HOME
Tangu lini kura iliyopigwa jana ikarudiwa kesho yake?
Wiki iliyopita Bunge la Katiba lilipitisha
Katiba waliyoipendekeza, badala ya ile ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba
iliyokuwa chini ya Jaji Joseph Warioba na kuwashawishi Watanzania
waipigie kura ya ndiyo.
Msingi hasa wa Bunge hilo kujitengenezea rasimu
yao, ni kwamba waliamini mambo mengi yaliyoandikwa kwenye Rasimu ya
Warioba kwamba hayakuwa sahihi na wakimlaumu mwanasiasa huyo mkongwe kwa
maelezo kuwa hakutumia busara kuandaa Katiba hiyo.
Hata hivyo, inavyofahamika ni kwamba Warioba na
wenzake waliandika rasimu hiyo kutokana na mapendekezo ya wananchi.
Walizunguka maeneo mbalimbali ya nchi, kukusanya maoni ya matakwa ya
wananchi, kazi iliyogharimu nchi zaidi ya Sh60 bilioni.
Rasimu hiyo ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya
Jaji Warioba ilikataliwa na wajumbe wa Bunge la Katiba na kuamua
kupendekeza ile ya kwao, ambayo ni ya kundi la wachache wenye nguvu.
Kitu kinachoweza kuonekana ni kuwa kulikuwa na
ubabaishaji mwingi katika mchakato mzima wa kupatikana Katiba hiyo
iliyotungwa na wajumbe wachache katika Bunge hilo.
Swali la kujiuliza ni kuwa tangu lini mtu anapiga kura leo, halafu kesho yake anasema jana nilikosea, naomba nipige tena kura.
Hata kama ni kanuni ziliwekwa hivyo, inaonyesha ni
namna gani watungaji wa kanuni hawakuwa makini au katika kuzingatia
demokrasia.
Binafsi, sijawahi kuona aina hii ya upigaji kura kwamba mtu akishapiga kura, huruhusiwi kurudia kwa namna yoyote ile.
Kokote kule duniani au hata hapa nchini, nje ya
mazingaombwe hayo ya Bunge la Katiba, ni wapi unaweza kupiga kura kwa
jambo fulani, halafu ukarudia na kusema nilichagua kwa makosa?
Ndani ya Bunge la Katiba ni kama hapakuwa na
hekima katika kujadili mambo kwa uwazi na matokeo yake ndiyo kuwaruhusu
waliopiga kura jana, kurudia siku ya pili yake kama ilivyokea kwa baadhi
ya wajumbe, akiwamo Mzee James Mapalala ambaye siku ya pili alisimama
bungeni humo akiomba apige kura upya kwa maelezo kuwa alipiga kura
kimakosa siku iliyotangulia.
Ni sawa, tunaambiwa kanuni iliruhusu hivyo, lakini
ndio nasema kwa namna inavyoonekana ni kama walioiweka kanuni hiyo
walikuwa na sababu zao ambazo kimsingi zilikuwa na kasoro.
Mchakato wa kutafuta Katiba umekuwako kwa muda
mrefu, muda wote huo Mapalala na wenzake kwanini hawakuwa na uwezo wa
kufikiri wapige kura upande gani, hadi leo wanapiga kura, halafu kesho
yake wanabadili na kusema naomba nipige kura tena jana nilikosea?
Niwashauri viongozi na wote wenye mamlaka, suala zima hili la
Katiba, linahitaji kuzingatia maoni ya wananchi, wasingetakiwa kukubali
kufanya jambo ambalo kesho au kesho kutwa watabebeshwa lawama kuwa
walifanya uamuzi usio sahihi kwa ustawi wa taifa.
Kurudia kura ni jambo ambalo halijawahi kutokea
nchini, lakini lilitokea katika upigaji kura wa rasimu ya Katiba
inayoitwa kuwa ya wananchi.
Wale wenye mamlaka wanaweza kusema watakavyo, lakini waelewe jambo hili limeacha nyuma maswali mengi.
Chapisha Maoni