Unknown Unknown Author
Title:
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
HOME UTAFITI : Ebola inaenea haraka zaidi kwa wanawake kuliko wanaume   Wanawake nchini Liberia wakisali...
HOME

UTAFITI : Ebola inaenea haraka zaidi kwa wanawake kuliko wanaume

 
Wanawake nchini Liberia wakisali ili kumuomba Mungu awaondolee balaa la ugonjwa wa Ebola 


Ingawa binadamu wote ni sawa, lakini ni jambo la kushangaza kuona kuwa wakati wa mlipuko wa ugonjwa fulani, jinsi moja inaathirika zaidi kuliko nyingine.
Takwimu zinaonyesha kuwa hadi katikati ya wiki hii watu zaidi ya 3,000 walikuwa wamekufa kwa ugonjwa huu unaoenea kwa kasi katika nchi tatu za Afrika Magharibi, Sierra Leone, Guinea na Liberia.
Nyingine ni Senegal iliyopata mgonjwa wake wa kwanza Agosti 29 mwaka huu, DRC na Nigeria ambayo hadi sasa imekwisha pata wagonjwa zaidi ya 20 na vifo saba.
Ebola ni ugonjwa hatari unaosambaa haraka kwa kugusana na majimaji yatokayo katika mwili wa mtu au mnyama mwenye maambukizi ya virusi wa ugonjwa huu.
Hadi sasa kuna aina tano za virusi vya ebola ambavyo ni Zaire ebolavirus, Reston ebolavirus, Sudan ebolavirus, Tai ebolavirus na Bundibugyo ebolavirus.
Bundibugyo ni aina mpya ya virusi vya ebola vilivyogunduliwa huko Uganda mwaka 2007. Katika mlipuko wake wa kwanza, watu wapatao 400 waliambukizwa virusi vya ebola na takriban asilimia 90 ya watu hao walipoteza maisha.
Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) hadi kufikia sasa inakadiriwa kuwa kiasi cha watu 3,685 wameshaugua ugonjwa huu tangu ulipogunduliwa na kati ya hao asilimia 67 wamepoteza maisha.
Ugonjwa wa ebola unaendelea kusambaa kwa kasi barani Afrika na kusababisha hofu kubwa kwa dunia nzima. Kuna wasiwasi kwamba ugonjwa huo unaweza ukaiangamiza dunia iwapo hatua madhubuti hazitachukuliwa. Kutokana na hali hiyo WHO imeutangaza ugonjwa huu kuwa ni janga la dunia.
Kwa mujibu wa Profesa Andrew Easton wa Chuo Kikuu cha Warwick, virusi vinavyosababisha ugonjwa wa ebola vilionekana kwa mara ya kwanza kwa binadamu mwaka 1976 katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Inadhaniwa kuwa ugonjwa huu umetokana na mwingiliano kati ya wanyamapori na binadamu hasa wanaume wanaowinda na kuchuna nyama za wanyama wenye virusi vya ebola.
Huko Ufilipino Januari mwaka 2009, serikali ya nchi hiyo ilitangaza kuwa watu wanne walikutwa na maambukizi ya virusi vya ebola aina ya Reston ebolavirus ambavyo waliambukizwa kutoka kwa nguruwe.
Ingawa wanaume wanaonekana kuwa katika hatari kubwa ya maambukizi kutokana na majukumu yao ya kutafuta kitoweo cha familia, lakini hali halisi na takwimu mbalimbali zinaonyesha kuwa wanawake ndio wanao ambukizwa kwa kasi zaidi.
Hali hiyo inaonyesha kuwa hata waliofariki, wanawake ni wengi zaidi kuliko wanaume.
Kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa kwenye gazeti la Washington Post la Agost 14 mwaka huu, asilimia 55 hadi 60 ya waathirika wa ebola katika nchi za Guinea, Sierra Leone na Liberia ni wanawake.
Taarifa zilizotolewa na maofisa wa Wizara ya Afya ya Liberia zinasema kwamba asilimia 75 ya watu waliokufa kwa ugonjwa wa ebola nchini humo ni wanawake.
Ripoti ya WHO ya mwaka 2007 pia inaonyesha kuwa, wakati wa mlipuko wa ugonjwa wa ebola wa mwaka 1979 huko Sudan, asilimia 69 ya wahanga wa ebola walikuwa wanawake.
Takwimu nyingine zinaongeza kueleza kuwa wakati wa mlipuko wa ebola katika miaka ya 2000 na 2001 huko Gulu nchini Uganda, pia idadi ya wanawake walioathiriwa na ebola ilikuwa kubwa zaidi ya idadi ya wanaume.
