Sababu za kusema hapana kwa Katiba Inayopendekezwa
Sheria ya Kura ya Maoni, Sheria namba 4 ya Mwaka
2014 inaweka masharti haya “35(3) Pale ambapo kura zilizopigwa za
“NDIYO” ya swali la kura ya maoni hazijazidi asilimia 50 ya jumla ya
kura halali zote zilizopigwa Tanzania Bara au Tanzania Zanzibar, Tume ya
Taifa ya Uchaguzi, kwa kushirikiana na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar na
kwa taarifa itakayotangazwa katika Gazeti la Serikali, itateua siku
nyingine ya kupiga kura ndani ya siku 60 baada ya kutangazwa matokeo, na
itarudia utaratibu wa kupiga kura ya maoni ambao utaanza upya. (4) Kwa
kuzingatia masharti ya kifungu kidogo cha (3), Tume ya Taifa ya
Uchaguzi, na pale ambapo mazingira yatahitaji, inaweza: (a) kutoa muda
wa kutosha kwa ajili ya uhamasishaji na kutoa elimu juu ya kura ya maoni
ya Katiba inayopendekezwa; au (b) kutoa muda unaofaa kwa Rais, kwa
kukubaliana na Rais wa Zanzibar kuitisha Bunge la Katiba kwa dhumuni la
kuangalia upya vifungu vya Katiba” tafsiri ni yangu.
Kifungu cha 35(5) cha Sheria hii kinaeleza itakuwa
ni katika duru ya pili ya kura ya Maoni ndipo wakati ambao iwapo
wananchi watasema HAPANA kwa mara ya pili ndipo Katiba ya Mwaka 1977
itaendelea kutumika.
Ninachojaribu kusema ni kwamba kusema hapana kwa
Katiba Inayopendekezwa siyo dhambi wala utovu wa nidhamu, ni fursa
iliyopo kisheria kabisa. Pongezi zangu za dhati ziwaendee wasanifu na
waandishi wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na baadaye Sheria ya Kura ya
Maoni kwa kuweka kifungu hiki cha kizalendo. Kifungu hiki ni kama
kilikuwa kinatoa unabii kwamba kuna uwezekano wa Bunge Maalumu kutoka na
Katiba Inayopendekezwa ambayo haijakidhi vigezo ambavyo wananchi
wanataka. Wasanifu na waandishi wa Sheria hii waliona ni vema na haki
kwamba wananchi wawe na fursa ya kuitizama kwa jicho pevu Katiba
Inayopendekezwa na kama ina mapungufu waipe kura za kutosha za HAPANA
ili Mheshimiwa Rais aliitishe Bunge Maalumu ili kuangalia upya vifungu
vya Katiba Inayopendekezwa.
Mimi ninaendelea kuwasisitiza kwamba wakati
ukifika tuseme HAPANA ili Bunge Maalumu liitishwe tena na ninatumaini
kipindi hiki hakutakuwa na mipasho, vitimbwi, vijembe, lugha za matusi,
kejeli na nidhamu ya Bunge Maalumu itakuwa ya hali ya juu. Bunge Maalumu
litakaloitishwa baada ya kupata kura ya HAPANA katika duru ya kwanza ya
Kura ya Maoni litakuwa na nidhamu tofauti na hili lililomaliza muda
wake, angalau nidhamu ya woga kwamba wananchi siyo watu wa kupuuzwa.
Vifuatavyo hapa chini ni vifungu ambavyo Bunge
Maalumu lilivifuta kutoka katika Rasimu ya Warioba na kwa kuvifuta
waliondoa msingi wa uimara na uthabiti wa Katiba kama Mkataba wa Kijamii
(social pact) kati ya wananchi na viongozi wao, Sheria Kuu ya Nchi na
Msingi wa Sheria.
