HOME
Warioba awasuta kwa Nyerere, vurugu zaibuka
Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa
zamani, Jaji Joseph Sinde Warioba jana alivamiwa na kikundi cha watu
wachache waliohudhuria mdahalo wa Katiba wakati akihoji vitendo vya
baadhi ya watu kutumia vibaya jina la Baba wa Taifa, Mwalimu Julius
Nyerere.
Jaji Warioba, ambaye alikuwa msemaji mkuu kwenye
mdahalo huo ulioandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere, alikuwa
akihitimisha hotuba yakle aliyoianza saa 9:15 alasiri, kwa kuhoji kuhusu
watu wanaotumia vibaya jina la Mwalimu Nyerere kupitisha hoja zao
katika misingi isiyokubalika.
Vurugu hizo zilidumu kwa takriban dakika 45 ndani
ya ukumbi wa mikutano wa hoteli ya Blue Pearl, Ubungo lakini katika hali
isiyokuwa ya kawaida wasaidizi wa waziri huyo mkuu wa zamani, walimtoa
ukumbini dakika 30 baada ya sakata hilo kuanza, hali iliyowapa nafasi
vijana hao walionekana kujiandaa kufanya vurugu, kumsogelea na kumpiga.
Baadhi ya watu walionekana kumzonga Jaji Warioba
ambaye alikuwa mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ni pamoja na
aliyekuwa mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Paul Makonda. Baada ya tukio
hilo, polisi waliokuwa na silaha na wakiwa wamevalia nguo za kiraia
walimtoa Jaji Warioba ukumbini.
Makonda na Amon Mpanju, ambaye pia alikuwa mjumbe
wa Bunge Maalum la Katiba, nao waliokolewa na polisi kutokana na vijana
walioonekana kumuunga mkono Jaji Warioba kuwatuhumu kuhusika kwenye
vurugu. Makonda aliambulia kipigo na kulazimika kujificha katika moja ya
ofisi zilizopo hotelini hapo.
Mbali na Jaji Warioba, wajumbe wenzake wa
iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambao ni Humphrey Polepole,
Profesa Paramagamba Kabudi, Profesa Mwesiga Baregu, Awadhi Said na Ester
Mkuchu nao walitolewa kwenye ukumbi huo na kupelekwa katika chumba
maalum hotelini hapo.
Akitolea mfano watu wanaotumia vibaya jina la
Mwalimu Nyerere kiasi cha kuwashangaza hata wale waliowahi kuishi naye
kwa karibu, Jaji Warioba alihoji iwapo Mwalimu Nyerere angekuwa hai
angekubali mambo haya yapite.
Baadhi ya mambo aliyodai kuwa hata Mwalimu Nyerere
asingeweza kuyapinga ni miiko ya uongozi, viongozi kupokea zawadi na
kuzimiliki.
“Watu walimuandikia barua Mwalimu Nyerere
kumshawishi kuwa fedha zake zitakuwa salama kama ataziweka nje ya nchi,
siyo kama alikataa tu, alitangaza jambo hilo katika vyombo vya habari,”
alisema.
Huku akizungumza kwa mtindo wa kuuliza swali Jaji
Warioba alisema: “Nauliza, hivi, Mwalimu Nyerere angekataa miiko ya
uongozi isiingizwe katika katiba? Angekubali watu wawe na akaunti nje ya
nchi? Watu wapate zawadi wakae nazo? Labda huyo si Mwalimu.”
Jaji Warioba, ambaye alianza kushangiliwa kwa
nguvu baada ya kuzungumza mambo hayo, alisema: “Kwa sisi tunaomjua
vizuri Mwalimu, tunajua kuwa ndio yuleyule ambaye alilipitia Azimio la
Arusha lililokuwa msingi wa utu na kutoona hata sehemu moja yenye makosa
ya kurekebisha.”
Mifano hiyo iligeuka ‘mwiba mchungu’ kwa baadhi ya
waliohudhuria mdahalo huo ambao walionekana kujiandaa kutokana na
kwenda ukumbini hapo na mabango yanayoonyesha kukubali Katiba
Inayopendekezwa.
Baada ya mneno hayo, watu hao walisimama na kunyanyua mabango
yaliyokuwa yamebeba ujumbe mbalimbali, ukiwemo “Katiba Inayopendekezwa
tumeipokea na tumeikubali”.
Kitendo hicho kiliwakera baadhi ya washiriki
kwenye mdahalo huo ambao walisimama na kuanza kuwakamata waliokuwa
wamebeba mabango hayo na kuanza kuyachana.
Licha ya Jaji Warioba na mshehereshaji wa mdahalo
huo, Said Kubenea kuwataka washiriki kutulia, vurugu zilizidi na kudumu
kwa dakika 45 huku viti vikirushwa kutoka upande mmoja kwenda mwingine
na kusababisha watu kukimbia hovyo.
