Unknown Unknown Author
Title:
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
HOME Bunge limemaliza kazi, sasa ni wananchi kuamua katiba mpya Hatimaye Bunge Maalum la Katiba limekamilisha kaz...
HOME

Bunge limemaliza kazi, sasa ni wananchi kuamua katiba mpya


Hatimaye Bunge Maalum la Katiba limekamilisha kazi yake ya kuandaa katiba inayopendekezwa na kubakiza kazi ndogo tu ya kuikabidhi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kabla ya kupelekwa kwa wananchi ili waipigie kura.

Hatua hiyo ya aina yake katika historia ya Tanzania ilifikiwa jana mjini Dodoma baada ya wajumbe wengi waliokuwa wakiunda Bunge hilo kupiga kura ya "ndiyo" dhidi ya katiba hiyo iliyoanzia kwenye mchakato wa kukusanya maoni ya wananchi uliosimamiwa na Tume Maalum ya Mabadiliko ya Katioba kabla ya kufikia ilipo sasa.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, hatua iliyofikiwa sasa inatokana na idadi kubwa ya wajumbe kupiga kura ya ndiyo iliyofikia idadi inayotakiwa kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba; ambayo inataka katiba inayopendekezwa kuungwa mkono na wajumbe wanaofikia walau theluthi mbili ya wajumbe wote wa Tanzania Bara na pia wa idadi kama hiyo kutoka Zanzibar.

Jumla ya wajumbe wote waliokuwa wakiunda Bunge hilo ni 629; wakiwa katika mgawanyo wa wajumbe 419 wa Bara na 210 wa Zanzibar. Katika upigaji wa kura hizo, wajumbe wa Zanzibar walipiga kura za ndiyo kati ya 147 na 148 huku kwa upande wa Bara ambako zilihitajika kura 274 ili kufikia yheluthi mbili, kura za ndiyo zilizopatikana zilikuwa ni kati ya 331 na 334.

Sisi tunapongeza hatua iliyoifikiwa jana na wajumbe, hasa kwa kutambua kuwa zoezi hilo muhimu kwa mustakabali wa taifa halikuwa rahisi. Mabishano ya hoja miongoni mwa wajumbe watokao katika makundi tofauti ya jamii yalikuwa makali na baadhi ya wajumbe walisusia vikao hivyo wakipinga kile walichosema kuwa ni kubadilishwa kwa maoni ya wananchi yaliyokusanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Mstaafu Joseph Warioba. Hata hivyo, hatimaye upigaji kura wa wajumbe hao ulianza rasmi Septemba 29 na kuhitimishwa jana, Oktoba 2.

NIPASHE tunatambua kuwa kwa mujibu wa ratiba, kukamilishwa kwa katiba hiyo iliyopendekezwa kutatoa fursa ya kuendelea kwa hatua inayofuata ambayo ni ile ya kupigiwa kura ya ndiyo au hapana na Watanzania wote wenye sifa zilizoainishwa kwenye Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Na kwamba, zoezi hilo la upigaji wa kura utakaohusisha pande zote za Muungano utafanyika baada ya kukamilka kwa Uchaguzi Mkuu wa 2015 na hivyo, kwa kiasi kikubwa utaendelezwa na rais ajaye wa Tanzania atakayekuwa wa tano tangu kupatikana kwa uhuru mwaka 1961.

Ni kwa kujua hilo, ndipo tunapoona kuwa sasa ni wakati muafaka wa kuachia uamuzi wa katiba hiyo iliyopendekezwa mikononi mwa wananchi. Ni wao pekee ndiyo wenye nafasi kubwa ya kuamua kuwa katiba hiyo iliyopendekezwa ipitishwe baada ya kuipigia kura nyingi za ndiyo ama kinyume chake.

Hakika, uamuzi kuhusu katiba mpya siyo lelemama. Ni zoezi linaloambatana na changamoto nyingi zitokanazo na kuwapo kwa mawazo tofauti yanayotakiwa kuwa na lengo moja kama ilivyojidhihirisha wakati wa mchakato wa kukusanywa kwa maoni kulikofanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Mstaafu Joseph Warioba na baadaye Bunge Maalum la Katiba lililokamilisha kazi yake jana Kwa sababu hiyo, ili kujipeusha na migongano inayoepukika wakati wa upigaji kura, ni vyma wananchi wote wakapewa nafasi ya kupitia katiba hiyo iliyopendekezwa kuanzia sura ya kwanza hadi ya mwisho.

Kwa kufanya hivyo, ni wazi kwamba wengi watajua ni kitu gani kilichomo na mwishowe kuwa katika nafasi nzuri ya kutekeleza wajibu wao wakati wa kupiga kura ya kukubali au kukataa katiba hiyo.

NIPASHE tunaamini kuwa jambo hili ni muhimu kuzingatiwa pindi wakati wake utakapowadia kwani kinyume chake, ikiwa wananchi hawatakuwa na ufahamu kuhusiana na katiba

hii inayopendekezwa, ni wazi kwamba maamuzi watakayofanya hayatotakana na wao wenyewe bali ushawishi wa wachache watakaopata fursa hiyo. Na hilo siyo jambo zuri. Halipaswi kuachwa litwae nafasi kubwa wakati wa upigaji wa kura za wananchi.

Na kwa sababu hiyo, tunasistiza kwamba ni vyema wananchi wakaelimishwa; wakajieleimisha na mwishowe kuachwa wafanye uamuzi wao wakati upigaji  kura utakapowadia. 

About Author

Advertisement

Chapisha Maoni

 
Top