HOME
Kihunzi kingine cha Katiba inayopendekezwa
Dar/Zanzibar. Katiba
inayopendekezwa itakutana na kihunzi kingine katika utekelezwaji wake
kutokana na Zanzibar kutakiwa kubadili Katiba yake, zikiwamo ibara
zilizobeba msingi wa mabadiliko ya 10 katika Katiba ya Zanzibar.
Mabadiliko hayo ya mwaka 2010, kwa kiasi kikubwa
yanakinzana na Katiba ya sasa ya Muungano pamoja na Katiba
inayopendekezwa ambayo inakabidhiwa leo kwa Rais Jakaya Kikwete na Rais
wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein mjini Dodoma.
Ili Katiba inayopendekezwa iweze kutekelezeka ni
lazima Zanzibar ifanyie mabadiliko Katiba yake kwa kuwa Katiba ya
Muungano ndiyo Sheria Kuu.
Hata hivyo, wachambuzi wanahoji iwapo mabadiliko
hayo yatawezekana kirahisi kwa kuwa yanatakiwa kuidhinishwa kwa kura ya
maoni ya wananchi wa Zanzibar, baada ya kupita kwenye chungu cha Baraza
la Wawakilishi na kuamuliwa kwa theluthi mbili za kura.
Tofauti zilizopo
Mosi, Katiba ya Zanzibar inatamka kwamba Zanzibar
ni nchi ambayo eneo la mipaka yake ni lote la visiwa vya Unguja na Pemba
pamoja na visiwa vidogo vilivyoizunguka na bahari yake ambayo kabla ya
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ikiitwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.
Ibara ya pili inaitambua Zanzibar kuwa miongoni mwa nchi mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Masharti hayo ni kinyume na Katiba inayopendekezwa
ambayo katika ibara yake ya kwanza inatamka kuwa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ni nchi yenye mamlaka kamili ambayo imetokana na Muungano wa
nchi mbili za Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar
ambazo kabla ya Hati ya Makubaliano ya Muungano ya tarehe 22 Aprili,
1964 zilikuwa nchi huru.
Pili, Katiba ya Zanzibar katika Ibara ya 26
inatamka kwamba Rais wa Zanzibar ni Mkuu wa nchi ya Zanzibar, jambo
ambalo ni kinyume na Katiba inayopendekezwa katika Ibara ya 80 (2)
ikisema; Rais wa Jamhuri ya Muungano atakuwa Mkuu wa Nchi, Kiongozi wa
Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Amiri Jeshi Mkuu.
Tatu, Katiba ya Zanzibar katika Ibara ya pili A
inatamka kwamba kwa ajili ya utekelezaji bora wa shughuli za Serikali,
Rais anaweza kuigawa Zanzibar katika mikoa, wilaya na maeneo mengineyo
kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria iliyotungwa na Baraza la
Wawakilishi.
Masharti hayo ni kinyume cha Katiba
inayopendekezwa Ibara ya 2(2) ambayo inatamka: “Rais wa Jamhuri ya
Muungano atakuwa na mamlaka ya kuigawa Jamhuri ya Muungano katika mikoa,
wilaya na maeneo mengine, isipokuwa kwa upande wa Tanzania Zanzibar,
Rais atashauriana na Rais wa Zanzibar kabla ya kuigawa Tanzania Zanzibar
katika mikoa, wilaya au maeneo mengine.
Nne, Katiba ya Zanzibar katika Sura ya 3 Ibara ya 24(3) inasema:
“Rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu (Zanzibar) katika shauri
lililofunguliwa dhidi ya masharti ya Sura hii ya Katiba yatasikilizwa na
Mahakama Kuu (Zanzibar) mbele ya majaji watatu bila ya kumjumuisha Jaji
aliyeamua shauri hilo mara ya kwanza.
Majaji hao watatu watateuliwa na Jaji Mkuu na
uamuzi wao utakuwa ni wa mwisho na hautokatiwa rufaa kwenye Mahakama ya
Rufaa ya Tanzania.
Masharti hayo ni kinyume na Katiba inayopendekezwa
Ibara ya 167(1)(2) na(3) ambazo zinatamka kwamba: “(1) Kutakuwa na
Mahakama ya Jamhuri ya Muungano, (2) Mahakama ya Jamhuri ya Muungano kwa
mujibu wa Katiba hii na sheria nyingine yoyote, itatekeleza mamlaka
yake kupitia Mahakama ya Juu na Mahakama ya Rufani na (3) Mahakama ya
Jamhuri ya Muungano itakuwa ni chombo chenye mamlaka ya mwisho ya utoaji
haki katika Jamhuri ya Muungano.
Mahakama ya Juu na Rufani ndiyo zenye Mamlaka ya juu ya kutoa haki nchini na uamuzi wake ni wa mwisho.
Sita, kuhusu masharti ya fedha yahusuyo SMZ ambayo
Katiba ya Zanzibar Ibara ya 104(1) inasema: “Kutakuwa na mfuko mkuu wa
hazina ambao bila ya kuathiri sheria nyingine yoyote inayotumika,
zitawekwa fedha zote zitakazopatikana kutokana na njia mbalimbali kwa
ajili ya matumizi ya SMZ.
Hata hivyo, Katiba inayopendekezwa katika Ibara ya
251 inasema: “Serikali ya Jamhuri ya Muungano itatunza akaunti maalumu
itakayoitwa “Akaunti ya Fedha ya Pamoja” na ambayo itakuwa ni sehemu ya
Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano, ambamo
kutawekwa fedha yote itakayochangwa na Serikali mbili kwa kiasi
kitakachoamuliwa na Tume ya Pamoja ya Fedha kwa mujibu wa sheria
itakayotungwa na Bunge, kwa madhumuni ya shughuli za Jamhuri ya Muungano
kwa Mambo ya Muungano.
