HOME
Utaratibu batili hauwezi kutupa kitu halali
Tunaposherehekea ushindi katika hali ya kushindwa: Tafakari
Utaratibu batili hauwezi kutupa kitu halali
Tuna Katiba inayopendekezwa na itakabidhiwa kwa
Rais kwenye tarehe 8 Oktoba na ninasikia kutakuwa na karamu kubwa
itakayo ambatana na wajumbe kupewa tuzo ya vyeti kama sehemu ya kutambua
mchango wao mkubwa na wa kifani katika historia ya Taifa letu. Tangu
Bunge Maalumu liipitishe Katiba inayopendekezwa nimeendelea kutafakuri
kwa kina kwamba tumefikia wapi kama Taifa na kama tuna utashi, utume,
dhamira ya kweli na safi, hamasa, ari na nguvu ya kutofautisha batili na
halali. Ninaposema batili nisieleweke vibaya, ninamaanisha jumla yote
ya kufanikisha ubaya hata kama kuna pahala kilifanyika kitu halali,
ilimradi dhamira ilikuwa ubaya kwa njia yoyote kwa hakika batili hubaki
batili.
Uongozi wa mchakato wakati wa Tume
Hivi ni nani asiyejua kwamba mchakato huu
umehodhiwa kwa kiasi kikubwa na vyama vya siasa? Wengi wenu mnaweza
kujiuliza kwa nini hili limeonekana zaidi wakati wa Bunge Maalumu ilhali
vyama viliendelea kuwavuruga watu tangu mwanzo wa mchakato? Jibu lake
ni jepesi, nilitoe jibu kwa msemo cha “kila zama huja na kitabu chake”
na mimi niboreshe msemo kwa kusema “kila zama huja na uongozi wake”.
Zama zile za awamu ya kwanza na awamu ya pili za mchakato wa Katiba
Mpya, Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilitoa uongozi thabiti kuhakikisha
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Sura ya 83 inafuatwa. Tume ilihakikisha
wananchi wanatoa maoni yao kwa uhuru, kwa kujiamini na tena bila
mashinikizo. Tume iliwakemea wote waliojaribu kuingilia uhuru wa watoa
maoni (wananchi) kwa maana ya kuwaelekeza tena kwa kuwatisha wananchi
nini cha kusema watoapo maoni yao.
Nakumbuka mashinikizo yaliyokuwepo awamu ya kwanza
hasa kutoka taasisi za dini hasa upande wa Tanzania Bara na mashinikizo
ya vyama vya siasa hasa kutoka Tanzania Zanzibar. Awamu ya pili ilikuwa
vyama na hasa wale walifanya zaidi wanajikumbuka hata leo. Wananchi
tuliochukua maoni yao katika mabaraza walikiri kwetu kwamba walitishwa
na kwamba walichosema hakikuwa chao na wakatusihi tuandike kilicho bora
kwa Taifa letu.
Tulisimama imara, tuliwasaidia wananchi kuelewa na
walipo hitaji ufafanuzi, tuliwafafanulia dhana mbalimbali zilizomo
kwenye Katiba ya sasa ya mwaka 1977. Tulichukua maoni yao kwa uadilifu
na uzalendo, kwa weledi na ustadi mkubwa, kwa maneno mengine hakuna mtoa
maoni ambaye maoni yake yalipotea au kusahauliwa njiani. Tulichukua
sauti za watoa maoni, tulichukua video ya kila mtoa maoni, tuliandika
maoni yao kwa mkono kama wajumbe na watendaji wa Tume, lakini pia
kulikuwa na mtambo wa hansard ambao ulikuwa ukichukua neno kwa neno kwa
kila mtoa maoni. Najua hapa nazungumzia historia, yote haya sasa ni
historia, imepita, imekwisha, kwa baadhi ya watu haina tija wala maana
tena, kwangu mimi ni kumbukumbu ya moyoni, nikikaa kutafakuri mara kwa
mara, ninawaona wananchi wale, ninawaona wakitoa maoni, wengine
wakiuliza maswali na tukijitahidi kutoa ufafanuzi na majibu kila
tulipoweza.