Wakati washiriki wakikimbilia nje, walikutana na
polisi ambao walipiga mabomu ya machozi ya kuwafanya baadhi yao kurejea
ndani ya hoteli hiyo.
Baada ya hali kutulia Joseph Butiku, ambaye ni
mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, alirudi ukumbini na kueleza
kuhuzunishwa na kilichotokea na kufafanua kuwa kutokana na hali ya
kiusalama ni vyema mkutano huo ukaahirishwa.
Akizungumza kwa masikitiko, Butiku alisema: “Hata
enzi za Nyerere aliwahi kupita katika wakati mgumu. Lakini haikuwahi
kufikia hatua ya watu kupigana ngumi na mateke na kurushiana viti kama
tuliyoshuhudia hapa. Kutokana na aibu iliyotokea leo, kwa nia njema ya
kuzuia lisije tokea jingine zaidi, tunaahirisha mdahalo huu kwa ajili ya
kwenda kujipanga vizuri zaidi.”
Butiku alisema anawafahamu baadhi ya watu
walioandaa vurugu hizo na kusisitiza kuwa watu wa aina hiyo
hawataruhusiwa kushiriki kwenye midahalo hiyo ambayo itaendelea kuwepo
katika maeneo mengi ya nchi ili kutoa fursa kwa wananchi kujadili namna
ya kupata katiba iliyo bora.
Mpaka gazeti hili linaondoka hotelini hapo,
Makonda alikuwa hajatoka eneo ambako inadaiwa alijificha huku Jaji
Warioba akiondolewa chini ya ulinzi mkali.
Alipotoka eneo la nje ya hoteli hiyo, Jaji Warioba
alikumbana na umati mkubwa wa watu ambao walikuwa wakiimba nyimbo za
kumsifu na kumuita kuwa ndio rais ajaye wa Tanzania.
Kabla ya vurugu
Shangwe, vifijo na nderemo zilitawala kutoka kwa
zaidi ya watu wengi waliohudhuria mdahalo huo wakati Jaji Warioba na
wenzake walipokuwa wakiingia ukumbini saa 9:00 alasiri.
Kabla ya Jaji Warioba kuanza kuzungumza katika mdahalo huo ambao
pia ulihudhuriwa na makada wa CCM na Chadema, Butiku alisema: “Hayawi
hawayi, sasa yamekuwa. Tume imeshamiliza kazi na Bunge nalo lmeshamaliza
kazi yake. Lengo ni moja tu, ni maendeleo yetu sote.”
Aliongeza: “Sasa tujadili kwa utulivu kwani
hatusimamiwi na makundi na badala yake tunaijadli Katiba kwa sheria,
hakuna kutishana, kuogopa mtu wala kusimamiwa na chama na hata
shinikizo,”
“Miaka ijayo tusije tukawa kwenye kundi la wajinga
na kushindwa kujua tulikuwa tunajadili nini ili tuepuke maswali kutoka
kwa wajukuu zetu na watoto pia.’’
Warioba
Kabla ya Jaji Warioba kuanza kuzungumza,
mshehereshaji wa mdahalo huo Hamza Kassongo alimuomba atoe jibu kama ni
kweli Katiba Inayopendekezwa imebeba asilimia 80 ya maudhui ya rasimu ya
Pili ya Katiba.
Jaji Warioba alianza kwa kuifafanua Sheria ya Kura
ya Maoni kuwa inamtaka wiki mbili baada ya rais kukabidhiwa Katiba
Inayopendekezwa kuitangaza katika gazeti la Serikali na kuiagiza Tume ya
Uchaguzi (NEC) kuanza kusimamia mchakato huo.
Pia alieleza kuwa kazi ya kutoa elimu kwa wananchi
itakayofanywa na NEC na asasi za kiraia kwa mujibu wa sheria hiyo
inatakiwa kufanyika kwa siku 60, baada ya hapo itafanyika kampeni kwa
muda wa mwezi mmoja.
“Sheria inasema Kamati ya Kampeni ndiyo itafanya
kampeni. Kamati hizo zinakuwa mbili ambazo ni Kamati ya Kitaifa na ya
Jimbo. Kamati moja ni ya kuungaa mkono Katiba Inayopendekezwa na ya pili
ni ya kupinga, zote lazima zisajiliwe na NEC. Baada ya kampeni NEC
itasimamia upigaji kura, kuhesabu na kutangaza matokeo,” alisema.
Jaji Warioba alikosoa utaratibu wa kufanya
maboresho daftari la kudumu la wapigakura na kuonyesha wasiwasi wake
kama kura ya maoni itaweza kufanyika kama sheria inavyosema kutokana na
kamati kutoundwa na muda wa NEC kuwa mdogo.
Katiba Inayopendekezwa
Akigusia Katiba Inayopendekezwa, Jaji Warioba alisema kuna
baadhi ya mambo ya muhimu yaliyokuwa katika rasimu ya Katiba
yameondolewa
“Katiba Inayopendekezwa haijasambazwa ipasavyo.
