NEWSROOM NEWSROOM Author
Title: Hakika Magufuli ni kiongozi wa zama hizi
Author: NEWSROOM
Rating 5 of 5 Des:
HOME IMEANDIKWA NA  MWANDISHI WETU IMECHAPISHWA: 31 MAI 2016  Kuchapa     Barua pepe Rais John Magufuli WAKATI w...
HOME



WAKATI wa kampeni, baadhi ya Watanzania walikuwa wakibeza kila mwanasiasa anayetokea CCM na kwa dhana hiyo hiyo walikuwa wakimbeza pia John Magufuli.
Waliona kwamba hana uwezo wa kuongoza nchi na au atakuwa mtu wa kuendeleza baadhi ya mambo ambayo Watanzania kwa muda mrefu wamekuwa wakiyapigia kelele, hususani ufisadi. Lakini sasa wanaanza kuona aibu na wengi wao wamekwishaanza kumuunga mkono japo kimya kimya. Hii ni kwa sababu sasa Magufuli anaonesha mabadiliko ya kweli na siyo yale ya ‘kuzungusha mikono waliyokuwa wanayafikiria waliokuwa wakiunga mkono kambi ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Wengi wao, wameanza kuamini kuwa Taifa lilikuwa linamhitaji kiongozi kama Magufuli kuweza kulinasua mahali lilipo kuliko kiongozi yule mwingine toka upinzani. Hatua zake mbalimbali za mwanzo kushughulikia; kubana matumizi, kupambana na ufisadi na kuondoa watendaji mizigo (majipu) kumewafanya waamini kabisa kuwa Magufuli kazi aliyonayo akiendelea na kasi hiyo basi ndani ya mwaka huu mmoja tu atakuwa ameleta heshima katika utumishi wa umma. Siyo hivyo tu bali pia alikuwa amerejesha heshima kwa Watanzania na fahari ya taifa letu.
Sasa bila shaka kwamba wanaamini kabisa kuwa Magufuli anafanya kazi hii bila woga, huruma, husuda, wivu au kusitasita. Kwamba, hatomwangalia yeyote, popote na kwa lolote. Ndani ya miezi sita hii na ujio wa bajeti ya kwanza ya serikali yakeghakuna shaka kwamba Magufuli ameweka alama za namna gani taifa linataka kwenda na kila kiongozi atakuwa amepata ujumbe. Waliombeza walifanya makosa kwa sababu walidhani hii ni kazi rahisi kwa Rais.
Walidhani ni kazi ya kutimua huyu, kuondoa yule na kumleta yule mwingine. Walidhani ni kazi ambayo akimaliza teuzi mbalimbali basi atakuwa ameipanga serikali yake kwa ajili ya kuchapa kazi. Sasa wanajua kuwa uamuzi wake wa kushughulika na watu kwanza kabla ya mfumo ni jambo muhimu sana. Ulikuwa ni uamuzi sahihi na unahitaji kuungwa mkono na kutetewa.
Watu ndio hutengeneza mfumo; ni watu ndio ambao hukaa chini na kufanya maamuzi mbalimbali yenye kuathiri (kwa uzuri au ubaya) uwepo na utendaji wa mfumo wa utawala. Ukiwa na watu wabovu, wabinafsi na wenye mwelekeo wa ufisadi basi mfumo utakuwa mbovu, wa kibinafsi na wenye uelekeo wa kifisadi kwa sababu moja kubwa; wale wenye kuiwamba ngoma ngozi huivutia kwao! Matobo (si matundu) kwenye sheria zetu yalitengenezwa na watu ambao walijua wakiziba na wao watakuwa wamejizibia.
Magufuli asingeweza kutengeneza mfumo mwingine kwa kutumia watu wale wale walioutengeneza mfumo huu wa sasa na hasa kama watu hao ni wanufaika wa mfumo huu. Ingelikuwa ni sawa sawa na kumtaka Rais awalazimishe watu wakate matawi ambayo wamekalia huku wakijua kwa kufanya hivyo wataangukia mtoni kwenye mamba wengi. Hakukuwa na jinsi na bado hakuna jinsi. Ni lazima kuwaondoa hawa na kuwashughulikia ili kuleta watu wenye fikra zinazoakisi mwelekeo wa serikali yake.
Ni kwa sababu hiyo, kumbe kazi ile ya miezi sita kwa kweli haiwezekani. Ni kazi ambayo inapaswa kuwa endelevu na yenye matokeo bora. Tayari tumeanza kuona dalili za yaliyomo ndani ya ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu (CAG) na tayari inatisha kama ilivyotisha kwa miaka kadhaa. Kwa muda mrefu tumekuwa tukijulishwa juu ya uchafu wa watendaji wetu na taasisi zetu na mara karibu hizo zote tumekuwa tukionesha kushtushwa na kusikitishwa tukiamini kuwa labda mwaka unaofuatia mambo yatakuwa tofauti.