Sasa kwa wale wenye mapenzi mema na Baba wa Taifa
Mwalimu Nyerere na wale walio tayari kufa kwa ajili ya Azimio la Arusha,
hebu oneni yaliyofutwa na Bunge Maalumu katika Katiba Inayopendekezwa
1. Zawadi katika Utumishi wa Umma
15.-(1) Kiongozi wa umma wakati anapotekeleza
shughuli za kiserikali, akipewa zawadi, zawadi hiyo itakuwa ni mali ya
Jamhuriya Muungano na ataiwasilisha kwa Katibu Mkuu Kiongozi kupitia kwa
Katibu Mkuu wa Wizara au kiongozi wa taasisi ya Serikali inayohusika,
akiainisha: aina ya zawadi; thamani ya zawadi; sababu ya kupewa zawadi;
na mtu au mamlaka iliyotoa zawadi hiyo. (2) Neno “zawadi” kama
lilivyotumika katika Ibara hii linajumuisha kitu chochote chenye thamani
atakachopewa Kiongozi wa umma katika utekelezaji wa shughuli za umma.
(3) Bunge litatunga sheria itakayosimamia, pamoja na mambo mengine,
thamani, kiwango, aina na uhifadhi wa zawadi kwa Jamhuri ya Muungano.
2. Akaunti nje ya Nchi na Mikopo
16. Kiongozi wa umma - hatafungua au kumiliki
akaunti ya benki nje ya Jamhuri ya Muungano isipokuwa tu kwa namna
ambayo sheria za nchi zinaruhusu; na hataomba au kupokea mkopo au faida
yoyote kwa namna au mazingira ambayo yanashusha hadhi au heshima ya
utumishi wa umma.
3. Wajibu wa Kutangaza Mali na Madeni
17-(1) Kiongozi wa umma atalazimika kutangaza na
kuwasilisha, ndani ya siku thelathini baada ya kupata uongozi na baada
ya kuacha uongozi, mali na thamani yake na madeni yake katika Tume ya
Maadili ya Uongozi na Uwajibikaji. (2) Bila ya kuathiri masharti ya
ibara ndogo ya (1), Kiongozi wa umma atalazimika kutangaza na
kuwasilisha taarifa ya mali na madeni: yake binafsi; ya mwenza wake wa
ndoa; na ya watoto wake walio chini ya umri wa miaka 18, mara moja kila
mwaka kwa Tume ya Maadili ya Uongozi na Uwajibikaji. (3) Bunge litatunga
sheria itakayosimamia, pamoja na mambo
mengine: ngazi au orodha ya viongozi wa umma wanaopaswa
kutangaza mali na madeni yao; na utaratibu wa kuwasilisha taarifa ya
mali na madeni kwa Tume ya Maadili ya Uongozi na Uwajibikaji kwa mujibu
wa Katiba hii.
4. Mgongano wa Maslahi
18.-(1) Kiongozi wa umma hatashiriki katika
kufanya uamuziwa jambo au shughuli yoyote ambayo ana maslahi nayo yeye
binafsi, mwenza wake, mtoto wake, jamaa yake, rafiki au mtu yeyote
wakaribu. (2) Kiongozi wa umma hatazungumzia kitu chochote katika Baraza
la Mawaziri, Bunge, Kamati au chombo kingine chochote rasmi ambacho ana
maslahi nacho ya moja kwa moja au vinginevyo, isipokuwa tu kama atatoa
taarifa ya mgongano huo wa maslahi katika chombo hicho. (3) Itakuwa ni
marufuku kwa Kiongozi wa umma kushiriki katika uamuzi unaohusu kuongeza
au kuboresha maslahi kwa namna yoyote ile yanayohusu wadhifa alionao, na
endapo atashiriki, basi masharti hayo mapya yataanza kutumika kwa
kiongozi wa umma atakayekuja baada ya kiongozi husika kuondoka au
kumaliza muda wa kukaa katika nafasi ya madaraka iliyompatia fursa ya
kushiriki katika kuamua maslahi husika. (4) Masharti ya ibara ndogo ya
(3), hayatamuhusu kiongozi wa umma ambaye kutokana na asili ya nafasi ya
madaraka au aina yakazi zake anapaswa kushiriki katika upangaji wa
mishahara au maslahi mengine ya watumishi wa umma. (5) Kiongozi wa umma
hataruhusiwa kushika nafasi za madaraka zaidi ya moja au kutumikia
mihimili ya Dola zaidi ya mmoja kwa wakati mmoja.
