Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (katikati waliokaa)
akiwa katika picha ya pamoja na Watendaji wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa
Geita, baadhi ya Wabunge na Wakuu wa Wilaya za mkoa huo, Wawakilishi wa
Wachimbaji Wadogo na Watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini, Wakala
wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) na Shirika la Madini la Taifa
(STAMICO) mara baada ya kumaliza kikao kilichofanyika mjini Geita. Wa
Pili kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Geita, Meja Jenerali Mstaafu, Ezekiel
Kyunga.
Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (Wa Pili kulia) akiwa na
baadhi ya wananchi wa mkoa wa Geita, waliohudhuria kikao baina ya
Waziri na Watendaji wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, baadhi ya Wabunge
na Wakuu wa Wilaya za mkoa huo, Wawakilishi wa Wachimbaji Wadogo na
Watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini, Wakala wa Ukaguzi wa Madini
Tanzania (TMAA) na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) mara baada ya
kumaliza kikao kilichofanyika mjini Geita. Kikao kililenga katika
kujadili suala la magwangala na maeneo ya wachimbaji wadogo nchini.
Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (katikati waliokaa)
akiwa katika picha ya pamoja na Watendaji wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita
(GGM), Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, baadhi ya Wabunge na Wakuu wa
Wilaya za mkoa huo, Wawakilishi wa Wachimbaji Wadogo na Watendaji wa
Wizara ya Nishati na Madini, Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA)
na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) mara baada ya kumaliza kikao
kilichofanyika mjini Geita. Wa Pili kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Geita,
Meja Jenerali Mstaafu, Ezekiel Kyunga.
Na Teresia Mhagama, Geita.
MGODI
wa Dhahabu wa Geita (GGM) uliopo mkoani Geita umeridhia ombi la
Serikali la kutoa mabaki ya mawe ya dhahabu kwa wananchi ili kuweza
kuyachenjua na kupata dhahabu.
Hayo
yameelezwa mjini Geita na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter
Muhongo mara baada ya kumaliza vikao vya majadiliano kati ya watendaji
wa GGM, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, baadhi ya Wabunge na Wakuu wa
Wilaya za mkoa huo, Wawakilishi wa Wachimbaji Wadogo na Watendaji wa
Wizara ya Nishati na Madini, Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA)
na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO).
“Tatizo
la Magwangala sasa limetatuliwa kwani Mgodi umekubali kuyatoa kwa
wananchi ila kinachotakiwa kufanywa kabla ya kuyatoa magwangala hayo ni
Serikali ya Mkoa huu kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali kuhakikisha
kuwa kwanza wanapata eneo ambalo uchenjuaji wa magwangala utafanyika,”
alisema Profesa Muhongo.
Aidha
aliongeza kuwa eneo hilo litakalotengwa na Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa
Geita lazima lifanyiwe tathmini ya mazingira na Baraza la Hifadhi na
Usimamizi wa Mazingira (NEMC) ili kuweza kuthibitika kama eneo hilo
linafaa kwa shughuli hizo bila kuleta athari kwa wananchi na mazingira.
Profesa
Muhongo alitoa agizo kuwa kazi hizo zinatakiwa kukamilika tarehe 30
Juni, mwaka huu ambapo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa itafanya kikao
kitakachohudhuriwa na watendaji wa Mgodi na Wabunge wa mkoa huo na
kutoa uthibitisho wa kimaandishi kuhusu eneo lililotengwa kwa shughuli
hiyo pamoja na Cheti kutoka NEMC cha uthibitisho kuwa eneo hilo linafaa
au halifai kwa shughuli za uchenjuaji madini kufanyika.
Aidha
alieleza kuwa katika kikao hicho cha tarehe 30 Juni GGM itapaswa pia
kutoa uthibitisho wa kimaandishi kuwa imekubali kutoa magwangala hayo
kwa wananchi.
“Baada
ya Eneo hilo na Cheti cha mazingira kupatikana, sasa katika kikao
hicho mtaweza kujadiliana kuhusu usafirishaji wa magwangala hayo
kutoka eneo la Mgodi hadi eneo lililotengwa, hapo mtakubaliana nani
atachukua jukumu la kusafirisha magwangala hayo,”alisema Profesa
Muhongo.
Aliongeza
kuwa Leseni za uchenjuaji madini zitakazotolewa mara baada ya eneo
hilo kupatikana, zitakuwa katika vikundi na si mtu mmoja mmoja ambapo
Ofisi ya Mkuu wa mkoa ndiyo itakayoratibu suala hilo huku jukumu la
Wizara likiwa ni kutoa Leseni hizo.
“Ni
vizuri pia mkashirikiana na viongozi wa Wachimbaji Wadogo katika
kuratibu uundaji wa vikundi hivyo na lazima vikundi hivyo vielezwe kuwa
ni lazima walipe kodi stahiki kwa Serikali kama ilivyo kwa shughuli
nyingine za uchenjuaji madini,” alisema Profesa Muhongo.
Kwa
nyakati tofauti Wabunge wa mkoa huo walieleza kuwa utoaji wa Magwangala
hayo kwa wananchi, utasaidia wanachi hao kujiajiri, kujiongezea kipato
na kuwaepusha katika kushiriki matendo ya uhalifu.
Chapisha Maoni