HOME
Jk utatekeleza lini ahadi ya meli Ziwa Victoria
Wiki moja iliyopita abiria 381 waliokuwa katika
meli ya Mv Victoria walinusurika kufa baada ya chombo hicho kilichokuwa
kikifanya safari kutoka Bukoba kwenda Mwanza kuzimika ghafla.
Meli hiyo ilipata hitilafu katika usukani na
baadaye injini zake kuzimika zaidi ya mara mbili kabla ya kujikongoja
hadi Bandari iliyo karibu ya Kemondo.
Uchakavu wa Mv Victoria umelalamikiwa kwa muda
mrefu lakini hakuna juhudi za maana zilizochukuliwa kuhakikisha kuwa
meli hiyo inafanyiwa ‘ukarabati wa maana’.
Katika kampeni za urais mwaka 2010 Rais Jakaya
Kikwete kwa kuelewa ubovu wa meli hiyo aliahidi kununua meli kubwa
kuliko Mv Bukoba ambayo ilizama mwaka 1996.
Kwa tafsiri ya kawaida, ahadi ya Rais Kikwete
ilitokana na hali halisi ya meli zinazotoa huduma ya usafiri katika Ziwa
Victoria kuchoka. Kinachoshangaza ni je, tangu mwaka 2010 hadi sasa
Serikali imekosa fedha za kununua meli mpya? Pia kama imekosa,
imeshindwa hata kuifanyia ukarabati wa maana meli hii kongwe?
Mv Bukoba ilizama na kuua abiria zaidi ya 1,000.
Tukio hili halijasahaulika kwa Watanzania ambao bado wanahoji iko wapi
meli mpya waliyoahidiwa na Rais Benjamin Mkapa baada ya kutokea ajali ya
Mv Bukoba.
Mkapa ameshaondoka madarakani, sasa iko wapi meli
mpya iliyoahidi? Iko wapi meli iliyoahidiwa na Rais Kikwete wakati wa
kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, nasema hivyo kwa sababu Rais
Kikwete amebakiwa na mwaka mmoja tu wa kuwa madarakani.
Nakumbuka Mei 30, 2011 wakati akizungumza na
wananchi wa eneo la Usagara, Bukumbi, Wilaya ya Misungwi, Mkoa wa
Mwanza, kabla ya kuzindua rasmi barabara ya lami ya kilomita 90 kutoka
Usagara hadi Geita, Rais Kikwete alisema mchakato wa kununua meli mpya
kwa ajili ya kusafirisha abiria katika Ziwa Victoria umeanza.
Alieleza kwamba wataalamu washauri wa kupatikana
kwa meli hiyo, yaani Kampuni ya OSK-Ship Tech ya Denmark, tayari
wamekamilisha upembuzi yakinifu juu ya aina ya meli inayofaa kwa
matumizi katika Ziwa Victoria.
Mboga ikatiwa chumvi kuwa eti, fedha za ununuzi wa
meli hiyo zitatengwa katika Bajeti ya Serikali ya mwaka 2012/2013 baada
ya kuwa maandalizi yote ya ununuzi wa meli hiyo kuwa yamekamilika.
Mboga ikapakuliwa kabisa, kwamba kazi ya tathmini
ya kuzikarabati meli za Mv Victoria, Mv Umoja na Mv Sengerema ambazo
zote zinatoa huduma ya usafiri wa abiria na mizigo katika Ziwa Victoria
umefanywa na sasa fedha zinatafutwa kwa ajili ya kuanza kazi yenyewe ya
ukarabati.
Ni swali tu nimemuuliza rais wangu Kikwete. Sijui
kama nitapatiwa majibu lakini lengo langu ni kufahamu tu maendeleo ya
upembuzi yakinifu na zile tathmini za meli hizo nilizozitaja hapo juu,
yavyokwenda mpaka sasa.
Tusisubiri meli izame ndio tuanze mipango ya kuleta meli mpya.
Tusisubiri meli izame ndio tuanza mipango ya kuzikarabati meli zilizopo.
Kwa miaka mingi Watanzania tumekuwa na utaratibu wa kuishi kwa matukio,
ikianguka ndege itajadiliwa na ukurasa utafungwa bila ufumbuzi
kupatikana, hivyo hivyo kwa meli, treni na ajali za barabarani.
Chapisha Maoni