Nakumbuka siku moja tulikuwa Wilaya ya Ulanga
katika mojawapo ya kata zake za pembezoni na milimani kabisa. Mwananchi
mtoa maoni alikuwa na ghadhabu kubwa alipokuwa akitoa maoni, na mimi
nilikuwa nikiendesha kikao, akasema kwa hali ilivyo inaonekana nchi ni
kubwa na imetushinda kuiongoza na kuwahudumia watu wake na akatoa maoni
kwamba bora nchi ya Tanzania tuigawe mara tatu, ili tuwe na nchi moja
kusini, ya pili kati na ya tatu kaskazini. Nikajaribu kumweleza tuna
nchi moja inaitwa Tanzania na kwamba kuigawa nchi ni kwenda kinyume na
sheria na kwamba bado anaweza akapendekeza nini kifanyike ili kuondoa
kero alizoziona. Mwananchi yule kwa hasira alinijibu “bwana mdogo
nisikilize ninachosema na hayo ndiyo maoni yangu” akamaliza.
Nilijifunza ustahimilivu, unyeyekevu, kusikiliza
zaidi na kusema kidogo. Ninasema haya kuonesha kwamba kulikuwa na
uongozi ambao si tu ulipewa uhalali wa kisheria lakini tulikuwa na
uongozi kwa maana ya utashi. Kama mjuavyo utashi haufungwi na sheria, ni
uamuzi wa kiongozi, na leo sioni haya kusema nimejifunza kutoka kwa
wajumbe wale 32 wenye utalaamu na uwezo katika maeneo mbalimbali
wakiwemo na timu ya uongozi ikiongozwa na Mwenyekiti wa Tume, Jaji
Warioba, Makamu wa Mwenyekiti Jaji Mkuu Mstaafu Agostino Ramadhani, Dk
Salim Ahmed Salim na Mzee Joseph Butiku. Ari ya kujifunza ilikuwepo
tangu mwanzo “aliponiasa kwenda kujifunza, nikaielewe vizuri nchi yangu
na kwamba ilikuwa fursa kubwa kwangu”, nilikubaliana naye asilimia zote
na kwa hakika katika hili la Katiba nitasimamia ukweli wakati wote.
Tulipoanza kukosa uongozi katika mchakato
Baada ya rai za mara kadhaa kutoka kwa Mkuu wa
Nchi, kutoka kwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na wananchi
mbalimbali kugonga ukuta, Bunge Maalumu lilianza pasina kuwa na uelewa
wa pamoja juu ya misingi, bila kufanya muafaka na kufikia maridhiano.
Ile nafasi ya vyama vya siasa ambayo katika michakato yote ya Katiba
huwa ambayo ni uwakilishi makini, nidhamu, kufanya mwafaka na maridhiano
ikageuka kuwa mtanange kati ya makundi ya walio wengi dhidi ya walio
wachache ndani Bunge Maalumu.
Nikiri uwepo wa mtanange ndani ya Bunge Maalumu
haingekuwa tatizo kama Bunge Maalumu na uongozi wake wangeonyesha
uongozi. Lakini ninaenda mbali zaidi katika tafakuri yangu kwamba kila
kitu kilipangwa kutokea kilivyo tokea. Matusi, lugha za kejeli, vijembe,
dhihaka na mara kadhaa wajumbe kutaka kutwangana makonde ndani ya
ukumbi wetu wa Bunge na Bunge Maalumu vilikuwa vitendo ambavyo
nashawishika kusema vilipangwa kisanyansi kabisa kufikia lengo fulani
tarajiwa.
