HOME
Wahitimu wa Kidato cha Sita wa Shule ya Sekondari WAMA- Nakayama
wakionyesha maonyesho ya masomo kwa Mgeni Rasmi, Mhe. Ummy
Mwalimu, Mwenyekiti wa WAMA, Mama Salma Kikwete pamoja na
wageni waalikwa.
Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Sekondari ya
WAMA- Nakayama, Dr. Ramadhani Dau, akitoa neno la ukaribisho kwa wageni waalikwa katika
Sherehe za mahafali ya Kidato cha sita shule ya sekondari WAMA
Nakayama
Kaimu Balozi wa Japan hapa nchini Bw. Hiroyuki KUBOTA akisoma
hotuba yake wakati wa Sherehe za Mahafali.
Mke wa Rais Mstaafu na Mwenyekiti wa WAMA, Mama Salma Kikwete
akisoma hotuba yake kwa wageni waalikwa na wahitimu wakati wa Sherehe
za Mahafali ya kwanza ya Kidato cha Sita ya Shule ya WAMA- Nakayama.
Wahitimu wa Kidato cha Sita wa Shule ya Sekondari ya WAMA -
Nakayama katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa WAMA mara baada
ya kumkabidhi Cheti cha Shukrani kwa mchango wake katika maendeleo
ya elimu yao.
Mgeni Rasmi Mhe. Ummy Mwalimu Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto akihutubia wahitimu, walimu na wageni
waalikwa wakati wa sherehe za mahafali.
Na Philomena Marijani, WAMA Foundation
Serikali imechukua hatua maalum za kisera na kimipango kuhakikisha kunakuwa
na usawa wa kijinsia katika elimu, mafunzo, sayansi na teknolojia. Maelezo hayo
yametolewa na Mhe.Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto wakati wa sherehe za Mahafali ya kwanza ya Kidato cha
Sita ya Shule ya Sekondari ya WAMA- Nakayama yaliyofanyika mwishoni wa
wiki katika ofisi za WAMA zilizopo Kawe, Dar es Salaam.
Mhe.Ummy Mwalimu ambaye alikuwa mgeni rasmi katika sherehe hizo amesema
moja ya hatua hizo ni pamoja na kuongeza idadi ya wasichana wanaopata elimu
ya msingi ili kuwepo na idadi sawa ya wavulana na wasichana.
Aliongeza kuwa kwa mwaka 2008 serikali ilifanyia marekebisho Sheria ya Elimu
na mafunzo ili kukidhi matakwa ya usawa wa kijinsia. “Baadhi ya maswala
ambayo yamerekebishwa ili kuboresha mazingira ya shule yaweze kuwa rafiki
kwa wasichana ni pamoja na kuhamasisha jamii kutoa chakula shuleni, kujenga
mabweni na vyoo kwa ajili ya wasichana na pia kuongeza idadi ya walimu.
Wizara yangu pia imeandaa Sera ya Maendeleo ya Mtoto ya mwaka 2008 na
Sheria ya Mtoto No.21 ya mwaka 2009 ambayo inasisitiza jamii kuzingatia utoaji
wa haki za msingi kwa watoto, moja ya haki hizo ni haki ya kuendelezwa.”
Alisema Mhe. Ummy Mwalimu.
Mhe. Mwalimu aliwashauri wahitimu wa WAMA-Nakayama wasiridhike na
elimu ya kidato cha sita bali wajiendeleze kwa kujiunga na vyuo mbalimbali hapa
nchini na hatimaye serikali ipate viongozi wengi wanawake.
Akiongea katika sherehe za mahafali hayo Mke wa Rais Mstaafu na Mwenyekiti
wa WAMA Mama Salma Kikwete alisema Shule ya Sekondari ya WAMA-
Nakayama ilianzishwa ili kutoa mchango katika Juhudi za Taifa za kumkomboa
mwanamke kwa kuwapatia fursa za elimu bora ya sekondari watoto wa kike
wanaotoka katika mazingira magumu wakiwemo yatima.
“Taasisi inatambua kwamba ili mtoto wa kike aweze kupata mafanikio katika
masomo yake ni muhimu kumjengea mazingira wezeshi ya kusomea na kuishi.
Ndiyo maana tuliamua kuwajengea shule yenye mahitaji yote ya kupata elimu bora
na pia kuepuka vishawishi mbalimbali vinavyoweza kupelekea kukatisha masomo.
Alisema Mama Kikwete.
Mama Kikwete aliwashukuru wadau wote ambao wamekuwa wakitoa misaada
mbalimbali tangu kuanzishwa kwa shule ya WAMA- Nakayama na kusema
ushirikiano huo umesaidia kufanikisha ndoto ya kuwasaidia watoto wa kike na
matunda yake yanaonekana kwa wanafunzi wanaohitimu kidato cha sita.
Akisoma hotuba yake Kaimu wa Balozi wa Japan hapa nchini,Bw. Hiroyuki
KUBOTA alisema shule hii iliweza kuanzishwa kwa msaada kutoka kwa Bw.
Nakayama wa Japan ambaye alichangia hela za ujenzi wa shule. Aliongeza kuwa
Ubalozi wa Japan hapa nchini umekuwa ukisaidia shule katika masuala mbalimbali
ikiwemo maboresho ya sick- bay, maabara, na kwa sasa ubalozi unasaidia upanuzi
wa jengo la utawala ambao utamalizika baada ya muda mfupi.
Shule ya Sekondari ya WAMA- Nakayama iliyopo Nyamisati, Rufiji katika Mkoa
wa Pwani ilianza rasmi mwaka 2010. Shule inasaidia wasichana yatima na
waliotoka katika mazingira hatarishi kutoka mikoa yote Tanzania bara na visiwani.
Jumla ya wanafunzi wa kike 27 watamaliza kidato cha sita mwezi mei mwaka huu
katika michepuo ya ECA na PCB.
Chapisha Maoni