HOME
MAKALA YA SHERIA: MNUNUZI WA GARI JIHADHARI NA UTAPELI HUU WA KIMKATABA
Na Bashir Yakub
1. KUTAPELIWA KATIKA UNUNUZI WA GARI.
Ununuzi
wa magari sawa na biashara nyingine yoyote unahitaji umakini. Lakini
ununuzi wa gari unahitaji umakini mkubwa zaidi pengine kuliko mali
nyingine yoyote inayohamishika kwa sasa. Hii ni kutokana na kukua kwa
biashara ya bidhaa hiyo kulikoleteleza kujipenyeza kwa matapeli hasa
mijini. Utapeli wa magari ni mkubwa kuliko watu wanavyofikiria na idadi
ya wanaotapeliwa kwa siku inaelekea kulingana na idadi ya magari
yanayouzwa kwa siku. Si rahisi kulijua hili kama hufuatilii mambo haya.
Uzuri au ubaya, wanaofanya matukio haya ni walewale. Nafasi kubwa
wanayotumia ni ulaghai wa kimkataba na wanatumia mapungufu ya mkataba
kumtapeli mtu halafu wanaendelea kuwapo na huna la kufanya sababu
mkataba wako una mapungufu ambayo uzito wake kisheria ni kama huna
mkataba. Aliyekutapeli atakuwapo na hutakuwa na la kufanya kwasababu ya
msemo wa kisheria usemao “Buyer Be Aware”(Mnunuzi kuwa Makini). Umakini
wako ni katika kufanya mkataba utakaolinda manunuzi yako. Lau ukifanya
kosa sheria imeshasema hivyo imemaliza.
2. MKATABA SALAMA WA KUNUNULIA GARI LAKO HAKIKISHA UNA TAARIFA HIZI.
( a )
Lazima uwe na majina ya wahusika ambayo yatakuwa yameandikwa kwa urefu
na kwa kueleweka.Mfano jina liwe Aloys Mayenge Archard. Epuka kuandika
vifupi mfano A.M. Archard. Jina linatakiwa liwe katika ukamilifu wake
na hasa pawe na majina matatu kamili. Pia majina ya pande zote mbili
yaani muuzaji na mnunuzi yatokee hivyohiyvo si tu majina ya upande
mmoja. Yawezekana mkataba mwingine unahusisha watu wengi zaidi pia ni
muhimu majina matatu ya kila mmoja yaonekane hata kama wako ishirini.
( b )
Katika majina hayo hadhi ya kila mmoja iainishwe mbele ya jina lake.
Mfano kama ni muuzaji au mnunuzi mbele iandikwe kuwa huyu ni muuzaji na
huyu ni mnunuzi. Halikadhalika kama ni mkopaji, mkopeshwaji, mtoa
zawadi mpokea zawadi viainishwe.
( c
) Bei au gharama halisi ya mauziano ioneshwe. Iandikwe kwa tarakimu
yaani namba mfano 10,000,000/= na kwa maneno katika mabano ( Milioni
kumi tu).Ni muhimu yote mawili yaonekane , hii huondoa utata.Tarehe ya
mkataba ioneshwe sambamba na maelezo kama fedha imelipwa yote au kiasi.
( d )
Kama kuna kiasi kilichobaki kianishwe kwa tarakimu na pia kwa maneno
kama nilivyoonesha hapo juu. Muda wa kulipa kilichobaki nao uainishwe
ikiwa ni pamoja na hatua za kuchukua ikiwa muda uliowekwa utapita.
Mkataba lazima uoneshe muda ukipita nini kifanyike mfano ikifika
tarehe 7. 12. 2015 saa kumi jioni kiasi cha pesa iliyobaki hakijalipwa
basi gari litamrudia muuzaji na mnunuzi hatakuwa na deni lolote dhidi ya
muuzaji, au itahesabika kuwa mkataba umevunjika na mnunuzi atatakiwa
kumlipa fidia ya kiasi fulani muuzaji kwa kuvunja mkataba.