Nakumbuka wajumbe wa Bunge Maalumu wakitumia
nafasi zao kuhalalisha kubadili na kuondoa maoni ya wananchi,
nikajiuliza hivi Bunge Maalumu lilitoa kazi kwa wajumbe ambao ni wabunge
kukusanya maoni kwa mara ya pili katika majimbo yao? Maana hata wakati
wa kura walipiga kura wakiwawakilisha wananchi katika majimbo yao ya
uchaguzi na hata baadhi ya wale wajumbe wa 201 na wao wakapiga kura ya
ndiyo huku wakijinasibu na makundi yaliyowapendekeza.
Vitendo vya baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu ambao ni wabunge
wa Bunge la Muungano na baadhi ya wajumbe kutoka kundi la 201 ambao
walipiga kura ya ndiyo kwa mbwembwe na kwa sauti kubwa “ndiyoooo” tena
kwa vifungu vyote wanifanya nijiulize swali la kimaadili kwa Kiingereza
“a moral question”. Bunge Maalumu ni Mkutano Mkuu wa Taifa, wajumbe wake
wanawakilisha Taifa na si kitu kingine, fikra zao ni Taifa kwanza,
Taifa kwanza na Taifa kwanza.
Swali la kimaadili nauliza, kama wajumbe walikuwa
wako pale kama wawakilishi wenye hadhi sawa wakiliwakilisha Taifa,
uhalali wa kutumia wananchi kutoka majimboni kubariki uamuzi hasa wa
walio wengi waliupata wapi?
Kama walipaswa kulitizama Taifa na kutenda kama
wawakilishi wa taifa kwanini walijishusha mpaka katika makundi yao na
majimbo yao ya uwakilishi? Tume ilikwenda kwenye kila wilaya na majimbo
nchi nzima na tulionana na wananchi wale wale iweje leo watoe maoni
tofauti na yale tuliyasikia? Naendelea kujiuliza, nani msaliti, ni
wananchi au ni ndugu zangu? Ambao kuanzia wiki hii nitaanza kuwatambua
kama “waliokuwa wajumbe wa lililokuwa Bunge Maalumu lililopaswa kuweka
Maslahi ya Wananchi mbele na hawakufanya hivyo”.
Nini matokeo ya kupuuza wananchi
Wananchi walisema mbunge asiwe waziri, Wananchi
waweze kumwajibisha mbunge, uwepo ukomo wa muda wa mtu kuwa mbunge, Rais
apunguziwe madaraka na awekewe vyombo vya kikatiba kumshauri, wakuu wa
mikoa na wilaya watizamwe upya, uhusiano na uratibu wa mambo yasiyo ya
Muungano kati ya Bara na Zanzibar uwekwe kikatiba, Wananchi wanataka
maadili na miiko iwekwe kikatiba na kuimarishwa, Wananchi wanasema Tunu
ziwepo ili sisi kama Taifa na Jamii ya Tanzania tuzienzi na kuziishi na
kadharika “waliokuwa wajumbe wa lililokuwa Bunge Malumu lililopaswa
kuweka masilahi ya wananchi mbele na hawakufanya hivyo” wamepuuza na
kufutilia mbali.
Najiuliza tunasherehekea kipi? Kufanikiwa
kuwapuuza wananchi? Kama tungeulizwa tuchague hii leo ni nani tungependa
kumtumikia kweli kweli, naamini wachache mno wangechagua wananchi wa
Tanzania na wengi mno wangechagua “majitu” yale yatishayo, yapumuayo
katika pua zao moshi na moto pamoja na makundi ambayo ni kana kwamba
yameshikilia mustakabali wao wa sasa na wa baadaye. Nikiwatizama watu
hawa najiuliza, nafasi ya Watanzania mioyoni mwao hata kabla sijajiuliza
nafasi ya Mwenyezi Mungu wanaye amini anawapa pumzi na vyote dhidi ya
masilahi yao binafsi na makundi yao.
Tuchukulie waraka huu kama, ujumbe kutoka kwa mtu
asiye na uzoefu wa namna tunatenda na kuenenda katika siasa dhidi ya
uhalisia wa maisha yetu ya leo na kesho.
Itaendelea wiki ijayo
Chapisha Maoni