Waziri wa Jinsia na Maendeleo wa Serikali ya Liberia, Julia Duncan-Cassell anasema kuwa pamoja na sababu nyingine, wanawake wengi wanapata maambukizi ya ugonjwa huu kutokana na majukumu yao ya kijinsia katika jamii.
Naye mke wa rais wa Sierra Leone, Sia Nyama Koroma anasema kuwa wanawake ndiyo wengi katika sekta ya huduma za afya, hivyo wengi hupata maambukizi wakati wa kutekeleza majukumu yao ya kuuguza na kuhudumia wagonjwa hospitalini na nyumbani.
“Wanawake ndiyo wanaowaogesha wagonjwa na kufua nguo zao na mara nyingi hufanya hivyo bila kuvaa vifaa vya kuwakinga,” anasema.
Dk Pritish Tosh wa kliniki ya moyo ya Marekani, akielezea kinachowafanya wanawake waambukizwe kwa wingi zaidi Afrika Magharibi, alisema:
“Wanawake ndiyo wanaotunza wagonjwa, hivyo wana uwezekano mkubwa wa kugusana na matapishi au vinyesi vya wagonjwa katika familia zao, jambo ambalo huwaweka katika hatari kubwa ya maambukizi.”
Ripoti ya Caroline Kiarie na Masa Amir wa taasisi ya kukabili matatizo ya dharura Kiafya ya Afrika, Urgent Action Fund-Africa inasema:
“Wanawake wengi hupata maambukizi ya magonjwa kutokana na hali duni ya kipato. Wengi hufanya kazi zisizowawezesha kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya magonjwa mbalimbali ikiwa ni pamoja na ebola.”
Profesa Wafaa El-Sadr ambaye ni mtaalamu wa maswala ya epidemiolojia katika Chuo Kikuu cha Columbia, yeye anaelezea tatizo hilo akisema linatokana na unyonge wa wanawake.
“Ukichunguza ni kina nani wanaokufa zaidi katika mlipuko wa ugonjwa, utatambua ni nani wana nguvu na nani ni mnyonge.”
Hali ya namna hii, Profesa El-Sadr anaielezea kuwa inaashiria ni jinsi gani jamii inavyoishi na hata kupeana majukumu pengine kwa uonevu.
Utafiti wa Kibadi Mupapa na wenzake, uliochapishwa katika jarida la magonjwa ya kuambukiza lijulikanalo kama Infectious Diseases toleo la 179 la mwaka 1999 unaonyesha kuwa wanawake wajawazito wako kwenye hatari kubwa ya kupata ugonjwa wa Ebola na kufariki.
Katika mlipuko mmoja wa ebola huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, hatari ya vifo kwa kinamama wajawazito ilifikia asilimia 95.5 na kuzidi ile ya kawaida ya asilimia 77 katika jamii.
Wachunguzi wengine wa mambo ya huduma za afya wanadai kuwa, pamoja na kuwa na kinga ndogo ya mwili, wakati wa mlipuko wa ebola wanawake wajawazito wanapoenda kujifungua wanaweza kukabiliwa na wakati mgumu wa unyanyapaa.
Hali hii inatokana na wahudumu wa afya kuhofia maambukizi wakati wa kuwahudumia wajawazito wakati wa kujifungua. Mazingira hayo pia yanatafsiriwa kuchangia ongezeko la vifo kwa wanawake hasa wajawazito.
Carol Vlassoff wa Kitivo cha Magonjwa na Afya ya Jamii cha Chuo Kikuu cha Ottawa Canada alibainisha, kwenye utafiti wake wa mwaka 2007, kuwa majukumu ya jinsia yana uwezo mkubwa wa kusababisha tofauti za kupata magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza.
Ripoti ya WHO ya mwaka 2007 kuhusu ugonjwa wa malaria na jinsia, ilionekana kuwa wanawake ni waathirika wa magonjwa mengi na siyo ebol;a pekee.
Ni jambo la muhimu kuelewa mambo yanayochangia jinsi ya kike kuathiriwa zaidi na ebola ili hatua stahiki zichukuliwe na mikakati madhubuti kuwekwa kwa lengo la kupunguza athari za ugonjwa huu kwa wanawake na jamii kwa jumla.
Ikumbukwe kwamba katika maeneo mengi ya vijijini, ambako wazalishaji wengi wa chakula ni wanawake, ugonjwa wowote unaoathiri na kuua wanawake kwa wingi unaweza kusababisha baa la njaa na athari za uchumi wa familia na taifa.

About Author

Advertisement

Chapisha Maoni

 
Top