Maoni ya wadau
Kutokana na mgongano huo, wanasheria, wanasiasa na
wananchi wa Zanzibar wametoa maoni tofauti; baadhi wakieleza kuwa iwapo
itapitishwa kuna hatari ya kuibuka mgogoro wa kikatiba baina ya pande
mbili za Muungano.
Akizungumzia tofauti hizo, Mwenyekiti wa iliyokuwa
Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba alisema ingawa Katiba
inayopendekezwa imetaja mambo kadhaa mazuri, utekelezaji wake
unategemea zaidi mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar na ina maswali mengi
kuliko majibu hasa kuhusu muungano na mgombea binafsi.
Alisema licha ya Zanzibar kuridhia mambo kadhaa
kuwekwa katika orodha ya mambo ya Muungano, hali inaweza kuwa tofauti
ukifikia wakati wa Zanzibar kubadili Katiba yao ili kuwezesha
utekelezaji wa mabadiliko hayo.
Pia, aligusia suala la kodi ya mapato, ushuru wa
forodha na bidhaa kuwa mambo ya Muungano na kufafanua kuwa kwa
mabadiliko hayo, Zanzibar itashindwa kutekeleza mambo mengi licha ya
kupewa uwezo wa kusimamia mambo yake, kwa sababu mapato yake yanaingia
kwenye mfuko wa mapato ya muungano.
Mwakilishi wa Mji Mkongwe (CUF), Ismail Jussa alisema msimamo wa
Zanzibar umeshahitimishwa na Mwanasheria Mkuu wake, Othman Masoud
Othman wakati alipopiga kura ya ‘hapana’ kwa mambo yanayohusu Muungano.
“Hatuko tayari kufanya marekebisho na ikitokea labda kuongeza mamlaka zaidi kwa Wazanzibari.”
Mbunge wa Uzini (CCM), Muhammed Seif Khatib alisema kwa kifupi, “Sina majibu kwa hilo, siwezi kujibu kwa kipindi hiki.”
Mbunge wa Tumbatu (CCM), Juma Othman Ali alisema:
“Rasimu inayopendekezwa haina tatizo na itapita kwani hakuna tatizo
lolote na wananchi hawana sababu ya kutoipitisha.”
Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Zanzibar), Vuai Ali Vuai
alisema mchakato wa Katiba unakwenda hatua kwa hatua na jambo ambalo
lipo mbele ni kuipitisha Katiba inayopendekezwa kisha itafuatiwa na
kuibadili Katiba ya Zanzibar.
“Hatua ya kwanza ni kuipitisha Rasimu kuwa Katiba
na ili ipite ni lazima ipitishwe na Wazanzibari na kama ndiyo hivyo
wameipitisha hiyo, hata Katiba nayo watakubali kuifanyia marekebisho
kulingana na masharti,” alisema.
Kuhusu kura ya hapana ya Mwanasheria Mkuu, Vuai
alisema, “Kura yake moja ni ndogo sana, kuna kura zaidi ya 150 zilipigwa
pale bungeni, moja haiwezi kuharibu chochote katika huu mchakato,
alipiga kadri alivyoona inafaa na sioni kama ni shida.”
Rais wa Chama cha Wanasheria Zanzibar, Awadhi Ali
Said alisema kabla ya kufanyika marekebisho hayo, Wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi Zanzibar (BLW), watalazimika kupiga kura kupitisha muswada
wa marekebisho ya Katiba kwa mujibu wa Kifungu cha 4 na 80 cha Katiba
yake na lazima theluthi mbili ipatikane.
Alisema baada kupitishwa na Baraza hilo ndipo SMZ
inaweza kuitisha kura ya maoni kwa wananchi lakini iwapo hatua ya awali
itakwama wakati Rasimu ya Katiba ya Muungano imepitishwa, mgogoro mkubwa
wa kikatiba utaibuka.
Mwanasheria Mkuu wa zamani (SMZ), Hamid Mbwezeleni
alisema suala la Katiba ya Zanzibar kufanyiwa marekebisho hakuna
mjadala iwapo Katiba inayopendekezwa itapitishwa.
Alisema kuwa Katiba ya Muungano ndiyo Katiba mama
hivyo vifungu vya katiba ya Zanzibar vinavyogongana na ile ya Muungano
vitalazimika kufutwa.
Mbwezeleni alisema marekebisho ya 10 ya Katiba ya Zanzibar yanawanyima haki wananchi ya kutumia Mahakama za juu za rufaa.
“Kama tunakubali Muungano tukubali na mambo mengine, suala la
Katiba ya Zanzibar kufanyiwa marekebisho halikwepeki katika mazingira ya
Serikali mbili,” alisema.
Katibu wa Bavicha Zanzibar, Francis Warema alisema
mgogoro wa kikatiba unanukia kwa vile hakuna Mzanzibari atakayekubali
Zanzibar kuondolewa hadhi yake ya kuwa ni nchi.
Mkazi wa Mwembemakumbi, Masoud Othman Said (49)
alisema muda wa kufanya marekebisho ya Katiba ya Zanzibar upo, jambo la
msingi lazima iwepo nia njema.
Alisema kinadharia, Katiba ya Zanzibar imetoa
hadhi ya Zanzibar kuwa nchi lakini kivitendo huwezi kuwa na nchi bila ya
kuwa na uraia, ulinzi, sarafu, ardhi pamoja na sifa za kujiunga na
jumuiya za kimataifa ikiwamo Umoja wa Mataifa.
Imeandikwa na Fidelis Butahe, Ibrahim Yamola na Mwinyi Sadallah
Chapisha Maoni