Tunatakiwa kutotazama wingi au uchache wa ibara, tutazame Katiba ina
mabadiliko gani,” alisema.
Aliyataja mabadiliko ambayo hayapo katika Katiba
ya sasa lakini yalikuwepo kwenye Rasimu kuwa ni tunu na maadili na
kusisitiza kuwa mambo hayo yalikuwa mapya.
Pia aligusia kuondolewa kwa madaraka ya wananchi
katika Katiba Inayopendekezwa, mawaziri kutokuwa wabunge, madaraka ya
rais kutopunguzwa, mgombea binafsi kuwekewa masharti mengi, haki
mbalimbali kutodaiwa mahakamani, idadi ya wabunge kuongezwa pamoja na
muundo wa muungano kuwa unazidisha kero baada ya kuzipunguza.
Mabango, wasemavyo washiriki
Baadhi ya vijana waliobeba mabango ya kuunga mkono Katiba Inayopendekezwa walilalamikia vurugu walizofanyiwa ukumbini.
“Wamechana mabango yetu… walichokifanya ni kuzuia
uhuru wetu wa kutoa mawazo yetu,” alisema mmoja ya vijana hao
aliyejitambulisha kwa jina la John Ndumbaro.
“Warioba anapingana na Katiba Inayopendekezwa,
lakini sisi tunaipenda na ndiyo maana tumekuja na ujumbe wa kuielewa,
kuipenda na kuikubali.”
Asilimia kubwa ya mabango yalikuwa yanafanana yakiwa na ujumbe wa Katiba Inayopendekezwa tumeielewa, tunaipenda na tunaikubali.
Alipoulizwa iwapo kundi lao ni miongoni mwa
wafuasi wanaodhaniwa kutumwa na CCM kuvuruga mdahalo, Ndumbaro alisema
nchi inawagusa watu wote na kwamba hawakuwa wafuasi wa chama chochote
bali walienda kutetea nchi.
Naye Wagese Wilson alisema kilichotokea pale ulikuwa ni uhuni ambao anaamini ulipangwa na kikundi anachodhani ni cha wana-CCM.
“Kimsingi hizi vurugu ziliandaliwa kwa sababu ulinzi ulikuwepo
nje muda wote. Kwa nini baada ya purukushani kutokea zimepita takriban
dakika 40 bila polisi kuingia na kumlinda mtu mkubwa kama Warioba?”
alihoji.
Mmoja ya washiriki waliokuwa jirani kabisa wakati
Warioba akitolewa nje ya ukumbi, William Ndiyekeiya alisema alisikitisha
kuona kiongozi mkubwa kama Warioba akikosa ulinzi wa kutosha hasa
katika mdahalo wa kitaifa.
“Yule mtu wa CCM alikuwa nyuma ya Warioba huku
amemng’ang’ania na askari wa FFU (kikosi cha kutuliza ghasia) aliyekuwa
ameingia hakuonyesha hali yoyote ya kutaka kuwatenganisha.
“Hili ni tatizo la serikali la kushindwa kuleta
ulinzi mapema…dakika 45 baada ya vurugu ndiyo wanaleta askari ndani!
Lazima watambue kuwa Watanzania wa sasa siyo sawa na wale wa mwaka 1977
au 1982,” alisema Ndiyekieya.
Mpango wa Vurugu ulipangwa
Mmoja wa Wanafunzi wa Taasisi ya Maendeleo na
Usimamizi wa Maji (WMDI) ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa ajili ya
usalama wake, alisema kuwa juzi usiku kulikuwa na ujumbe mfupi uliokuwa
ukisambazwa ukitaka kujiandaa na mdahalo.
“Nilipokea ujumbe uliokuwa unatutaka leo muda wa
saa 6:30 kuja Ubungo Plaza na nauli zingetolewa… baadaye kidogo ujumbe
huo ulieleza kwamba hatukutakiwa kwenda na nguo za kijani wala njano kwa
sababu kulikuwa na shughuli maalumu,” kilisema chanzo hicho.
Alipouliza mtu aliyekuwa anawasiliana naye,
mwanafunzi huyo wa mwaka wa tatu, alijulishwa kuwa aliyetuma ujumbe
alikuwa ni mmoja wa viongozi wa chama kimoja chenye tawi chuoni hapo.
“Pale Chuo hakuna matawi ya vyama vingine…na
zitazame meseji zote hizi tulizokuwa tunachati akijaribu kutuelekeza
namna ya kuandaa ‘kazi hiyo maalumu’,” alisema.
“Hata baada ya kuingia ukumbini nilianza kuwaona
wanafunzi wenzangu kidogokidogo ambao walienda kujirundika upande mmoja
na baadaye kuanza kuonyesha mabango,” aliongeza huku akimuonyesha
mwandishi wetu meseji hizo.
Chapisha Maoni