HOME
Matumaini ya uraia pacha kwa Watanzania waishio nje ya nchi yamepotea, baada ya Bunge la Katiba kupendekeza wapewe hadhi badala ya uraia.
Bunge la maalum la katiba lilivyozika hoja ya uraia pacha
Matumaini ya uraia pacha kwa Watanzania waishio nje ya nchi yamepotea, baada ya Bunge la Katiba kupendekeza wapewe hadhi badala ya uraia.
Kamati nane za Bunge hilo zimependekeza Ibara hiyo
ya 59 ibaki kama ilivyo katika Rasimu ya Katiba na kamati nne
zimependekeza marekebisho yanayolenga kuboresha maudhui yaliyomo ndani
yake.
Kamati nne hizo zinapendekeza uraia pacha na hivyo
kutoa fursa kwa raia wa Jamhuri ya Muungano aliyepata uraia wa nchi
nyingine kuendelea kubaki na uraia wa Jamhuri ya Muungano.
Aidha, Kamati moja imependekeza kuongeza Ibara
mpya itakayoipa Bunge mamlaka ya kutunga sheria itakayosimamia masuala
yanayohusu Sura hii ya Tano.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi ya Bunge la
Katiba, AndrewChenge anasema baada ya kamati yake kuyatafakari
mapendekezo ya Kamati pamoja na maoni ya wajumbe katika mijadala ya
Bunge Maalumu, inapendekeza marekebisho madogo kwenye Ibara hii kwa
kuongeza neno maalumu mbele ya neno ‘hadhi’ ili lisomeke hadhi maalum.
Anasema mapendekezo hayo yanatokana na ukweli
kwamba ibara hiyo kama ilivyo kwenye Rasimu ya Tume, inaweka msingi wa
kuwapa hadhi maalumu kwa sheria itakayotungwa na Bunge, watu wenye asili
au nasaba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambao wameacha kuwa raia
wa Jamhuri ya Muungano.
“Utaratibu wa kisheria unaopendekezwa hapa
unatumika sehemu nyingine duniani kwa mafanikio makubwa na unatoa fursa
mbalimbali kwa watu hao bila ya kupewa uraia pacha,” anasema.
Kwa mantiki hiyo, fursa mbalimbali zinazofikiriwa
kuwa zitapatikana kwa kuwepo kwa uraia pacha zinaweza pia kupatikana
bila ya kuwepo kwa uraia pacha kwa misingi iliyowekwa katika ibara hiyo.
Uraia pacha ni miongoni mwa mambo ambayo yalileta
mjadala mkubwa katika majadiliano yaliyoanzia kwenye kamati za Bunge
Maalumu la Katiba.
Majadiliano hayo yanaonekana kuwagawa wajumbe wa
Bunge hilo ambapo wengine wanatetea uwepo wa aina hiyo ya uraia huku
wengine wakiupinga.
Hata hivyo, wajumbe wengi wa upande wa Zanzibar
ndiyo wamekuwa mstari wa mbele kuupinga uraia huo kwa kuhofia kurudi kwa
Wanzibari waliokimbia nchi wakati wa mapinduzi. Kutokana na ugumu wa
jambo hilo Kamati ya uongozi wa Bunge iliunda kamati ndogo ya wajumbe 10
ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samia Suluhu kulishauri
Bunge.
Hata hivyo, kamati hiyo ambayo ilipewa jukumu la
kuyafanyia kazi mambo manne likiwamo hilo, haikuweza kuondoa mgawanyiko
huo ambao ulianzia kwenye kamati.
Akichangia katika mjadala wa ripoti zilizowasilishwa na kamati,
Profesa David Mwakyusya anasema anafahamu kuwa uraia pacha unaonekana
kupingwa na watu wa Zanzibar kwa sababu uliwajeruhi.
Anasema wanaona kuwa watu waliokimbia Zanzibar ambao wengine wako nchini Oman wataleta shida iwapo utaruhusiwa.
“Lakini ni faida kwetu kwa kuwa tunajua kuwa ni
hatari kwa usalama hivyo sheria tunazotunga zinaweza kuwabana. Nadhani
kuwa ni kitu (uraia pacha) kizuri,” alisema.
Anasema kwa waliobahatika kwenda katika hospitali
za nchi za Canada na Marekani, watakuwa wamekutana na madaktari wengi
kutoka India.
Hata hivyo, anasema miaka 1990, madaktari hao waliamua kurudi kwao na ndiyo maana hata leo Watanzania wakienda huko wanawakuta.
