HOME
Shughuli za binadamu lazima zizingatie kuendeleza uhai
0
Lengo la mafunzo lilikuwa ni kuwajengea uwezo
watafiti, wafanyabiashara, wanamazingira na wachumi ili watambue mambo
ya hatari kwa uhai yanayoweza kujitokeza katika shughuli zao za kila
siku na jinsi ya kuyakabili.
Waliendesha mafunzo hayo chini ya kaulimbiu Weka
Mazingira Mazuri ya Shughuli za Makundi ya Kijamii ili Kuimarisha na
Kuendeleza Mahitaji kwa Uhai.”
Hii ni kaulimbiu ambayo inahamasisha shughuli mbalimbali ili ziendane na mipango ya mapinduzi ya kijani barani Afrika.
Haya ni mapinduzi yanayolenga kuimarisha kilimo
kupambana na njaa na wakati huohuo kuhifadhi mazingira kwa lengo la
kukabili matatizo yanayotokana na mabadiliko ya tabianchi.
Mchumi na mtafiti wa UNU-INRA, Dk Calvin Atewamba
anasema binadamu ana kila sababu ya kujutia kwa kuharibu mazingira
wakati akiendesha shughuli mbalimbali ili kupata chakula na kufanya
biashara.
Alisisitiza kuwa “shughuli zote za kijamii hapa
duniani zina matokeo chanya au hasi kwa mazingira. Kinachotakiwa
kifanyike ni jamii kuelimishwa ili kutekeleza malengo ya Afrika katika
kufikia mapinduzi ya kijani katika uchumi”.
Alitoa mfano wa shughuli zinazochangia athari za
mazingira kama vile uvunaji kupita kiasi wa raslimali za bahari,
uchafuzi wa mazingira na kuongeza athari za mabadiliko ya tabianchi.
Dk Atewamba anasema jamii kwa sasa inahitaji
kuwekewa mfumo ambao utasimamia na kutathmini shughuli mbalimbali ili
kuelekeza nini kifanyike kwa lengo la kupunguza athari za mazingira
zinazosababishwa na shughuli za binadamu.
Kufanya hivyo, Dk Atewamba anaamini, kutainua hadhi ya binadamu kwa kuboresha mazingira yanayoendeleza uhai.
Mkurugenzi wa UNU-INRA, Dk Elias Ayuk anaamini
kuwa ipo haja ya kuweka kiunganishi kati watafiti wa mazingira na jamii
kwa kuwa shughuli za kila siku za binadamu ndizo zinachangia athari za
mazingira.
Nchi zilizokuwa na uwakilishi kwenye mafunzo haya
ni Ghana, Cameroon, Nigeria, Kenya, Zimbabwe, Misri, Uganda, Malawi,
Benin, Swaziland, Tunisia na Zambia.
Tanzania haikuwa na mwakilishi kwenye mkutano huo, lakini kama
moja ya nchi za Afrika, maazimio na mikakati ya mkutano huo yanaihusu.
Ni muhimu kutambua kwamba hakuna nchi ambayo ina
kinga dhidi ya mabadiliko ya tabianchi. Kwa hiyo mataifa yote duniani
yanapaswa kushirikiana ili kufikia malengo ya kukabili mabadiliko ya
tabianchi ambayo yanaandamana na kuongezeka kwa joto duniani.
Hii ni kusema kila mtu anapaswa kuzingatia
maelekezo ya kitaalamu ili kulinda na kuendeleza uhai. Kila mtu kwa
nafasi yake ajitahidi kuifanya dunia kuwa mahali pazuri kwa ustawi wa
uhai.
Tanzania inakabiliwa na matatizo mengi ya athari
za mazingira kama vile ukataji ovyo wa misitu kwa ajili ya kupasua mbao,
kuni, mkaa na kupanua mashamba.
Isitoshe taifa linakabiliwa na tatizo kubwa la
utupaji hovyo wa mifuko ya plastiki. Wataalamu wanasema mifuko ya
plastiki ni sumu kwa viumbe hai na mimea inayoweza kudumu kwenye ardhi
kwa zaidi ya miaka 400. Hii ni hatari.
Wafugaji hapa nchini nao wamekuwa na mifugo ambayo
ni mingi kuliko maeneo ya kuchunga na matokeo yake imekuwa ikifanya
safari ndefu kutafuta malisho na kuwa chanzo cha uharibifu wa mazingira.
Yote hayo ni machache kati ya yale yanatendwa na
binadamu wa leo na kuchangia uharibifu wa mazingira unaosababisha dunia
kuwa katika hali ambayo siyo rafiki wa kuendeleza uhai.
Hali hiyo inachochea mabadiliko ya tabianchi badala ya kusaidia kupunguza athari zake.
Ardhi yetu ingekuwa na miti mingi ingeweza
kusaidia kupunguza hewa ukaa kwenye tabaka la dunia ambayo ni chanzo
kikubwa cha kuongezeka kwa joto duniani.
Athari za mazingira nchini zimesababisha misitu
kutoweka, kuenea kwa jangwa, kukauka kwa vyanzo vya maji, ukame wa muda
mrefu, kutoweka kwa mito, kupungua kwa barafu kwenye milima mirefu kama
vile Kilimanjaro na kuenea kwa magonjwa kama vile malaria, dengue na
utapiamlo.
Katika miaka ya karibuni, ukame umesababisha kupungua kwa uzalishaji wa chakula hapa nchini kutokana na kilimo kutegemea mvua.
Ili kuepusha mabalaa hayo ni wakati wa kufuata
ushauri wa UNU-INRA. Watafiti, wafanyabiashara, wanamazingira na wachumi
lazima waelimishwe namna ya kutekeleza shughuli zao kulingana na
mikakati ya kulinda mazingira yetu.
Chapisha Maoni