HOME
Katiba
Balozi Sefue afunguka Katiba Mpya
Kauli ya Balozi Sefue imekuja ikiwa ni siku chache
tangu Rais Jakaya Kikwete kukutana na viongozi wa Kituo cha Demokrasia
(TCD) na kutoa uamuzi wa kuahirisha mchakato wa Katiba hadi baada ya
uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Suala la muundo wa muungano lilichukua mjadala
mkali ndani ya Bunge Maalumu la Katiba huku wajumbe wanaounda kundi la
Ukawa wakiunga mkono mapendekezo ya Rasimu ya Katiba ya muundo wa
Serikali tatu na wajumbe wa CCM wakisisitiza muundo wa Serikali mbili.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti
hili, Balozi Sefue alisema mchakato wa Katiba unahitaji maridhiano,
lakini suala la muundo wa muungano halina maridhiano katika jamii hivyo
litachelewesha upatikanaji wa Katiba:
“Katika historia ya nchi yoyote, wakati unafika
wananchi wakawa na maridhiano fulani, wakaamua kuyaingiza ndani ya
Katiba. Tatizo linajitokeza pale watu au makundi fulani
yanapong’ang’ania kuingiza ndani ya Katiba mambo ambayo ni dhahiri
hayana maridhiano ndani ya jamii. Mfano ni suala la muundo wa Muungano,”
alisema na kuongeza:
“Uzoefu wa Bunge Maalumu hadi sasa ni kuwa hakuna
uwezekano wa kupata maridhiano ya kubadili muundo wa Muungano kutoka
Serikali mbili kwenda tatu. Hutapata maridhiano hayo ndani ya Bunge
Maalumu na hutapata maridhiano ukienda kwa wananchi,” alisema.
Alisema anaamini wajumbe wa Bunge Maalumu
walifanya uamuzi wa busara kuliweka kando jambo hilo linalotugawa, na
kuendelea kujadili Rasimu ya Katiba kwa msingi wa mfumo uliopo wa
Serikali mbili,” alisema.
Balozi Sefue aliongeza kuwa tangu suala hilo liwekwe kando kumekuwa na kasi na matumaini ya kupata Katiba Mpya.
Alisema jambo hilo ni kubwa na uzoefu unaonyesha lina uwezo mkubwa wa kutugawa na kuchelewesha kupatikana kwa Katiba Mpya.
Balozi Sefue alisema Tume ya Mabadiliko ya Katiba
iliamini yatapatikana maridhiano kuhusu kubadili muundo wa Muungano,
ilivyo sasa, ni wazi kuwa maridhiano kuhusu mabadiliko hayo hayapo na
hayatapatikana.
“Hakuna idadi ya makongamano na maandamano yatakayobadili hali hiyo sasa,” alisema.
Licha ya kusema kuwa kuna matumaini ya kupata
Katiba Mpya, Balozi Sefue alisema ikishindikana Katiba iliyopo
itafanyiwa marekebisho ili ituvushe hadi mchakato utakaporejeshwa tena.
“Naelewa hisia za wanaokata tamaa kuwa pengine tunapoteza muda
na fedha, lakini ni jambo la kawaida kwa mchakato wa kutunga Katiba
kupita katika misukosuko. Jambo muhimu la kuzingatia ni kuwa Katiba ni
maridhiano ndani ya jamii kuhusu namna wananchi wanavyotaka kutawaliwa.”
Ajivunia utawala wa Rais Kikwete
Kuhusu utendaji wa Rais Jakaya Kikwete, Balozi
Sefue amesema kuwa Watanzania wana bahati ya kuongozwa na Rais huyo
akisema kuwa amefanya mambo makubwa katika utawala wake.
“Kwanza niseme kuwa Watanzania tunayo bahati sana,
kipindi cha awamu hii kumekuwa na mivutano mingi ya kisiasa, ndani ya
vyama na baina ya vyama. Kila mivutano hii ilipotokea, Rais Kikwete
alifanikiwa kuturudisha kwenye mstari,” alisema na kuongeza.
Alisema uchumi umeendelea kukua kwa viwango kati
ya asilimia sita na saba, na sasa tuko tayari kuvuka hapo na kuelekea
asilimia nane na mfumuko wa bei umedhibitiwa vya kutosha na unaweza kuwa
wastani wa asilimia tano kabla awamu hii haijamaliza muda wake.
Sefue alisema pato la wastani la kila mtu kwa mwaka sasa limefikia dola 742 kwa bei za Dola ya Marekani sawa na Sh1,200,000.
Aliendelea kusema kuwa takwimu za Sensa ya Makazi
na Watu ya 2012 imeonyesha ongezeko kubwa la hali ya maisha na kwamba
wastani wa umri wa kuishi umefikia miaka 61 huku idadi ya wananchi walio
katika umaskini uliokithiri sasa ni chini ya asilimia 10, na wenye
umaskini wa mahitaji ya msingi ni chini ya asilimia 30.
“Hivyo siyo kweli kuwa uchumi wetu unakua kwa
tarakimu tu, bali yapo mabadiliko ya wazi katika ubora wa maisha ya
wananchi walio wengi.”
Aligusia pia eneo la uchumi akisema kumekuwa na
juhudi za kuondosha vikwazo vya uchumi kukua na kupanua fursa za
wananchi kujiendeleza. Amevitaja vikwazo vilivyowekewa mkazo ni
miundombinu, hususan barabara, bandari, reli, umeme na maji.
“Kwenye kila pembe ya nchi utaona kazi
zinazoendelea za kujenga barabara za lami na changarawe, na kuwekeza
kwenye kufua, kusafirisha na kusambaza umeme,” alisema.
