyabiashara. Hao wakileta bidhaa zisizofaa wanachukuliwa
hatua ikiwa ni pamoja na kuchoma bidhaa hizo. Hatuwezi kuchoma ahadi
kwani ikishatolewa imetolewa lakini tunaweza kumchoma mtoa ahadi kwa
kumpa adhabu ambayo inaweza kuwa fundisho kwake yeye ili asitoe tena
ahadi hewa au kwa wengine kutofanya kosa kama hilo. Tuna mifano mingi
kwetu ya watu wanaotoa ahadi hewa kwa jamii.
Mbunge anaahidi kwamba “mkinichagua, kero moja
mbili na tatu zitatoweka katika kipindi changu cha miaka mitano”.
Anayatoa hayo kwa kujiamini na kwa msisitizo.
Kutokana na ahadi hiyo watu wanawekeza katika
mambo mbalimbali wakiamini kwamba yale waliyoyawekeza yatawezekana kwa
utekelezaji wa ahadi aliyotoa mheshimiwa.
Kinachotokea ni kutotekelezwa kwa ahadi hizo, kero
zinaendelea na watu wanapata hasara na usumbufu mkubwa sana. Waziri
anapata uwaziri anatoa ahadi kwamba matatizo ya umeme yatakuwa historia.
Watu wanawekeza katika vitu ambavyo vinatumia
umeme, majumbani wananunua vyakula vya wiki nzima na kuvitunza katika
‘mafriji’ wakijua kwamba sasa hakuna kuharibika kitu kwani umeme
hautazimika.
Kinachotokea ni umeme kukatwa bila hata wananchi
kufahamishwa na kusababisha miradi iliyoanzishwa kusuasua au vyakula vya
majumbani kuharibika. Hali hii sasa ni kawaida katika nchi hii; ahadi
zinazotolewa hazitekelezwi, watu wanaumia halafu basi. Hakuna anayejali
maumivu tunayopata kutokana na kutotimizwa ahadi hizo. Mimi nafikiri
pamoja na kwamba watu wanaotoa ahadi kwa jamii hawafungi mkataba nao
bado matamshi yao peke yake na hasa pale yanapotolewa kupitia katika
vyombo vya habari yahesabike kama ni mkataba unaowabana katika
utekelezaji.
Pale ambapo wanashindwa kutimiza basi waadhibiwe.
Tunapozungumzia adhabu zisiwe tu adhabu za kushawishi watu kutomchagua
katika nafasi ya uongozi kipindi kijacho, bali ziwe ni adhabu ambazo
zitatoa fundisho kwa wengine kutotoa ahadi ambazo wanajua hawataweza
kuzitekeleza.
Kwa mfano kumpigia kura ya hapana mtu akiwa bado
kwenye uongozi hivyo kumwondoa katika madaraka kabla ya kuisha muda wake
wa uongozi.
Najua katika Rasimu ya Katiba Mpya kipo kipengele
kinachotoa fursa kwa wapiga kura kuchukua hatua kama hizo kwa mbunge
ambaye hatimizi ahadi zake, lakini kwa kuwa sehemu kubwa ya wale
wanaoijadili rasimu hiyo ni wabunge haohao basi kipengele hicho
kimekataliwa.
Katika mambo tunayotakiwa kuyapigia kelele na
kuhakikisha kuwa yanapitishwa katika bunge ni pamoja na hilo. Kwa nini
mbunge aondoe kipengele kinachomwajibisha pale anapotoa ahadi hewa?
Je, ni kwa sababu mtaji wao mkubwa wa kupatia kura
ni hizo ahadi hewa hivyo kipengele kinakula mitaji yao? Hapa tunatakiwa
‘kukomaa’ kuhakikisha kwamba kipengele hicho kinarudishwa.
Watu wengine ambao ni kero katika kutoa ahadi hewa ni watumishi wa Mungu waliozuka siku hizi.
Wameacha kutuahidi nafasi mbinguni pale
tutakapoishi kwa matakwa ya Mungu bali sasa wanatuahidi kuwa na magari,
nyumba, fedha nyingi, watoto n.k. wakiongea kwa kujiamini kana kwamba
wao ndiyo watoaji.
Utasikia maneno kama; mkutano huu utakapokwisha
basi ujue tumbo lako la uzazi litafunguka, kazi uliokuwa unaitafuta
utaipata, ugonjwa wako wa kisukari utaisha, mtoto wako atapona, biashara
zako zitakwenda kushamiri n.k.
Hii ni ahadi ambayo mtumishi anatoa kwa wote watakaohudhuria mkutano ule.
Hawasemi kwamba kuna uwezekano wa mtu kutojaliwa kwa kipindi hicho hata kipindi chochote; wao wanaweka mafanikio tu.
Hebu fikiria mtu anakopa nauli kwa siku 10 za
mkutano kwa matumaini kwamba mkutano utakapoisha basi zitakuja nyingine.
Licha ya nauli mtu huyo kakopa hata ile fedha ya kuweka kwenye bahasha
ambayo anaambiwa ikishaombewa majibu yake ni katika mkutano huo ambapo
zitaongezeka nyingine. Nani analipa deni hilo kama yale matarajio
hayajapatikana? Siyo kwamba haitokei, mbona inatokea mara nyingi tu!
Mtu akaenda kwenye hiyo mikutano akashindwa kupata kile anachomlazimisha Mungu ampe tena kwa muda anaotaka yeye.
Mimi ni muumini mzuri na ninaamini Mungu yupo na
anajibu maombi. Lakini naamini anajibu maombi kwa wakati na kwa namna
yake, anampa mtu anachostahili kupewa tena kwa wakati wake.
Nisingependa kuanzisha malumbano na hao wenye
kuwahakikishia watu kupata magari, nyumba, uponyaji wakienda kwenye
makanisa yao au kuhudhuria mikutano yao ya dini; ninachodai mimi ni
kwamba pale wanapotoa ahadi hizo basi ichukuliwe kwamba ni deni na
lazima walipe pale ambapo yale waliyoyaahidi hayajatekelezeka.
Wawajibishwe kwani wanawapa watu matumaini ambayo wao hawana uwezo wa kuyatekeleza.
Watumishi hao wanatoa fursa ya wale ambao wanasema
wamefanikiwa kutoa ushuhuda wao mbele ya kadamnasi ili kila mtu ajue
wamefanikiwa.
Vivyohivyo wale wasiofanikiwa nao wapate fursa ya
kujieleza maumivu yaliyowapata kwa kutotimia yale ambayo waliahidiwa
pindi watakaposhiriki na kujitoa katika mkutano ule.
Watumishi wabanwe kufidia maumivu ambayo waumini wao wanayapata
kwa kuamini kile wanachokisema. Kama hiyo haiwezekani, basi taasisi
husika zifute usajili wa madhehebu yanayowaahidi watu mambo
yasiyotekelezeka.
Kwa kuwa watu hawaadhibiwi kwa kutoa ahadi hewa basi utoaji wa ahadi hizo umekuwa ni jambo la kawaida.
Watu wanatumia ahadi hizo kama mtaji wa kujinufaisha na kisha kuwaacha wale waliowaahidi mikono mitupu.
Huu ni utapeli ambao kama ulivyo utapeli mwingine unatakiwa kuchukuliwa hatua.
Kama waganga wa kienyeji wanafungiwa kwa
kuichanganya jamii kwa nini hao watoa ahadi hewa nao wasifungiwe kwa
sababu hiyo hiyo ya kuichanganya jamii?
Chapisha Maoni