( e )
Mashahidi ni muhimu kila upande. Kila upande hata ukiwa na shahidi
mmoja wala si mbaya. Shahidi awe mtu wa kuaminika , mtu mzima na mwenye
akili timamu. Wataandika majina yao matatu kwa urefu kama yalivyo ya
wahusika na pia wataweka sahihi zao huku ikioneshwa shahidi yupi wa
upande upi na yupi wa upande upi.
( f
) Gari iliyouzwa au iliyohusishwa kwenye mkataba ichambuliwe
vyema.Mfano chasis No, aina ya bodi,watengenezaji,rangi,namba kama
imesajiliwa,uwezo wa injini,aina ya mafuta inayotumia,mwaka
iliyotengenezwa n.k.
( g )Mkataba ni lazima ueleze gari imeingia nchini ikitokea wapi kama ni Japan,Dubai n.k.
( h )
Anuani za muuzaji au mnunuzi ziwepo ikiwa ni pamoja na namba ya simu.
Hili la namba ya simu ni muhimu sana kwasasa kutokana na msaada mkubwa
wa mawasiliano haya endapo mtu atahitajika.
( I )
Alama ya dole gumba mbele ya jina nayo ni muhimu sana. Hii ni kutokama
na alama hii kutoweza kwa namna yoyote kuingiliwa au kughushiwa.Tia dole
kwenye kablasha ya muhuri na weka dole gumba mbele ya kila jina. Na
hapa ndipo wanapokamatiwa matapeli walio wengi. Hatua hii pia si lazima
kwa mashahidi.
( j )
Lazima mkataba ueleze kama gari imelipiwa leseni ya barabarani( road
licence), bima, na kama ililipa ushuru wote muhimu unaotakiwa wakati wa
kuingia nchini.Kama haijalipiwa baadhi au vyote mkataba ueleze na deni
liainishwe.
( k )
Ni muhimu pia mkataba uoneshe iwapo gari lina tatizo lolote la
kiufundi(machenical problem) kama hapana basi isemwe nini kifanyike kama
muda mfupi baada ya manunuzi litagundulika tatizo ambalo muuzaji
hakulisema.
( L )
Pia ni muhimu sana mkataba uoneshe iwapo mgogoro wowote utatokea
kuhusiana na mauzo ya gari nini wahusika wafanye, mfano endapo mgogoro
utatokea kuhusiana na mkataba huu mahakama ya Tanzania yenye mamlaka
ndio itahusika na utatuzi wa mgogoro. Sambamba na hilo mkataba uweke
wajibu kwa muuzaji kuwa tayari kumpa ushirikiano mnunuzi iwapo gari
alilomuuzia litakuwa na mgogoro kuhusu wizi,ushuru,mkopo, au mgogoro
wowote unaotokana na mkataba wa mauziano hayo.
( M ) Aidha kipengele kinachomtaka muuzaji kurejesha fedha yote au sehemu yake iwapo jambo fulani litatokea pia chaweza kuwekwa.
3. TUSIPENDE KUFANYA MAMBO KIENYEJI.
Muda
wa kufanya mambo kienyeji umekwisha. Dunia imebadilika sana lazima watu
walikubali hili. Ieleweke kuwa kufanya mambo kienyeji kuna gharama zake
kubwa tu. Unaweza kuuziwa gari ambayo inatafutwa kwa kuua mtu jana.
Unaweza kuuziwa gari ambayo inatafutwa kwa kushiriki katika uhalifu
mkubwa wiki iliyopita.Haya yote utayajibu vipi na yataisha lini. Unaweza
kuuziwa gari ambayo haikulipa ushuru kwakuwa imesajiliwa kama
inasafirishwa( IN TRANSIT, IT) si ya hapa nchini, vipi utamaliza kesi
na mzigo wa mamilioni ya deni la ushuru. Jihadhari ndugu epuka kufanya
mambo kienyeji.
.
MWANDISHI
WA MAKALA HAYA NI MWANASHERIA NA MSHAURI WA SHERIA
KUPITIA GAZETI LA SERIKALI LA HABARI LEO KILA JUMANNE ,
GAZETI JAMHURI KILA JUMANNE NA GAZETI NIPASHE KILA JUMATANO.
0784482959,
0714047241,
bashiryakub@ymail.com
Chapisha Maoni