HOME
Ijue historia ya Serikali za mitaa Tanzania
Serikali za mitaa ni chombo cha utawala wa umma,
kilichopewa madaraka ya kuamua na kuendesha shughuli zake katika sehemu
ndogo ya nchi au Taifa. Ifuatayo ni sehemu ya pili ya makala
inayoelezea historia ya Serikali za mitaa Tanzania.
Baada ya uhuru, Serikali za baadhi ya nchi za
Afrika kama vile Zaire (Congo Kinshasa), Uganda, Senegal na nyingine
nyingi ama zilifuta mfumo wa serikali za mitaa au kubadilisha mfumo wake
ulioanzishwa na Serikali za Kikoloni.
Kwa mfano, Serikali ya Tanganyika ya wakati huo
haikufuta mfumo huo mara moja. Badala yake ilizirithi serikali za mitaa
na kuzitumia kama nyenzo za kuleta maendeleo kwa misingi ya
kidemokrasia.
Katika kipindi cha miaka ya mwanzo ya uhuru,
yalikuwapo makundi matatu ya serikali za mitaa. Miongoni mwao ni zile
zilizoundwa chini ya Sheria Namba 72 ya mwaka 1926 zilizokuwa 47.
Aidha, chini ya Sheria Namba 333 ya mwaka 1953, zilikuwa 9 kwa mijini na 10 kwa vijijini.
Kundi la tatu lilikuwa ni la Manispaa ya Dar es Salaam, iliyoundwa na Sheria Na. 105 ya mwaka 1946.
Mwaka 1962 Sheria na 333 ilirekebishwa kwa kuondoa
mamlaka za wenyeji na mwaka 1963 Sheria Namba 13/62 ilipitishwa
kusitisha utawala wa machifu nchini.
Inaelekea kuwa uamuzi wa kufuta utawala wa machifu
nchini ulitokana na sababu kuu tatu. Serikali ya wananchi ilitaka
kujenga mfumo wa kidemokrasia wa Serikali za mitaa. Aidha, ilionekana
utawala wa machifu uliendeleza fikra za ukabila badala ya utaifa. Pia
ikumbukwe kwamba wengi wa machifu waliwekwa madarakani na serikali ya
kikoloni.
Kwa mantiki hiyo, machifu walikuwa kama mawakala
wa serikali ya kikoloni. Mfumo huu usingeweza kukubalika katika Serikali
iliyochaguliwa na wananchi.
Serikali ya wananchi ilikuwa na sera yake
madhubuti juu ya serikali za mitaa. Ilibidi ichukue hatua kadhaa katika
kutekeleza sera hiyo. Na hatua zilizochukuliwa ni:-
Kuanzishwa kwa uchaguzi wa madiwani katika
halmashauri zote zilizokuwa zimeandikishwa na serikali ya kikoloni,
Kuundwa kwa Halmashauri katika wilaya au miji ambayo zilikuwa
hazijaundwa.
Mafanikio ya Serikali za mitaa 1961- 1972
Katika kipindi kati ya mwaka 1962 na 1972 Serikali za mitaa zilipata mafanikio machache na matatizo kuwa mengi.
Majukumu ya halmashauri yaliongezeka kama vile usimamizi wa elimu ya msingi, matibabu, barabara na maji.
Ingawa halmashauri za wilaya zilikuwa na majukumu
mazito zaidi kuliko yale ya halmashauri za miji, inashangaza kuona kuwa
sehemu kubwa ya ruzuku kutoka Serikali Kuu kwenda kwa Serikali za mitaa
ilitolewa kwa halmashauri za miji.
Licha ya hali hiyo ya upendeleo kwa halmashauri za
miji, kwa jumla halmashauri za wilaya ziliweza kutekeleza majukumu yake
vizuri kwa kujikusanyia mapato kutokana na kodi na ushuru wa mazao na
wakati huo huo kuhudumia miradi mbalimbali ya huduma za jamii.
Katika kipindi hiki mapato ya halmashauri
yalishuka sana. Kushuka kwa uwezo wa halmashauri za wilaya kukusanya
mapato ni ishara ya kukumbwa na matatizo katika utekelezaji wa majukumu
yake.
Hivyo, halmashauri zikashindwa kutekeleza majukumu
yake kwa ufanisi. Hali hiyo ndiyo iliyojitokeza kwa serikali nyingi za
mitaa katika kipindi hiki cha mwaka 1962-1972. Matatizo yaliyozikabili
serikali za mitaa yalitokana na sababu zifuatazo:
Kama ilivyoelezwa hapo awali kwamba, serikali za
mitaa zilipewa majukumu mara baada ya uhuru na kwamba Serikali Kuu
ilikuwa na nia ya kuleta maendeleo ya haraka kwa watu wake. Lakini
vyanzo vya mapato kwa Serikali za mitaa vilikuwa vichache.
Halmashauri za wilaya, kwa mfano, ziliruhusiwa kukusanya mapato kutokana na kodi na ushuru wa mazao.
Ukusanyaji wa kodi kutoka kwa wananchi ulikuwa mgumu. Wananchi wengi walikuwa wakikwepa kulipa kodi ya kichwa.
Ilikuwa kama kero kwao na kusababisha matukio ya
aibu na hata maafa. Kutokana na matukio hayo, Serikali Kuu iliamua
kufuta kodi ya kichwa.
Aidha, ilipofika Mei, 1969 ushuru wa mazao nao
ulifutwa. Uamuzi huo katika masuala mawili uliathiri kwa kiasi kikubwa
mapato ya serikali za mitaa nchini.
Licha ya kwamba Serikali za mitaa zilitegemea zaidi misaada na
ruzuku kutoka Serikali Kuu baada ya vyanzo kadhaa vya mapato yake
kufutwa, pia katika kipindi hicho hicho Serikali Kuu ilipunguza ruzuku
kwa serikali za mitaa.
Uamuzi huu ulitokana na sababu kwamba Serikali Kuu
ilichukua baadhi ya majukumu ambayo hapo awali yalikuwa ya serikali za
mitaa. Mifano ya majukumu hayo ni ulipaji wa mishahara ya walimu wa
shule za msingi wa Daraja “A” na “B” na ununuzi wa vifaa vya kufundishia
na kusomea.
Wizara nyingine, kama Afya, Ujenzi na Madini nazo
pia zilichukua baadhi ya majukumu ya Serikali za Mitaa. Kutokana na
upungufu wa mapato, halmashauri nyingi zilishindwa kutekeleza majumumu
yao kwa ufanisi, hali ambayo ililaumiwa sana na Serikali Kuu.
Chapisha Maoni