Thursday, June 19, 2014
KESI TANO ZA MABILIONI USWISI ZACHUNGUZWA KATIKA SAKATA LA MABILIONI YALIYOFICHWA USWISS
Tanzania imeomba msaada kwa taasisi iitwayo International Centre for
Asset Recovery – ICAR (Kituo cha Kimataifa cha Urejeshaji Mali) ya
Uswisi kuchunguza kesi tano zinazohusu watu na taasisi zinazotuhumiwa
kuficha mabilioni ya fedha nchini humo.
Itakumbukwa kuwa baada ya kuibuka kwa sakata la mabilioni hayo ya
Uswisi, Serikali iliunda kikosi kazi chini ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, Jaji Fredrick Werema kulifanyia kazi.
Gazeti hili lilifuatilia suala hilo hadi Uswisi na kubaini kuanza kwa
uchunguzi huo, huku fedha nyingi zikitajwa kwamba zinatokana na vitendo
vya rushwa.
Akizungumza na mwandishi wetu mjini Bern, Uswisi hivi karibuni, Mtafiti
wa Sheria wa ICAR, Andrew Dornbierer alisema: “Tuna makubaliano na
Serikali ya Tanzania hasa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG),
tunachunguza kwa kina kesi za rushwa na utoroshwaji wa fedha, hivyo tuko
katika ukusanyaji wa taarifa. Siwezi kukupa mifano ya moja kwa moja kwa
sababu bado tunazifanyia kazi na tunadhibitiwa katika utoaji wa
taarifa.”
Mkurugenzi wa ICAR, Gretta Fenner Zinkernagel alithibitisha uwepo wa kesi hizo za Tanzania.
“Ni kweli tumeombwa na Serikali ya Tanzania kusaidia kuchunguza baadhi
ya kesi… zilikuwa zimeshachunguzwa lakini kutokana na uwezo wao mdogo
tunawasaidia. Kwa harakaharaka naweza kusema tunazo kesi tano hivi… ni
kesi za watu binafsi na taasisi na zinahusu masuala ya fedha. Hatuwezi
kutaja majina kwa sababu tunakatazwa kabisa na mkataba wetu na taasisi
tunazofanya nazo kazi.”
Licha ya kutotaja majina, Zinkernagel alisema wanaochunguzwa katika kesi
hizo wanahusishwa na kampuni hewa zilizoanzishwa kwa lengo la kuchota
fedha kisha kwenda kuzificha nje ya nchi.
“Kuna watu wenye masilahi binafsi na wamekuwa wakipokea rushwa au
wamekuwa wakitumia mashirika kwa ubia au kampuni kivuli na ushirika
mwingine wa kimataifa ili kusafirisha fedha kwenda kwenye kampuni fulani
kwa lengo la kuzificha. Ni kampuni zinazotumiwa na wafanyabiashara
kuhamisha fedha haramu na mwisho hujisafisha,” alisema.
Jaji Werema
Jaji Werema alikiri Tanzania kuiomba ICAR kufanya uchunguzi huo lakini
akakataa katakata kutaja watu wala kampuni zinazofanyiwa uchunguzi.
“Hatuwezi kutaja majina ya watu waliofunguliwa kesi kwa sababu kwanza
tutakuwa tumeingilia haki zao kisheria. Pili, tunaweza kuwataja lakini
baadaye ikabainika kuwa si kweli, bali ni tuhuma tu na wakaja kutushtaki
na tatu, tutakapowataja watu hao tuliowafungulia kesi tutaharibu
upelelezi wetu.
“Katika kesi hizi, kisheria, tunafanya kazi zetu kwa utaratibu ili
tusiharibu upelelezi na tupate mambo mengi. Mnadhani tumekaa kimya
hatufuatilii lakini tunafanya kazi yetu. Siku ikifika mtaona na
mtasikia.
Chapisha Maoni