CAG aliyepita alikuwa anarudia baadhi ya hoja mwaka baada ya mwaka na wakati mwingine kuhusiana na taasisi au watu wale wale. Na safari hii tusije kushangaa kuwa hata CAG wa sasa anaweza kujikuta amegusa maeneo yale yale; matumizi mabaya ya sheria ya manunuzi ya umma, fedha kutumiwa bila maelezo, kutopatikana kwa vitabu vya masuala ya fedha wakati wa ukaguzi, na upotevu wa fedha za umma kwa namna ambayo inadokeza tu kuwa zimeliwa.
Magufuli basi ana kazi kubwa; kushughulikia viongozi wabadhirifu, wazembe, wezi na wenye kutumia madaraka yao vibaya na wakati huo huo kupanga na kusimamia serikali yake huku akiunda upya mfumo uliojaribiwa na kuharibiwa. Kwa mwendo alioanza nao hakuna shaka yoyote jambo moja lilikuwa sahihi kwa upande wangu; kuunga mkono mabadiliko haya. Wapo wanadhani hali ni ngumu sasa na kuwa serikali inabana, naamini bado hatujaona hasa ugumu kwani hadi hivi sasa bado serikali inahangaika na madudu ya nyuma na yanatisha.
Kusahihisha uchumi (correcting an economy) ambao umejengwa na kusimamiwa na utamaduni wa kifisadi (corrupt culture) haiwezekani kuwa ni jambo jepesi. Ni kwa sababu hiyo sasa mimi na wengine wenye mawazo kama mimi tuamini yafuatayo: Mosi, kuanza kazi kwa mahakama za kushughulikia ufisadi na uhujumu uchumi kunahitajika mara moja.
Pili, sheria ya CAG ifanyiwe mabadiliko mapema zaidi ili CAG awe na madaraka ya kutoa agizo la kusimamishwa kazi na hata kufikishwa mahakamani kwa mtendaji yeyote wa umma ambaye uchunguzi wake (CAG) unaonesha kuwa kuna uvunjaji wa sheria. Ikiwezekana ofisi ya CAG iwe na waendesha mashtaka wake kama ilivyo kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa (Takukuru). Haipaswi madudu ya mwaka mzima yanasubiri mwaka mwingine kujulikana.
CAG anapofanya ukaguzi na kukuta madudu na ushahidi wa kisayansi upo (forensic evidence) basi hatua zichukuliwe mara moja. Siyo awe na uwezo wa kupeleka mashtaka lakini kwa kupendekeza kwa DPP. Ikiwezekana, kutegemea ushahidi alio nao, watuhumiwa watiwe mbaroni, mali zao zinazohisiwa kupatikana kwa njia haramu zikamatwe ili zije kufilisiwa wakikutwa na hatia mahakamani. Pili, Sheria ya Usalama wa Taifa inahitaji kufanyiwa marekebisho ya haraka.
Hili ni jambo ambalo limekuwa katika mada zangu kwa karibu miaka kumi sasa. TISS bado ni dhaifu na udhaifu wake umechangia sana kutamalaki kwa utamaduni wa kifisadi. Natumaini Magufuli hatochukua muda mrefu kuifumua hii taasisi kwani ndio moyo wa taifa. Ikilegea taifa liko mashakani. Kuna na mengine mengi ambayo naamini Magufuli atayafanya kwani tayari ameshaanza kuyafanya na kuwa endapo atafanikiwa tutakapofika mwisho wa mwaka huu kama taifa tutashusha pumzi kidogo kwani angalau tutakuwa katika mazingira ya kusema ‘kweli hakika huyu alikuwa anahitajika.’
Ni wazi pia, kutokana na kazi hii ngumu ambayo tunaamini Magufuli anaiweza kutakuwepo na wasema ‘hapana’ na waleta ‘vikwazo.’ Wale ambao wataona maslahi yao yanaguswa na kuwa pale walipokuwa wakihemea sasa panaanza kuondolewa. Watakuwepo watu ambao watajaribu kudhulumu na kuharibu jitihada hizi; raia wa kawaida, watendaji serikalini, wabunge na tusije kushangaa hata watu wake wa karibu!
La maana ni kukaza mwendo na kuendelea kusafisha serikali, kuleta uwajibikaji, na nidhamu ili hatimaye ujenzi mpya (Reconstruction) wa taifa letu uanze tena kwani pale tulipoacha kulijenga tulianza kulibomoa. Hizi ni zama mpya, zama za ujenzi mpya wa taifa letu. Katika hili, naamini nipo sahihi na bado naendelea kuwa sahihi. Magufuli ni kiongozi wa zama hizi.
VIA HABARI LEO

About Author

Advertisement

Chapisha Maoni

 
Top