HOME
Katiba Mpya: Ni mchezo wa namba
Rasimu hiyo pia ina sura mpya mbili ambazo ni
Mamlaka na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na nyingine inayohusu Ardhi,
Maliasili na Mazingira.
Akiwasilisha rasimu hiyo, Mwenyekiti wa kamati
hiyo, Andrew Chenge aliliambia Bunge kuwa Ibara 233 za rasimu hiyo
zinatokana na Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Chenge, ambaye aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa
Serikali (AG), alisema ibara 47 za Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya
Katiba zimebaki kama zilivyokuwa, 186 zimefanyiwa marekebisho, 28
zimefutwa na 41 ni mpya.
Rasimu hiyo ya Katiba inayopendekezwa imefuta
kabisa muundo wa Muungano wa shirikisho ambao ungezaa muundo wa serikali
tatu na badala yake imerudisha muundo wa sasa wa serikali mbili.
Chenge alisema kamati za Bunge hilo pamoja na
wajumbe walio wengi, waliona kuingiza muundo wa shirikisho ilikuwa ni
kukiuka makubaliano ya Muungano yaliyofikiwa mwaka 1964.
Kwa kurejesha muundo wa serikali mbili uliokuwa
ukipigiwa chapuo na CCM, Rasimu hiyo imependekeza kuwapo kwa makamu
watatu wa rais.
Chenge alisema uongozi wa Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania utakuwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
na mgombea mwenza atakayekuwa makamu wa kwanza wa rais.
Chini ya muundo huo, Rais wa Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar (SMZ), atakuwa makamu wa pili wa rais ilhali Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atakuwa makamu wa tatu wa rais.
Chenge alisema mapendekezo hayo yamezingatia
ukweli kuwa kuwapo kwa mgombea mwenza anayekuwa makamu wa kwanza wa
rais, kutafanya rais na makamu wake kutoka chama kimoja.
Rasimu hiyo inayopendekezwa, imepunguza Tunu za
Taifa kutoka saba zilizokuwamo kwenye Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya
Katiba hadi nne huku mambo ya muungano yakiongezwa kutoka saba hadi 14.
Katika Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
Tunu za Taifa zilikuwa ni utu, uzalendo, uadilifu, umoja, uwazi,
uwajibikaji na lugha ya Taifa; sasa zimebaki Lugha ya Kiswahili,
Muungano, utu na undugu na amani na utulivu. Tunu tatu ambazo ni
uzalendo, uadilifu na umoja zimeondolewa.
Mambo ya Muungano
Katika Rasimu ya Tume, mambo ya Muungano
yaliyoorodheshwa ni Katiba na Mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
na ulinzi na usalama.
Mambo mengine yalikuwa ni uraia na uhamiaji,
sarafu na benki kuu, mambo ya nje, usajili wa vyama vya siasa, ushuru wa
bidhaa na mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na mambo ya Muungano.
Rasimu inayopendekezwa imetaja mambo ya muungano
kuwa ni Katiba na Mamlaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ulinzi na
usalama, usafiri wa anga, uraia, uhamiaji, polisi, sarafu na benki kuu
na kodi ya mapato inayolipwa na watu binafsi na mashirika, ushuru wa
forodha na bidhaa zinazotengenezwa Tanzania na kusimamiwa na idara ya
forodha.
Mengine ni mambo ya nje, usajili wa vyama vya
siasa, Mahakama ya Juu na Mahakama ya Rufani, elimu ya juu, Baraza la
Taifa la Mitihani, Utabiri wa Hali ya Hewa na utumishi Serikali ya
Jamhuri.
Mambo mengine ambayo yalikuwa katika Rasimu ya
Warioba yaliyowekwa kando ni pendekezo la wabunge kutokuwa mawaziri
ikipendekezwa utaratibu wa sasa wa wabunge kuwa mawaziri uendelee
kutumika.
Chenge alisema Rasimu ya Katiba inayopendekezwa,
imeweka ukomo wa mawaziri kuwa wasizidi 30 wakati naibu mawaziri
watateuliwa kulingana na mahitaji mahsusi. Tume ya Warioba ilipendekeza
mawaziri wasiozidi 15.
Rasimu hiyo inayopendekezwa imefumua muundo wa
Bunge uliopendekezwa na Rasimu ya Warioba kuwa wawe 75 wa kuchaguliwa
majimboni na watano kutoka kundi la watu wenye ulemavu, badala yake
imesema muundo wa sasa uendelee ukiwa na wabunge 360 kwa sharti la
kuwapo uwiano sawa kati ya wanawake na wanaume.
