HOME
Mbinu mpya za kusafirisha dawa za kulevya
Dar es Salaam. Baadhi ya
wanawake wa Kitanzania waliofungwa katika magereza ya China na Hong
Kong, walishika ujauzito kama moja ya mbinu ya kupitisha dawa za kulevya
bila kugundulika kwenye viwanja vya ndege na mipaka mingine ya
kimataifa. Mwananchi limebaini.
Watanzania wanne walio katika magereza ya China na
Hong Kong walijifungua watoto kwa nyakati tofauti wakiwa wanatumikia
vifungo na wamekiri kuwa walibeba ujauzito kama mbinu ya kupitisha dawa
hizo bila kukaguliwa.
Watoto wanaozaliwa magereza baada ya kufikisha
mwaka mmoja hupelekwa katika vituo vya watoto yatima na kusomeshwa na
Serikali ya China hadi pale wazazi wao watakapomaliza adhabu.
Imebainika kuwa watoto wawili wapo katika vituo
hivyo, mmoja tayari yupo Tanzania baada ya bibi yake kumrejesha na
mwingine bado yupo gerezani na mama yake.
Wanawake hao ambao wote wana umri wa kati ya miaka
20 na 30 walieleza masikitiko yao jinsi ambavyo wafanyabiashara wakubwa
wa dawa za kulevya wanavyowarubuni ili kubeba dawa hizo kwa ahadi za
kuwapa fedha nyingi.
“Tunapata mimba makusudi kwa sababu tulijua kuwa
katika viwanja vya ndege vingi wajawazito hawakaguliwi hasa wakiwa na
mimba kwa hiyo tungebeba unga na kuupeleka China, halafu baadaye
tungerudi nchini na kutoa mimba au tukiamua tunajifungua,” alisema mmoja
wa wafungwa hao.
Hata hivyo, mbinu hiyo ilifanikiwa katika Uwanja
wa Ndege Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), lakini haikufua dafu katika
viwanja vya ndege vya China, Hong Kong, Macau na Guang Zhou.
Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna
Diwani Athuman alisema hana taarifa za Watanzania hao lakini ofisi yake
inafanya taratibu za kuwasiliana na China ili kujua hali za wanawake
hao.
Mkurugenzi wa JNIA, Moses Malaki alisema kwa
kawaida kila mtu hukaguliwa kwa uangalifu bila kujali mjamzito au la.
Akielezea namna wanavyopimwa, Malaki alisema kwanza kila msafiri hupimwa
kwa mashine ya kawaida ambayo hubaini uwepo wa kifaa chochote
kisichotakiwa mwilini kwa mfano chuma kama hereni, bangili, mikanda
lakini si ndani ya tumbo.
“Iwapo mashine ya awali itatoa mlio hata baada ya
msafiri kutoa vitu vya chuma, basi atatakiwa kwenda katika chumba
maalumu cha ukaguzi wa mikono,” alisema.
Kamanda wa kitengo cha Polisi cha Dawa za Kulevya,
(SACP), Godfrey Nzowa alisema wapo wanawake kadhaa raia wa Zambia,
Zimbabwe, Nigeria, Afrika Kusini na Malawi ambao wamefungwa katika
magereza ya Tanzania kwa kusafirisha dawa za kulevya wakitumia mbinu
hiyo ya ubebaji wa mimba.
Alisema mbinu hizo zinatumiwa na wanawake kwa
sababu wajawazito hawakaguliwi kwa mashine za x-ray na kwamba wengi
walikamatwa kutokana na taarifa za kikachero.
“Hata magereza ya hapa tunao na wamejifungua watoto wakiwa
gerezani, lakini wajue kabisa kuwa watakwepa mashine lakini taarifa
zinatusaidia na ndiyo maana nasema taarifa ni nguvu,” alisema.
Pamoja na kukamatwa kwa raia wa kigeni wanaotumia
mbinu hiyo, Kamishna Nzowa hakuwa na taarifa za Watanzania waliokamatwa
nje ya nchi kwa kutumia mbinu hiyo.
Septemba mwaka jana, raia wa Canada, Tabitha
Ritchie alikamatwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Columbia kwa kubeba dawa za
kulevya kwenye mimba ya bandia, mbinu ambayo ilibainika baada ya
kuhojiwa na maofisa wa uhamiaji kuhusu umri wa mimba yake na walipomgusa
tumboni walibaini kuwa tumbo lilikuwa baridi na gumu.
Askari mmoja wa Kitengo cha Dawa za Kulevya wa
JNIA, (jina linahifadhiwa), alieleza wazi kuwa hakuna mashine ya kujua
mtu aliyemeza dawa hizo zaidi ya kuhisi tu kwa mbinu za kiaskari.
Alisema mara nyingi watu waliomeza dawa hizo
hukamatwa kwa kuhisiwa na baada ya kupekuliwa huamriwa kuruka kichura au
kujisaidia ili kujua iwapo wana ‘mzigo’ tumboni.
Hata hivyo, askari huyo alisema kwa kawaida
wajawazito hawawezi kurushwa kichura au kulazimishwa wajisaidie kutokana
na hali zao.
Miongoni mwa wanawake waliobeba mimba kwa ajili ya
kubeba dawa za kulevya na wasichana maarufu nchini, mmoja wao mtoto
wake sasa analelewa katika kituo cha watoto yatima China.
Baada ya kupata taarifa hizo, Mwananchi
ilizitafuta familia za wafungwa hao ambazo hazikuwa na taarifa kuwa na
ndugu zao walikuwa na ujauzito walipokuwa wakisafiri.
Baadhi ya waliohojiwa walisema walipata taarifa za ndugu zao kuwa na watoto wachanga lakini hawakuwa na habari za ujauzito.
“Hata hivyo, ninamshukuru Mungu kwa kuwa amepata
mtoto na anaendelea vizuri, kutokana na uwezo wetu kuwa mdogo siwezi
kwenda kumchukua mjukuu wangu huko Hong Kong, mwache akae kituoni hadi
mama yake atakapoachiwa,” alisema mama wa mmoja wa wafungwa hao.
Chapisha Maoni