Anasema madaktari hao walichota utaalamu katika nchi hizo na kurejea nchi kwao ambapo wamekuwa wakiutumia.
Dk Ave-Maria Semakafu anasema vijana wanaokwenda nje ya nchi kwa ajili ya kutafuta ajira, wasiambiwe kuwa hawana uzalendo.
“Je, tunataka vijana wetu wabaki hapa wawe vibaka?
Lakini unakuta hao vijana wanapotoka na kwenda huko nje ya nchi wao
ndiyo wanaohudumia familia zao. Siyo kwamba wamejisahau, wao wanaendelea
kuwa wazalendo wanazihudumia familia zao,” anasema.
Anasema wanapoongelea kuhusu haki ya vijana waliokwenda nje ya nchi hawaongelei wale ambao wamekwenda kwa ajili ya uhalifu.
Anaomba haki maalumu kwa ajili ya watoto hao ambao
wanakwenda nje ya nchi kutafuta nafuu ya maisha na kupunguza mzigo kwa
serikali.
Naye Dk Zainabu Gama anawashambulia wale wanaotaka
Katiba iwaruhusu watu kwenda kuweka fedha nje ya nchi lakini wanakataa
suala la uraia pacha.
“Kwa nini kama nchi hii anaipenda asiweke fedha
ndani? Aende akaweke nje ya nchi. Kama mnakubali kuweka fedha nje ya
nchi kwa sababu ya biashara basi mkubali na uraia pacha,” anasema.
Anasema suala la vijana kwenda nje ya nchi linatokana na kukosekana kwa utaalamu mwingine nchini.
Hata hivyo, anasema wengine hupata kazi katika
nchi hizo wanapokwenda kusoma lakini kwa masharti wawe raia. “Usimwone
huyu msaliti. Kama huyu ni msaliti na huyu anayeweka fedha nje ya nchi
naye ni msaliti,” anasema Dk. Zainabu na kuomba uraia pacha kutambuliwa.
Kwa upande wake, Ezekiah Olouch, anasema kama
uraia pacha ukikubalika karibu robo tatu ya wakazi wa Rorya watakuwa ni
raia wa Kenya.
“Kule Kenya wamekubali uraia wa nchi mbili, sasa
hii itafanya tuwe na wabunge humu ndani wenye uraia wa Kenya na
Tanzania, tuachane na hii biashara kabisa,” anasema.
Anasema yeye amekaa nchini Uingereza na anafahamu madhara wanayoyapata Watanzania wanaoishi nje ya nchi lakini…
Anahoji ni nani ambaye anazuiwa kuleta fedha kwa
ajili ya uwekezaji nchini,” Kwani nani anazuia kumletea fedha mama yako
akafanya uwekezaji? Hiyo si mali yako? Tusiikubali kabisa biashara hii.”
“Tusiuze nchi kwa 800 bilioni ambazo tutapata kwa
watu wa diaspora (wanaoishi nje ya nchi), hapana. Tufike mahali
tuwaambie watu hili haliwezekani,” anasema na kuongeza hata kitabu cha
Biblia kimekataza suala la uraia wa nchi mbili.
Kwa upande wake, Deogratias Ntukamazina alisema nchi ambazo zimekubali uraia pacha zimenufaika na jambo hilo.
Anatoa mfano wa Kigali nchini Rwanda ambapo
majengo mengi yamejengwa na watu wanaoishi nje ya nchi baada ya
kuruhusiwa uraia wa nchi mbili.
Jasimin Aloo anasema hakuna maana kudai uraia pacha kwa sababu unataka kuleta fedha nchini.
“Suala la uraia pacha linalenga katika
kuwadhalilisha Watanzania walio wengi, ni asilimia tano ya Watanzania
ndiyo wanaodai uraia pacha na hasa ambao wanataka kujilimbikizia mali
huku na kule,” anasema. Wengine waliomunga mkono Jasmin kwa kupinga
uraia pacha ni Mohamed Seif Khatibu, Teddy Malulu, Dk Charles Tizeba na
Gaudensia Kabaka.
Dk Tizeba anasema kuruhusu uraia pacha ni sawa na
kuonja sumu ambayo inaua nchi na kutaka wajumbe kuachana na jambo hilo
kwa sababu nchi bado ni changa.
“Tunapozungumzia habari ya uraia pacha ni sawa na kuiningininiza nchi yetu katika moto,” anasema Khatibu.
Naye Gaudensia anasema suala la uraia pacha ni mapema mno na kwamba katika kipindi hiki linatakiwa kuliache kwanza.
Chapisha Maoni