Balozi Sefue alisema uzoefu unaonyesha kuwa
ukishawapatia wananchi barabara nzuri, umeme wa uhakika na maji,
yanatokea mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kijamii katika kila jamii
husika.
Alisema mwaka 2002 ni asilimia 10 tu ya wananchi
walipatiwa umeme, leo umeme umewafikia asilimia 36 ya wananchi, na
asilimia 24 tayari wameunganishiwa umeme.
Ametaja pia mafanikio katika sekta ya elimu na huduma za jamii
ikiwa pamoja na uboraji wa shule za msingi wa sekondari na elimu ya juu.
“Elimu ya juu imepanuka sana. Chuo Kikuu kipya na
kikubwa sana cha Serikali kimejengwa Dodoma, pamoja na Taasisi ya Nelson
Mandela kule Arusha, Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Mbeya na
Chuo Kikuu cha Kilimo kinachopangwa kujengwa Butiama pamoja na Kampasi
mpya ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili kule
Mloganzila, ni mifano ya wazi,” alisema na kuongeza:
“Kwenye afya tunapiga hatua kubwa kupunguza kasi
ya Ukimwi na malaria na kupunguza sana vifo vya watoto chini ya umri wa
miaka mitano, na kadhalika.”
Utawala Bora
Kuhusu utawala bora, Balozi Sefue amemwagia pia
sifa Rais Kikwete kwa kuziimarisha taasisi zake ambazo ni na kuongeza
matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano, vitendea kazi, majengo
na mafunzo ya mahakama, taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru), Tume ya Maadili ya Umma na Sekretarieti yake, Ofisi ya
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na Ofisi ya Mkurugenzi wa
Mashtaka.
“Kwenye ulinzi na usalama, ameongeza na kuboresha
sana mazingira ya kufanyia kazi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa
Tanzania, yakiwamo masilahi, mafunzo na silaha za kisasa; amerejesha
Jeshi la Kujenga Taifa kwa mujibu wa sheria; na ameanzisha maboresho
makubwa ya Jeshi la Polisi, miongoni mwa mengine mengi,” alisema.
Kustaafu
Kuhusu kustaafu kwake, Balozi Sefue anasema amefanya kazi kwa muda mrefu na angependa kupumzika baada ya kustaafu.
“Kazi ya Katibu Mkuu Kiongozi ina msongo wa
mawazo. Natarajia kupumzika baada ya kustaafu. Lakini nitatumia muda
mwingi kusoma,” anasema.
Alisema ana vitabu vingi alivyonunua ambavyo
hakupata nafasi ya kuvisoma na pengine anaweza kuandika vitabu pia na
hana nia ya kuingia katika siasa.
Kuporomoka kwa maadili
Balozi Sefue alikiri kuporomoka kwa maadili kwa
baadhi ya watumishi wa umma akisema ni matokeo ya tabia kama hiyo kwa
jamii nzima:
“Zipo sababu nyingi za kuporomoka kwa maadili, siyo Tanzania tu bali duniani kote,” alisema.
Alisema malezi ni eneo moja linaloweza kusaidia;
malezi ndani ya familia, na malezi kwa maana ya elimu shuleni, vyuoni na
Jeshi la Kujenga Taifa, na elimu kwa maana ya mafundisho ya dini,”
alisema na kuongeza:
“Utandawazi nao ni tatizo, hasa utandawazi wa
utamaduni. Teknolojia ya Habari na mawasiliano, televisheni, mitandao ya
kijamii social media, vyote vinachangia kuwapa vijana wetu, hata watu
wazima, tamaa ya aina ya maisha ambayo ni nje ya uwezo wao.”
“Uchumi unavyokua, na bidhaa za kila aina
zinapojaa madukani zinavutia macho na kuchangia watu kukosa subira na
kuvitaka vitu hivyo leo, hata kama ni kwa vipato visivyo halali. Kwa
usahihi, ingefaa kuwa tamaa ya maisha bora na kumiliki vitu vizuri iwe
kichocheo cha kujituma na kuongeza kipato kwa njia halali, na si kwa
njia ya mkato ya rushwa,” aliongeza.
Mawaziri mizigo
Kuhusu mawaziri mizigo, Balozi Sefue amekanusha
kutoa kauli kwamba hakuna mawaziri mizigo kabla Rais Kikwete
hajabadilisha Baraza la Mawaziri, bali aliitoa baada ya kuulizwa swali
na mwandishi wa habari wakati akitangaza mabadiliko hayo:
“Msingi wa swali hilo ulikuwa kwamba baadhi ya
mawaziri waliobakizwa ndani ya Baraza walikuwa miongoni mwa waliotajwa
kuwa mizigo. Kwa bahati mbaya baadhi ya vyombo vya habari vilipotosha
nilichosema,” alisema na kuongeza:
“Nilichosema ni kuwa Waziri anaitwa mzigo kwa vile
inaonekana kuwa yapo mambo kwenye Wizara anayoiongoza ambayo hayaendi
vizuri. Inawezekana Waziri ni tatizo, lakini inawezekana pia tatizo liko
nje ya uwezo wake, kama vile uhaba wa fedha.”
“Jambo la pili ni kama Waziri huyo anaonekana kuwa
anaelewa tatizo lililopo na anao mpango unaoridhisha wa
kulishughulikia. Ikiwa hivyo ndivyo, Rais anaweza kumpa fursa nyingine
ya kulishughulikia. Lakini si kweli kuwa nilisema hakuna mawaziri
mizigo. Sikusema hivyo hata kidogo, na kwa maana hiyo sijapingana na
yaliyosemwa na viongozi wa CCM.”
Chapisha Maoni