HOME
Treni Dar kwa kadi, kila baada ya nusu saa
SERIKALI imetia saini mkataba wa
uwekezaji wa pamoja kati yake na kampuni ya Marekani kwa ajili ya kuanza
mradi wa usafiri wa treni ya kisasa itakayoanzia Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa Julius Nyerere (JNIA) hadi katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison
Mwakyembe amesisitiza ni lazima kufanya haraka kwani mwekezaji, Kampuni
ya Ms Shimoja ya Marekani, iko tayari hata sasa kuleta treni hizo aina
ya Diesel Multiple Unit (DMU) ambazo ni za kisasa, itakayopita kila
baada ya nusu saa.
Usafiri huo wa treni kwenye njia ya
umbali wa kilometa 13 kutoka uwanja wa ndege hadi katikati ya jiji,
unatarajiwa kukamilika Desemba mwaka huu au mapema mwakani ukilenga
kubeba abiria kati ya 800 na 1,000.
Katika hafla ya kutia saini kati ya
mwekezaji huyo na Shirika la Reli Tanzania (TRL) jana jijini Dar es
Salaam, Waziri Mwakyembe aliwaambia watendaji kwamba ikiwa watafanya
haraka, baada ya wiki mbili watasaini makubaliano ya mwisho na kuanza
urekebishaji na ujenzi wa vituo sita vya kupandia treni kwa kadi.
Mkurugenzi wa Kampuni hiyo ya Ms
Shimoja, Dk Robert Shumake na Mkurugenzi Mtendaji wa TRL, Kipallo
Kisamfu walitia saini jana katika hafla iliyoshuhudiwa na Waziri
Mwakyembe na Katibu Mkuu wake, Dk Shaaban Mwinjaka.
Waziri Mwakyembe alimshukuru Rais Jakaya
Kikwete kwa kusafisha njia ya kupata wawekezaji, akiwemo mfanyabiashara
huyo mkubwa ambaye ametajwa kuwa na imani kuwekeza katika mradi huo
utakaogharimu zaidi ya dola za Marekani milioni 35.
Kwa mujibu wa waziri, waliamua kuanza
mradi huo baada ya kuhamasisha mashirika makubwa ya ndege kufanya safari
katika kiwanja hicho cha ndege. Hata hivyo, alisema wasafiri wanapata
kero ya usafiri kufika katikati ya jiji jambo wanalotegemea mradi
kuondoa kero hiyo.
“Mabehewa hayo yataunganishwa kulingana
na idadi ya abiria waliopo na muda, huku mwekezaji akiwekeza bila
masharti kama walivyo wengine; kama vile kutaka dhamana ya serikali,”
alisema Mwakyembe.
Hata hivyo alisisitiza, “lakini ni lazima watendaji waache ukiritimba kwa kufanya utaratibu haraka ili kazi zianze.”
Alisema katika utaratibu wa PPP,
uwekezaji na idara nyingine lazima wafanye haraka. Aidha alitaka
watendaji TRL kumsihi mfanyabiashara huyo kuleta treni nyingine mbili za
Ubungo mpaka Stesheni na kwingineko.
Treni hiyo itasaidia kupunguza adha kwa
abiria wanaosafiri kwa ndege, ambapo katika kituo cha Karakata,
itajengwa njia ndogo ya treni mpaka barabarani. Pia litajengwa daraja
kwa ajili ya wasafiri kuvuka na mizigo yao.
Akizungumza katika hafla hiyo ya utiaji
saini, Mkurugenzi Mtendaji wa TRL, Kisamfu alisema watafanya kazi usiku
na mchana kuhakikisha usafiri huo unaanza mapema iwezekanvyo kutoka
katikati ya jiji hadi Pugu kupitia maeneo ya Karakata, kwenye Uwanja wa
Ndege kwa kutumia Reli ya Kati.
Mwekezaji Dk Shumake ambaye ni Balozi wa
Heshima Tanzania nchini Marekani, alisema wako tayari kuanza mradi huo
hata leo kama utaratibu utakamilika.
Alisisitiza kwamba uwekezaji huo
utaondoa tatizo la foleni barabarani kutoka uwanja huo wa kimataifa wa
ndege hadi katikati ya jiji.
Chapisha Maoni