HOME
Tuufanyie kazi mpango wa EPZ ili kuongeza ajira
Maana yake ni kwamba hali ya uchumi nchini haikui vizuri, hivyo inashindwa kusaidia wengi kupata ajira.
Sekta ya huduma ndiyo inayochangia asilimia kubwa
(48%) ya uchumi wetu kwa sasa, huku sekta ya viwanda ikiwa inasuasua kwa
kuchangia ajira chini ya asilimia kumi. Hali imekuwa hivyo kwa takriban
miaka kumi hivi sasa.
Sekta ya huduma tuliyonayo ina kasoro nyingi ikiwamo kushindwa kuchochea maendeleo ya sekta nyingine za kiuchumi.
Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji (EPZA) ni
kati ya taasisi za Serikali zilizopewa kazi ya kuzalisha bidhaa kwa
ajili ya kuuza nje.
EPZ ni miongoni mwa mikakati ya Serikali yenye lengo la kuimarisha uchumi na kupunguza tatizo la ajira.
Historia inaonyesha mamlaka kama hizo kwa mara ya
kwanza zilianzishwa nchini Ireland miaka ya 50. Kufikia miaka ya 70,
mfumo huo ulikuwa umeenea katika maeneo mbalimbali duniani, ikiwamo Asia
ya Mashariki, Marekani ya Kusini na hata barani Afrika.
Pamoja na kwamba mfumo huu ulishika kasi kubwa barani Afrika katika miaka ya 80, Tanzania ilianzisha EPZ rasmi mwaka 2002/2003.
Malengo ya kuanzishwa EPZ ni pamoja na kuongeza
ajira, kupata fedha za kigeni, kuongeza ushindani wa bidhaa kwenye soko
la dunia, kusambaza teknolojia kwa wazalishaji wa ndani, kuunganisha
uchumi wa ndani na soko la dunia na kusindika mazao na bidhaa za ndani.
Hata hivyo, ukweli ni kwamba malengo yake yanaweza
kufikiwa iwapo mwekezaji aliyeko chini ya mfumo huu ananunua malighafi
kutoka kwenye viwanda vya ndani na kutoa mafunzo kwa watu wanaomsambazia
bidhaa kulingana na ubora wa mahitaji yake.
Mafanikio yanaweza kupatikana pia kama Serikali
itaweka mazingira rafiki kwa maana ya yale mazingira yanayofanya watu
kufanya biashara bila kusumbuliwa.
Korea Kusini na China ni miongoni mwa nchi
zilizofanikiwa sana kukuza uchumi, kuongeza ajira, kueneza teknolojia na
kutoa mafunzo kwa ajili ya mbinu bora za uzalishaji kwa watu wake
kupitia mfumo huu wa EPZ.
Hata hivyo, hali imekuwa kinyume kwa upande wa Tanzania EPZ,
kwani kadri miaka inavyokwenda ni kama wananchi hawaoni manufaa hasa ya
EPZ.
Taarifa ya Umoja wa Ushirikiano wa Maendeleo ya
Kiuchumi (OECD) iliyotolewa Februari mwaka huu inatanabaisha kuwa mfumo
wa EPZ umeshindwa kutimiza lengo la kuzalisha ajira za kutosha kwani kwa
takriban miaka 12 tangu kuanzishwa kwake, ni ajira 15,000 tu ndiyo
zimeweza kuzalishwa.
Mwaka 2012 taasisi isiyokuwa ya kiserikali la
STIPRO ambalo hujihusisha na tafiti za kisera katika masula ya sayansi,
teknolojia na ubunifu ilifanya utafiti kuangalia uwezo wa kampuni zilizo
chini ya mfumo wa EPZ katika kusambaza teknolojia kwenye sekta ya
viwanda ndani ya Tanzania.
Utafiti huo ulibaini kuwa kwa kwa kiasi kikubwa
wawekezaji walio chini ya EPZ wana uwezo mdogo kiteknolojia na
hujihusisha na kazi nyingi zisizohitaji maarifa makubwa kama vile
kukarabati magari kwa asilimia 32, kufungasha bidhaa kwa asilimia 4,
kushona nguo kwa asilimia 20, kusindika vyakula kwa asilimia 28, na
kadhalika.
Ilibainika pia kuwa wengi wa waajiriwa aidha
hawapati mafunzo ama hupewa mafunzo kwa muda mfupi; kwa mfano utafiti
ulibaini kuwa asilimia 48 ya waajiriwa, walipata mafunzo kwa muda wa
wiki moja hadi mbili.
Chapisha Maoni