HOME
Tumejiandaa kisaikolojia na kura ya maoni?
Kazi ya Bunge Maalumu la Katiba imefikia kikomo,
wamefanya walilofanya, kazi iliyobaki sasa ni kwa umma kuamua kuhusu
hayo waliyopendekeza kama yamekidhi matakwa yao au la.
Hatua ya upigaji kura ya maoni ni muhimu katika nchi ya kidemokrasia, nina amini kuwa uamuzi wa wananchi utaheshimiwa.
Lakini pia mchakato wenyewe wa kura ya maoni utakuwa huru, wazi, na wenye kutimiza vigezo vinavyotakiwa.
Hatutarajii kuwapo kwa mizengwe, ulaghai,
ubabaishaji au ubabe wakati wa mchakato huo wa kura ya maoni. Watu
washindane kwa hoja na siyo ubabe wa kisiasa.
Bila shaka, ile safari yetu tuliyoanza ya kuandika
Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sasa inakaribia kufikia
ukingoni wakati wowote kama tulivyoambiwa.
Tukiwa tumo katika kumsubiri mgeni huyo atufikie
kwenye nyumba zetu, tunatakiwa kujiandaa kwa mapokezi yake na maandalizi
yenyewe ninayoyakusudia hapa ni kujiandaa kisaikolojia, hususan
wanasiasa na vyama vyao.
Sina wasiwasi na wananchi wa kawaida ambao wao
wanalotaka ni kuona maoni waliyotoa yamezingatiwa, lakini kwa wanasiasa
wanataka Katiba yenye kuwahakikishia masilahi yao katika uwanja wa
kisiasa.
Wananchi wanataka kuona masuala kama ya umasikini
yakipewa nafasi katika Katiba Mpya, kwani umasikini hauwezi kuondolewa
kwa maneno matupu.
Ukiwa na Katiba inayotokana na matakwa ya
wananchi, unaweza pia kuendelea katika nyanja za viwanda, kiteknolojia,
huku ubunifu na uvumbuzi wa wasomi na watafiti vijana katika taaluma
mbalimbali za sayansi za jamii, sayansi asilia na umbile, sayansi
tumizi, bioteknolojia na nyanja nyinginezo za sayansi na utafiti
ukishika kasi katika nchi.
Masuala kama hayo yakipewa uzito ndani ya Katiba,
tunaweza kuingia katika orodha ya nchi ambazo zinauza wataalamu kwa
mataifa mengine katika nyanja tafauti maana uchumi uwekezaji siyo lazima
tuwekeze kwenye viwanda tu, tunaweza kuwekeza kwenye taaluma.
Pia dhana ya ujana ikiwa itafanyiwa kazi katika
Katiba Mpya kwa vijana kupewa nafasi kuonyesha vipawa vyao,
wakijiegemeza katika mustakabli mpya wa nchi yenye usawa, umoja na
mshikamano na zaidi kuwa na mfumo mpya wa muundo wa Muungano, wanaweza
kututoa katika hali tuliyonayo.
Naamini safari yetu ya kuandika Katiba Mpya
iliyoanza, inaweza kutufikisha katika zama ambazo hakutakuwa na viongozi
wa maisha wala watendaji wa milele. Tutakuwa na vifungu vya sheria
vyenye kuweka ukomo wa uongozi na kila mmoja wetu kuvifuata.
Katiba ya sasa ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hata ya
Zanzibar inatoa mwanya kwa baadhi ya watu, kwa mfano waliostaafu
kuendelea kubaki katika utumishi wa umma kwa kisingizo cha “mikataba” na
hati hakuna wazoefu, ajabu hii vijana watapataje uzoefu ilhali wazee
wamekuwa ving’ang’anizi?
Hapa Zanzibar wazee ndio kwanza wanaendelea
kung’ang’ania katika nafasi ambazo wangeshika vijana wao ili wao kubaki
kama washauri, hali hii inawavunja moyo vijana.
Hatuwapingi wazee kuwamo katika kazi, lakini
tunawakumbusha kujiandaa na maisha ya kustaafu, huku wakiwatayarisha
vijana kuchukua nafasi zao sio kuendelea kuwa ving’ang’anizi katika
nafasi za utendaji huku baadhi yao wakiwafisidi vijana.
Katika kufikia malengo ya ustawi, siku za usoni
hatuwezi kutegemea tu mafanikio ya zamani ili kuweza kustawi katika
nyanja tofauti.
Leo hii leo, jamii nyingi duniani zimeathiriwa kwa
kiwango kikubwa na ustawi wa kasi wa sayansi na teknolojia pamoja na
matukio ya kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.
Kwa hivyo, nchi zote zinalazimika kuandaa mipango
yao ya siku za usoni kwa kuzingatia matukio na mahitaji ya hivi sasa
kwani, Tanzania ya leo na Zanzibar ya leo sio ya jana wala juzi ni mpya,
mahitaji mapya fikra mpya kwani idadi kubwa ya watu wake sasa ni wapya.
Ndiyo maana, mjadala wa Katiba Mpya kwa pande zote
za Muungano tumezisikia kauli zenye kutaka ikidhi matakwa ya wananchi
siyo ya wanasiasa na makundi masilahi.
Katika ulimwengu wa kisasa, uendelevu, uhai na
ustawi wa nchi unategemea vijana ambao wanaweza kufanya kazi kwa haraka
zaidi na kutumia weledi wao katika kuongeza kasi ya maendeleo katika
nyanja zote.
Ni wakati muafaka tukijiandaa kisaikolojia,
kufikiria pia kuwapo na ukomo wa umri wa mtu kuweza kugombea urais,
ubunge na uwakilishi mwisho uwe miaka 60 zaidi ya hapo apumzike, kwani
umri wa kustaafu kazi Tanzania siyo zaidi ya miaka 60, hivyo hakutakuwa
na ubaya kwa nafasi hizo zikiwekewa ukomo wa umri.
Watetezi wa uzee wanajenga hoja kwamba umri wa
miaka 35 haufai kumfanya kijana kuweza kuongoza Serikali, maana mawazo
na matendo yake bado ni ya utoto, yawezekana ikawa sahihi na inawezekana
pia siyo sahihi.
Katika hili, hawapaswi kuwahukumu vijana kwa
sababu ya haiba ya ujana wao, mnapaswa kuhukumu matendo ya kijana husika
maana uongozi na kiongozi ni vitu tafauti na hususan kazi ya urais
maana urais si mtu ni taasisi.
Falsafa ya ujana inakwenda mbali zaidi na
wanazuoni wengi wanauchukulia ujana kuwa siyo suala la umri peke yake
bali ni pamoja na ufahamu wa jambo wenye kuambatana na fikra sahihi na
pevu.
Kupata fikra mpya katika zama mpya kunahitaji mabadiliko ya
mfumo katika mataifa yetu. Ni jambo la wazi kabisa nguvu kazi ya vijana
haijatumika sawa sawa, miaka takriban hamsini wimbo ni ule ule vijana
taifa la kesho badala ya taifa la leo. Pengine upeo wa fikra pevu ndio
unaotofautisha mataifa yanayoendelea.
na yaliyoendelea.
Fikra mpya za vijana zinaweza kuwa ndio sababu na
msukumo wa mabadiliko ya kiuchumi, kijamii na kisiasa tukiwa na Katiba
mpya yenye kukubaliwa na pande zote za Muungano iliyotokana na matakwa
ya watu wenyewe.
Chapisha Maoni