Tangu kuanza kwa zoezi la kufuatilia wafanyabiashara wanaoficha sukari kwa agizo la Rais wa Jamhuri ya Tanzania Mh. Dr John Pombe Magufuli, kumekuwa na wimbi la watu wanaojiita “makachero wa TAKUKURU kutoka Makao Makuu” nao wakifuatilia sakata la sukari mkoani Kilimanjaro.
Matapeli hao ambao kwa sasa wapo wilayani SIHA, wamekuwa wakiwasumbua wafanya biashara kwa kudai kuwa wametumwa kuwashughulikia huku wakiomba kupewa fedha ili wawasafishe.
Kiasi cha fedha ambacho kimekuwa kikiombwa ni kati ya Shilingi 150,000/= hadi 500,000/= kama “gharama ya kuwasafisha kwa Mheshimiwa Rais”
Naomba wafanya baiashara Mkoani Kilimanjaro waelewe kwamba, TAKUKURU inao mfumo wa utendaji kazi ambao unajali misingi ya utawala bora na kamwe haihusiki na utapeli wa aina hii.
TAKUKURU katika utendaji wake wa kazi, haiwatozi wafanya biashara fedha kama adhabu kwa kuhifadhi sukari kinyume na taratibu. TAKUKURU inafuatilia, kuhoji na kumtaka mfanyabiashara kuonesha namna anavyomiliki sukari hiyo kwa kutoa vielelezo husika. Mwisho wa zoezi hili, atakayetoa tamko ni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.
Ifahamike kuwa hakuna afisa wa TAKUKURU mpaka sasa aliyetumwa kutoka Makao Makuu kuja mkoani Kilimanjaro kufuatilia zoezi la sukari. Zoezi hili mkoani hapa linaendeshwa na vyombo vya ulinzi na usalama kama timu moja na wala halifanywi na TAKUKURU pekee .
Ifahamike pia kuwa hakuna zoezi linaloihusisha TAKUKURU litakaloendeshwa mkoani bila ofisi ya mkoa kuwa na taarifa.
Kwa misingi hiyo yeyote anayeendesha zoezi hilo nje ya utaratibu nilioufafanua ni tapeli, taarifa zake zitolewe mapema ili akamatwe na kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria.
Maofisa wote kutoka ofisi ya TAKUKURU mkoa wanavyo vitambulisho na kama watatiliwa shaka basi ofisi yangu ijulishwe kupitia simu namba 0784 998 804 au 0786 089 805 muda wowote.
IMETOLEWA NA
ALEX J KUHANDA
MKUU WA TAKUKURU MKOA WA KILIMANJARO
11/5/2106.
Chapisha Maoni