5. Matumizi ya Mali za Umma
19. Kiongozi wa umma hataruhusiwa kutumia au
kuruhusu kutumika kwa mali yoyote ya umma, zikiwemo zilizokodishwa kwa
Serikali, kwa madhumuni ya kujipatia yeye binafsi au kumpatia mtu
mwingine manufaa yoyote.
6.Utekelezaji wa Masharti ya Maadili
20.-(1) Bunge litatunga sheria itakayosimamia, pamoja na mambo mengine:
utaratibu wa utwaaji wa mali za viongozi wa umma zilizopatikana kwa kukiuka sheria;
utaratibu wa kumwajibisha Kiongozi wa umma
aliyekiuka maadili na Miiko ya Uongozi; na uanzishaji wa mitaala
inayohusu Katiba, maadili na uraia, shuleni na vyuoni.
(2) Masharti yaliyoainishwa katika Sehemu hii ya
Sura ya Tatu yatatumika pia kwa watumishi wa umma baada ya kufanyiwa
marekebisho stahiki.
7.Utii wa Miiko ya Uongozi wa Umma
21.-(1) Bila ya kuathiri masharti ya Katiba hii,
kiongozi wa Umma atapaswa kuheshimu na kutii maadili ya viongozi wa
umma, ikiwemo Miiko ya Uongozi. (2) Miiko ya Uongozi inayorejewa katika
ibara ndogo ya (1), itakuwa kama ifuatavyo: (a) Kiongozi wa umma
hatopaswa – kuvunja au kukiuka masharti ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano;
kutoa au kupokea rushwa; kujilimbikizia mali kinyume cha sheria;
kusema uongo au kutoa taarifa zisizo za ukweli; kutoa siri za Serikali
kinyume cha sheria; kutumia wadhifa, nafasi au cheo chake kwa manufaa
yake binafsi, familia yake, ndugu, jamaa au marafiki zake au mtu yeyote
aliye na uhusiano naye wa karibu; kufanya vitendo vya uzembe, uvivu,
ubaguzi, kiburi, dharau au unyanyasaji wa kijinsia. (b) Kiongozi wa umma
atapaswa kuheshimu na kuendeleza - dhana ya uwajibikaji wa pamoja kwa
viongozi wanaohusika; na maadili na Miiko ya Uongozi wa Umma,
ikijumuisha:
(aa) kuwa na tabia na mienendo inayokubalika
katika jamii; (bb) kuheshimu, kutunza na kulinda mali za umma; na (cc)
kutambua, kuheshimu na kuzingatia Kanuni za Maadili na Mienendo ya
Watumishi wa Umma, Kanuni za Kudumu za Watumishi wa Umma, nyaraka za
umma na miongozo mbalimbali ya Serikali kuhusu viongozi na watumishi wa
umma. kutenganisha biashara na shughuli binafsi na masuala yanayohusiana
na uongozi. (3) Kiongozi wa umma ambaye anatuhumiwa kwa makosa ya:
kimaadili; udhalilishaji wa mtu au wa kijinsia; au wizi au ubadhirifu wa
mali za umma, atasimamishwa kazi hadi suala lake litakapoamuliwa kwa
mujibu wa sheria za nchi au taratibu nyingine zinazowahusu viongozi wa
umma.
ANGALIZO
Ndugu wananchi nimefuatilia wale wanaopigia chapuo
Katiba Inayopendekezwa kuna mambo wanapotosha sana na muwe macho. Kwa
mfano, juzi katika kipindi kimoja cha Televisheni ya “Wote” kuna
waliokuwa wajumbe wa lililokuwa Bunge Maalumu walikuwa wanatoa elimu juu
ya Katiba Inayopendekezwa na wakawa wanaizungumzia Katiba
Inayopendekezwa kwa kuilinganisha na Katiba ya Mwaka 1977, hiyo ni
hadaa.
Ulinganifu wa kuonesha Katiba Inayopendekezwa ni
bora au la unapaswa kupimwa kwa kuonesha ni kiasi gani Katiba
Inayopendekezwa imeyaweka sawa maoni ya wananchi kama ambavyo yalikuwa
katika Rasimu ya Warioba.
Chapisha Maoni