HOME
BAADA ya Rais John Magufuli, kuja na mtindo wa kuteua wakuu wa wilaya
mmoja mmoja kujaza nafasi zilizo wazi badala ya kufanya mabadiliko kwa
nchi nzima, baadhi ya wasomi wamepongeza hatua hiyo wakisema inasaidia
kubana bajeti na kupata watu makini.
RAIS JOHN MAGUFULI.
Hivi Karibuni, Rais Magufuli alimteua, Gelasius Byakanwa, kuwa Mkuu wa
Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro kabla ya juzi kumteua Ally Hapi, kuwa
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni na Humphrey Polepole kuwa Mkuu wa Wilaya ya
Musoma.
Hatua hiyo ni tofauti na ya Marais waliotangulia ambao mara baada ya
kuapishwa, walikuwa wakiteua Baraza la Mawaziri, makatibu wakuu na
wakurugenzi, wakuu wa mikoa wa wilaya nchi nzima.
Mchambuzi wa masuala ya kisiasa na kidiplomasia kutoka Chuo cha
Diplomasia, Israel Sostenes, alisema alichokifanya Rais Magufuli ni
kujaza nafasi muhimu kwa upande wa watendaji na watawala.
“Ameshateua Baraza la Mawaziri, wakuu wa mikoa na wakurugenzi wa idara
nyeti, hatua mbayo ni nzuri, wakuu wa wilaya siyo jambo la muhimu sana
kwa sababu ameshapanga vyema safu yake ya ngazi ya juu,” alisema.
Alisema Rais Magufuli ana nia njema na ya dhati na kwamba anaangalia na
kufuatilia kwa makini kabla ya kuteua ili kupata wanaotosha kwenye
nafasi hizo.
Alisema kuchelewa kwa uteuzi huo, hakuwezi kutokana na kukosekana kwa
fedha bali ni kuona namna anaweza kuokoa fedha kwa kuteua wakuu wa
wilaya.
Kwa upande wake, mchambuzi wa masuala ya siasa, Abdulhakim Atiki,
alisema suala la kuteua wakuu kwa kujaza nafasi linatokana na Rais
kuridhika na utendaji wa waliopo.
Alisema Baraza la Mawaziri ndiyo muhimu kwa sababu linavunjika, lakini
kwa upande wa wakuu wa mikoa na wilaya wanaweza kuendelea kufanya kazi
bila kuteua wapya.
“Huenda Rais ameona utendaji wao uko vizuri na akaishia kubadili wakuu
wa mikoa pekee na wakuu wa wilaya akaendela kujaza nafasi. Hili ni jambo
jema kwa sababu yuko makini na uteuzi wake,” alisema.
Naye Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(UDSM), Richard Mbunda, alisema utaratibu huo alioufanya Rais Magufuli,
ni jambo zuri kwani kitu cha msingi anachokiangalia ni utendaji wa kazi.
Alisema marais wanapoingia madarakani, wanakuwa na nafasi za uteuzi
zaidi ya 5,000, hivyo Rais Magufuli anachokiangalia ni maslahi ya taifa
na si vingine.
“Rais hajaingia kwa shinikizo la mtu ama kumchagua mtu kwa vile analipa
fadhila, wapo wakuu wa wilaya ambao ni wazuri na amewabakiza hakuna
umuhimu wa kuwaondoa wote, utaratibu mzuri ni kuangalia utendaji kazi
kama ilivyo kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro alivyoachwa kulikuwa na
sababu,” alisema Mbunda na kuongeza:
“Huu ni utaratibu mzuri wa utendaji kazi kwani anawafuatilia na baadaye
kufanya uamuzi. Hii itasaidia kuongeza ufanisi wa kazi kwa viongozi
wetu.
Chanzo: NIPASHE
Chapisha Maoni