HOME
Kikwete- Tumshukuru Mungu
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dkt.Ally Mohamed Shein walioinua rasimu ya katiba muda mfupi baada ya kukabidhiwa na aliyekuwa mwenyekiti wa bunge maalum la katiba Mh.Samwel Sitta
RAIS Jakaya Kikwete amesema, tukio la
kukabidhiwa Katiba Inayopendekezwa ni muhimu na la kihistoria
linalokidhi matakwa ya Sheria, alisema kukamilika kwake kunabakiza hatua
moja ya mwisho ya wananchi wote kupiga kura ya maoni kufanya uamuzi wa
katiba mpya.
“Tumshukuru Mwenyezi Mungu kwa hapa
tulikofikia,…hakika Mungu anaipenda nchi yetu,” alisema na kumpongeza
Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta na Makamu wake,
Samia Suluhu Hassan kwa kazi waliyoifanya pamoja na wajumbe wengine
kukamilisha kazi hiyo kwa kiwango cha juu.
Alisema, “haikuwa kazi rahisi hata
kidogo, kulikuwa na milima na mabonde, na wakati mwingine mawimbi ambayo
yalikuwa makali yalielekea kuwa tufani.” Alisema mchakato wa katiba
mpya ni jambo jema aliloanzisha kwa nia njema ingawa lilipokewa kwa
hisia tofauti.
Alisema wapo walioona kwamba
halitawezekana lakini yeye alibaki kuwa mmoja wa walioamini kwamba
litawezekana. Kwa mujibu wake, Desemba 31, 2010 alipotangaza dhamira ya
kuanza mchakato wa katiba, ilipokewa kwa hisia tofauti; kwa maana wapo
waliunga mkono moja kwa moja, wapo waliopinga na waliobaki katikati.
Akisimulia, alisema jambo ambalo wengi
hawalifahamu, miongoni mwa makundi yaliyopinga yalikuwamo pia ndani ya
Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Nakumbuka walikuwapo baadhi ya watu
waliodiriki hata kulihoji na kuniambia kuwa wewe jambo hili umelizua
wapi?...Hii si ajenda ya CCM bali ni ya watu wengine.” Alisema
aliwaambia hiyo ni ajenda ya Watanzania na kwamba yeye ndiye mwaklishi
wao mkuu ambaye ana dhamana hiyo.
“Nashukuru Mungu baada ya mjadala mkali,
tukaelewana,” alisema na kuendelea kusimulia kwamba, “walikuwepo pia
watu walioondoka pale shingo upande wakisema jamaa anaingiza jambo
ambalo si letu”.
Kwa mujibu wa Rais Kikwte, baadhi ya
waliokuwa wakali kwenye NEC na Kamati Kuu ya chama, aliwateua kuwa
wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba ambao hata hivyo, alisema anafurahi
kwamba watu hao wamekuwa msaada na kutoa mchango mkubwa uliowezesha
bunge kupendekeza katiba iliyo nzuri.
Alisema hatimaye wameelewa hoja na haja
ya kuandika katiba mpya; ulioanza mwaka 2011 kwa Serikali kuandaa
Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ambao ulijadiliwa na
kupitishwa Novemba 18, 2011.
Changamoto nyingine alizosema ni
‘sintofahamu’ iliyojitokeza kwenye Bunge ambayo baadhi ya wabunge
walisusa wakitaka Rais asiridhie muswada wa sheria hadi hapo
yatakapofanyika marekebisho waliyoona wao ni muhimu. Wakakubaliana kuwa
kila chama kilete mapendekezo ya marekebisho wanayoona yanafaa
yafanyike.
Wakawa na kamati ya pamoja kati ya serikali na wao, wakachambua moja baada ya jingine wakakubaliana kuwasilisha kwenye bunge.
Akizungumzia mara nyingine baadhi ya
wabunge (Ukawa) kususa, Rais Kikwete alisema wabunge waliobaki na hasa
wengi wao wakiwa wa CCM, walikuwa wakimwambia safari hii asikutane nao,
awaache kwamba kazi wataifanya na kumaliza bila ya wao.
“Niliwasikiliza lakini nikafanya uamuzi
wa kiuongozi; kwamba lazima tufanye jitihada shughuli hii tuifanye wote
tuimalize wote,” alisema.
Aidha, alisema kutokana na mchakato wa
bunge kukumbwa na malumbano ya mara kwa mara, pia alikuwa akishauriwa
ikiwamo kupokea meseji nyingi zilizomtaka avunje Bunge Maalumu la
Katiba.
Chapisha Maoni