HOME
Elimu isiyomkomboa Mtanzania ni mwendelezo wa utumwa
Elimu ni suala la jamii ambalo mipango na taratibu zake zinahitaji kushirikisha wadau wote katika jamii.
Madhumuni ya elimu kwa jumla ni kuifanya dunia
kuwa mahali pazuri pa kuishi watu wa vizazi vyote. Inakusudiwa kuwapa
watu maarifa na ujuzi watakaoutumia kuwasaidia kupata njia mpya na bora
zaidi ya kutatua matatizo yao.
Elimu lazima imkomboe binadamu kiakili na kimwili,
imwezeshe kujikwamua na kumpa uwezo wa kupambana na matatizo au
changamoto zinazomkabili katika maisha.
Malengo ya msingi ya elimu ni kumkomboa binadamu.
Kumkomboa maana yake ni kumweka huru kutoka hali au jambo fulani.
Inamaanisha kuwa kuna vikwazo ambavyo lazima avishinde.
Tulipopata uhuru mwaka 1961, tulisema kuwa tuna
maadui watatu: ujinga, maradhi na umaskini. Maadui hawa bado tunao hadi
leo, tena wameongezeka. Hivi ni vikwazo tunavyoweza kuvishinda tukipata
elimu sahihi.
Mwalimu Nyerere alifafanua Elimukombozi kuwa ‘ni
aina ya elimu inayomkomboa Mwafrika kutoka mawazo ya utumwa na ukoloni
na kumfanya ajihisi kuwa binadamu sawa na binadamu wengine, mwenye haki
na wajibu wa kibinadamu.
Elimu inayomkomboa kutoka tabia za kukubali
mazingira yanayomnyanyasa na kupunguza utu wake na hadhi yake kana
kwamba hayabadilishiki na hana uwezo juu ya mazingira hayo.
Pia lazima imkomboe kutoka minyororo ya ujinga wa
teknolojia ili aweze kutumia vifaa vya kujiweka sawa ili kujiendeleza
yeye na binadamu wenzake.
Dhana hii ya elimukombozi hapa imetumika
kumaanisha elimu inayomwezesha binadamu kujitambua, kujikomboa na
kushiriki katika kuikomboa jamii yake.
Katika muktadha wa Afrika na Tanzania, ni elimu
inayomtoa Mwafrika kutoka mawazo ya kitumwa tuliyopandikiziwa na elimu
tuliyoirithi kutoka kwa wakoloni na ambayo mengi tumeyaendeleza hata
baada ya Afrika yote kuwa na uhuru wa bendera.
Elimu yetu hivi sasa haina sifa tulizotaja za
elimukombozi. Elimu ya sasa ni elimu tuliyoirithi kutoka kwa wakoloni.
Sote tumeathirika kwa kiasi kikubwa na elimu hii.
Malengo yake yalikuwa kutubadili ili tuwe
watumishi wema, watiifu, wasiouliza maswali, wavumilivu, wenye bidii ya
kutapanya mapato ya familia kwa kuchangamkia bidhaa na starehe za
kizungu badala ya kuchangamkia fursa za maendeleo.
Pia imetufanya tuwe walalamikaji wazuri na watu wanaokubali hali
yoyote ya maisha, hata iwe ngumu kiasi gani. Ni elimu inayojenga uoga
na utiifu usiohoji hata masuala ya msingi; inayojenga upole
unaorahisisha kutawaliwa kwa maslahi ya wengine.
Elimu ya kikoloni pia imetugeuza na kutufanya
tudharau mambo yetu na kujidharau au kukosa kujiamini. Elimu hii
imetugeuza kuwa watumwa kiasi kwamba sasa, miaka zaidi ya 53
tunaiendesha wenyewe kama ilivyokusudiwa na mkoloni.
Kwa maneno mengine, tunajigeuza kuwa watumwa wa
ukoloni sisi wenyewe kwa manufaa ya nchi tajiri na gharama ya kujigeuza
kuwa watumwa tunailipa sisi.
Kibaya zaidi, hatuamini kwamba hicho ndicho
tunachokifanya. Elimu pia imetufanya kuthamini kipato kuliko huduma
tunazotoa kwa jamii zetu; tukidai kuwa thamani yetu katika soko ni juu
zaidi kuliko mshahara tunaolipwa Tanzania.
Mwaka (1974), Mwalimu Nyerere alisema: ‘’Binadamu
pekee wenye thamani katika soko ni watumwa. Yaani bila kujitambua
tunasema kwamba elimu hii tuliyopata imetugeuza kuwa bidhaa za kuuzwa
sokoni kama pamba, katani au kahawa’’.
Katika mustakabali wa utandawazi na soko huria,
elimu tuliyoipata na tunayoendelea kutoa haitusaidii kama jamii, kwa
kuwa haitukomboi katika utumwa, bali inatuweka tayari kuwa watumishi
wema, watiifu, wasiouliza maswali, na wavumilivu wa mataifa tajiri.
Elimu yetu imekuwa mradi wa mataifa tajiri wa
kuendeleza ukoloni wao hata baada ya uhuru wa kisiasa. Tumegeuzwa
kitoweo ndani ya mfumo wa utandawazi.
Ndiyo maana kila anayesoma hafikiriii kuiendeleza
jamii anafikiri kuipora nchi, kujibadili kuwa kama mzungu, kufanya
starehe za kizungu, kuongea lugha za kizungu na kudharau kila kilicho
chetu.
Haijatuandaa kutafuta suluhu au kujiuliza namna ya
kujikwamua. Tumebaki kulalamika na kukosa matumaini. Hata viongozi,
maprofesa, madaktari wasomi wa falsafa wanalalamika; tumechanganyikiwa,
hatujui tulipokosea na tunaamua kuukataa ukweli tunaoujua!
Wageni wanaokuja nchini na elimu ndogo tu iliyo
sahihi wanachangamkia fursa zetu na kutajiriwa, sisi wanatukuta maskini
na tunabaki maskini wa kutupwa. Haya ni matunda ya elimu tuliyorithi na
tunayoendelea kutoa katika taifa letu na hata bara zima la Afrika.
Nimewahi kusema huko nyuma kuwa elimu tuliyopata imetuandaa kuulimbukia
utandawazi (na mengine yote watakayosema nchi tajiri) bila kutambua kuwa
ni mwendelezo wa ukoloni.
Ni muhimu tujiulize kama tunapenda kuendelea na
hali hii ya utumwa wa kujitumikisha wenyewe kwa manufaa ya mataifa
tajiri huku tukilipa gharama za kujigeuza watumwa, au tujikomboe na
tuondokane na utumwa huu.
Njia mojawapo ya kujikomboa ni kurudi katika
misingi ya elimu ya maadili ya mtu wa ndani, itakayo wakomboa Watanzania
kifikra, kiujuzi, kiutambuzi na mengineyo.
Chapisha Maoni