Unknown Unknown Author
Title:
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
HOME Nyarubanja ya kisasa inavyowatesa wananchi masikini Nilikuwa Mvomero,mkoani Morogoro katika msitu wa akiba kwa ajili ya...
HOME

Nyarubanja ya kisasa inavyowatesa wananchi masikini

Nilikuwa Mvomero,mkoani Morogoro katika msitu wa akiba kwa ajili ya nishati. Ndani ya msitu huo kumejengwa makazi ya muda wenyewe wakisema kuwa wako humo kwa muda, kwani wanatakiwa kuondoka mara moja kwa vile huo ni msitu wa serikali na sio eneo la kujenga makazi.

Ukivuka barabara, unakutana na mbuga ya msitu unaoweza kusafiri kwa dakika kumi kwa gari bila kufika mwisho wake. Na tunaambiwa, huo msitu umenunuliwa na kigogo wa serikali akishirikiana na mfanyabiashara.

Huko mbele nako, kuna vigogo wamenunua maheka ya ardhi na kuamua kufuga ng’ombe, kutunza ardhi kama vihamba vyao kwa ajili ya kuiuza baadaye.

Wananchi hao, walijihamishia kwenye msitu huo wa serikali baada ya kufukuzwa na wanunuzi hao wa ardhi. Waliishi hapo, wengine , kwa zaidi ya miaka hamsini.

Na sasa wanatakiwa kuhama waende kokote wanakoweza kwa sababu eneo husika si rasmi kwa ajili ya makazi, bali ni sehemu ya hifadhi ya misitu.

Hawa wananchi sasa ni sehemu ya kundi kubwa la wananchi wanaohangaikia makazi na ardhi ya kulima kutokana na wajanja wachache wasioweza kufikiri ni athari na hasara yake, kuamua kujimegea mapande ya ardhi kwa mtindo ule wa zamani wa nyarubanja.

Nyarubanja ilikuwa kwa ajili ya wakubwa wa serikali katika kabila la Kihaya, na nyarubanja ya sasa ni ya wakubwa wale wale wakishirikiana na maswahiba wao wenye fedha wa nje na ndani ya nchi. Nyarubanja hii inatesa wananchi, na hasa wale masikini.

Nyarubanja hii, imekuwa ni moja ya sababu ya wananchi masikini kuhama kutoka maeneo yao ya asili kutafuta ardhi ya kulima, maeneo mengine na hivyo kusababisha kuvunjika kwa mila na desturi za watu na makabila yao.

Huko waendako, nako ardhi imekuwa tayari imemegwa na wenye meno na matokeo yake kupata eneo dogo na pengine kukosa, na kusababisha watu wasio na ajira katika maeneo ya vijijini.

Lakini kuhamahama huko, kunajenga hatari zaidi ya kuanzishwa kwa majangwa kwa sababu kila ardhi sasa inatakiwa kulimwa, au inavamiwa ili kulimwa kwa sababu, ile ambayo wangeweza kutumia kwa shughuli za kilimo imenunuliwa, imejaa watu na mfumo wenyewe wa kulima ni wa kizamani.

Nyarubanja hii, imesababisha wafugaji kuhamahama kwa sababu, mojawapo  kule wanaokotoka mashamba ya machungaji yamechukuliwa na wenye fedha.

Lakini huko wanakokwenda nako ardhi imechukuliwa na sijui wataendelea kuhamahama. Nilipokuwa wilayani Kilombero wakati Fulani, niliona makundi ya ng’ombe yakihamishwa kwa kile kinachodaiwa kuvamia maeneo oevu lakini sasa waende wapi, likawa ndio swali. Kila wanakokwenda wanaambiwa ni wavamizi.

Kwa hiyo tuna watu ambao wanaishi uhamishoni- internally displaced, kwa sababu za kuchukuliwa kwa ardhi kubwa kubwa na wenye fedha, kwa msaada na uhamasishwaji wa sera ya uwekezaji ambayo inahimiza wawekezaji wapewe ardhi mara moja.

Nyarubanja hii imesabbisha kupanuka kwa miji bila sababu, kwa sababu wenye fedha wananunua ardhi nje ya mji na hivyo kuupanua mji bila sababu za msingi; au wenye pesa wananunua viwanja katikati ya miji ili wajenge nyumba zao na hivyo kuwafukuzia wakazi pembezoni mwa miji ambako kunapanuka.

Hasara yake katika hili ni kubwa: miji inapanuka bila kwenda sambamba na uwezo wa halmashauri za miji wa kutoa huduma kama za afya, maji, shule, barabara nzuri,  ulinzi na burudani.

Mfumo huu wa nyarubanja, sasa inawamilikisha ardhi kubwa watu wachache, bila kuwajali wengi  wanaotakiwa kulindwa na sera na sheria na taratibu.

Kama serikali inataka kuokoa misitu, kuondoa magomvi, na kupunguza tatizo la ajira, nyarubanja hii ya kisasa izuiwe.
Email:malundelubuyi@gmail.com +25575052883

About Author

Advertisement

Chapisha Maoni

 
Top