Rasimu hiyo imetupilia mbali pendekezo la mtu
anayetaka kugombea ubunge awe na elimu isiyopungua kidato cha nne na
kurudisha kuwa ajue tu kusoma na kuandika Kiswahili au Kiingereza.
“Haki ya wananchi kumwajibisha mbunge kabla ya
miaka mitano imeondolewa kutokana na mapendekezo ya kamati na wajumbe na
watafanya hivyo baada ya miaka mitano,” alisema.
Rasimu hiyo imembana mgombea binafsi wa ubunge
kwamba atakoma kuwa mbunge pale tu itakapotokea amejiunga na chama
chochote cha siasa nchini.
Pendekezo la Warioba la kutaka Spika wa Bunge na Naibu wake
wasitokane na wabunge wa Bunge la Jamhuri au kuwa viongozi wa juu wa
vyama, nalo limewekwa kando na badala yake spika kupendekezwa achaguliwe
miongoni mwa wabunge au kutoka kwa Watanzania wenye sifa ambao
watajitokeza kuomba nafasi hiyo kama ilivyo sasa.
Hata hivyo, Chenge alisema wamependekeza Naibu Spika ni lazima atoke miongoni mwa wabunge.
Mgombea binafsi
Chenge alisema pamoja na kwamba mgombea huru wa
nafasi ya urais ni haki ya kikatiba, lakini kamati yake imelazimika
kuchukua tahadhari na kuweka masharti juu ya mgombea huyo.
Masharti hayo ni pamoja na kuweka kipengele katika
Katiba kinacholitaka Bunge kutunga sheria itakayoweka masharti ya
mgombea huru ikiwamo idadi ya watu watakaohitajika kumdhamini.
Pia sheria hiyo itaweka sharti la lazima
linalomzuia kujiunga na chama chochote cha siasa, kuainisha vyanzo vya
mapato vya kugharimia kampeni zake na kuweka wazi ilani yake ya
uchaguzi.
Masuala ya kuingizwa kwa Mahakama ya Kadhi na
kuruhusiwa kwa uraia wa nchi mbili ambayo yaliwagawa wajumbe wa Bunge
hilo katika makundi mawili nayo hayakuingizwa katika rasimu hiyo.
Kuhusu Mahakama ya Kadhi, Chenge alisema kamati
yake imezingatia mijadala ya wajumbe, taarifa za kamati za Bunge hilo na
Katiba za nchi mbalimbali katika kufikia uamuzi huo.
Alisema katiba inayotungwa inahusu Mahakama Kuu,
Mahakama ya Rufani na Mahakama ya Juu hivyo masuala ya Mahakama ya Kadhi
yanaweza kusimamiwa na sheria inayohusu mahakimu.
Kuhusu suala la uraia pacha, Chenge alisema
waliozaliwa Tanzania lakini wakapoteza uraia na kuamua baadaye kurudi
nchini, watarejeshewa uraia wao baada ya kuukana uraia wa nje. Alisema
Watanzania wanaoishi nje ya nchi wakiwa na uraia wa nchi hizo,
watakapokuja nchini hawatakuwa na uraia wa nchi mbili, badala yake
watapewa hadhi maalumu.
Baada ya kukamilika kwa uwasilishaji huo,
Mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta alitoa fursa kwa wajumbe wa Bunge hilo
kuipitia Rasimu jioni na leo watakutana kwenye kamati zao 12 kwa lengo
la kuhakiki ni kwa kiasi gani waliyoyapendekeza wakiwa ndani ya kamati
na kwenye mijadala yamezingatiwa.
Kesho wajumbe wote watakutana katika Bunge zima
kwa lengo la kuhakiki kwa pamoja kuhusu yale yatakayoletwa na
sekretarieti kutoka kwenye kamati za Bunge hilo. Septemba 28, wajumbe
hao watakutana tena kwenye kamati kwa lengo la kupewa maelekezo ya namna
ya kukaa ndani ya ukumbi na pia namna watakavyopiga kura siku
inayofuata.
Sitta alisema upigaji wa kura utaanza Septemba 29 hadi Oktoba 2 na baada ya hapo itajulikana kama rasimu hiyo imepitishwa kwa wingi wa kura wa theluthi mbili kwa pande zote za Muungano au la.
Sitta alisema upigaji wa kura utaanza Septemba 29 hadi Oktoba 2 na baada ya hapo itajulikana kama rasimu hiyo imepitishwa kwa wingi wa kura wa theluthi mbili kwa pande zote za Muungano au la.
Chapisha Maoni