MBUNGE HALIMA MDEE (CHADEMA), AMEMTAKA MBUNGE MWENZAKE, LETICIA NYERERE, AACHE UBUNGE NA AKAJIUNGE CCM
MBUNGE wa Kawe, Halima Mdee (CHADEMA), amemtaka mbunge mwenzake, Leticia
Nyerere, aache ubunge na akajiunge na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuliko
kuendelea kukipigia debe chama hicho akiwa upinzani.
Kauli hiyo ameitoa jana alipokuwa akichangia bajeti ya serikali kwa
mwaka 2014/2015 ambapo alisema matendo anayofanya Leticia ya
kujipendekeza kwa CCM yatamgharimu kama ilivyotokea kwa wenzake.
Juzi wakati akichangia bajeti hiyo, Leticia alisema serikali ikifanya
vizuri, lazima ipongezwe kwakuwa imepeleka maendeleo katika jimbo
analotoka.
“Serikali yangu imefanya mambo mengi, imeniletea maji, walimu katika
jimbo langu la Kwimba, ni lazima tuipongeze si kila wakati tunailaumu
humu ndani,” alisema.
Katika mchango wake jana, Mdee, alisema jukumu kubwa la upinzani ni
kuikosoa serikali na kuonyesha mbadala katika masuala mbalimbali na si
kuisifia kwa kutekeleza wajibu wake wa kuwahudumia wananchi.
“Serikali inapata fedha kutokana na kodi za wananchi, inalazimika
kupeleka maji, barabara na huduma mbalimbali kwa lazima si hiyari,
tunapoikosoa tunatimiza wajibu wetu kama yenyewe inavyotekeleza
inapowahudumia wananchi.
“Leticia Nyerere anaweza kwenda CCM, kwakuwa Rais Kikwete ana nafasi
mbili za uteuzi wa wabunge, lakini lazima ajue waliojipendekeza CCM
wamepigika sana hivi sasa, aachie ubunge aende huko kwakuwa ana mapenzi
nao,” alisema.
Mdee alisema kuwa Leticia anaiaibisha kambi ya upinzani inayofanya kazi
usiku na mchana kuhakikisha serikali inaboresha huduma inazozitoa kwa
wananchi.
“Upinzani si lelemama, kama anafikiria CCM ni kuzuri zaidi ni vema akaenda huko kuliko kubakia hapa pasipomfaa,” alisema
Chapisha Maoni