HOME
Kikwete aiweka kura ya maoni njiapanda
Dodoma/Dar. Rais Jakaya Kikwete
jana alipokea Katiba inayopendekezwa kutoka kwa Mwenyekiti wa Bunge
Maalumu la Katiba, Samuel Sitta, na papo hapo kurejesha mpira kwa
viongozi wa Serikali kutafuta njia za kukamilisha mchakato huo.
Bunge la Katiba lilikamilisha kazi yake ya
kuandika Katiba mpya Oktoba 2 kwa kukamilisha upigaji wa kura za
kupitisha Rasimu ya Katiba ambayo ilitakiwa ipitishwe kwa theluthi mbili
ya kura kutoka kila upande wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mchakato huo wa kupata Katiba mpya unatakiwa
ukamilike kwa wananchi kupiga kura ya maoni, lakini Rais Kikwete jana
aliacha maswali ambayo alisema itabidi yafanyiwe kazi kabla ya
kukamilisha kazi hiyo ya kihistoria.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa Katiba
inayopendekezwa kwenye hafla iliyofanyika Uwanja wa Jamhuri mjini
Dodoma, Rais Kikwete alitaja maeneo matatu yenye utata ambayo yanatakiwa
kupatiwa ufumbuzi ili kufanikisha hatua hiyo.
Rais Kikwete, ambaye alianza kuzungumza kuanzia
saa 1:00 usiku hadi saa 2:25 usiku, alisema suala la kwanza ni ratiba
iliyotolewa na Tume ya Uchaguzi kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao ambayo
inaonyesha mchakato wa kuandika upya Daftari la Wapigakura utakamilika
Mei mwakani.
Alisema suala hilo litaingiliana na mchakato wa
Kura ya Maoni ambayo inatakiwa ifanyike katika muda wa siku 84 tangu
siku ambayo Rais amepokea Katiba inayopendekezwa.
Alisema ili suala hilo lifanikiwe, ni lazima
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ifanyiwe marekebisho, jambo ambalo
linaweza kushughulikiwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ambaye atatakiwa
kupeleka muswada bungeni.
“Ikifika mwezi Mei inabaki miezi miwili au mitatu
kabla ya Bunge kuvunjwa na hapo ndipo watu huanza kampeni, wenye kusema
‘iyenaiyena’, wenye kusema ‘peoples’ na wale wa haki… wanaanza kazi,”
alisema akimaanisha maneno yanayotumiwa na vyama vya CCM, Chadema na
CUF.
“Lakini wapo pia wanaopingana na NEC. Wao wanasema
mbona akifariki mbunge uchaguzi hufanyika. Jambo hili ninawaachieni na
pale ambapo litapatiwa ufumbuzi mtaelezwa.”
Alisema kutokana na uwapo wa utata huo, ni jambo
gumu kwa Katiba Mpya kupatikana kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kwa
sababu ya utata wa masuala hayo matatu, huku akisisitiza jambo hilo
kutazamwa ili kuona kama linaweza kupatiwa ufumbuzi.
Rais Kikwete pia aligusia hofu aliyokuwa nayo baada ya kutangaza nia yake ya kutaka Tanzania ipate Katiba mpya.
“Nilikuwa na hofu na kudhani kuwa jambo hili
halitawezekana, lakini kwa sababu lilikuwa jambo jema, Mwenyezi Mungu
amesaidia mpaka tumefikia katika hatua hii,” alisema.
“Wapo waliopingana na wazo langu na wapo waliokuwa katikati.
Jambo ambalo watu hawalifahamu ni kwamba makundi hayo yalikuwa ndani ya
CCM.”
Alisema kuwa wapo waliomhoji kwamba wazo la kuandika Katiba mpya alilitoa wapi na kwamba halikuwa ajenda ya CCM.
“Mimi niliwaeleza kuwa Katiba ni ajenda ya Watanzania na mimi ndiyo kiongozi wao.”
Alisema baada ya mjadala mkali alieleweka na
kusisitiza kuwa makada wa CCM waliokuwa wakali katika vikao vya chama
kuhusu kuandikwa kwa Katiba Mpya na kwamba aliwateua baadhi yao kuwa
wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba.
Rais Kikwete alielezea mvutano ulioibuka tangu
mchakato ulipoanza na vikwazo alivyokumbana navyo, ukiwamo msimamo wa
vyama vya upinzani vilivyosusia vikao vya Bunge na kulazimika kukutana
nao mara kwa mara.
“Hata lilipoanza Bunge Maalumu la Katiba wapo
wabunge waliosusia vikao vyake. Wajumbe wa CCM walinitaka nisikutane na
wajumbe waliosusia Bunge. Niliwasikiliza lakini niliamua kama kiongozi
kwa kufanya jitihada za kuzungumza na pande zote ili kujua tatizo,”
alisema.
Katika hotuba yake rais Kikwete alisema wapo
wanaopinga Katiba inayopendekezwa kwa sababu mambo wanayoyataka hayamo,
kuwataka wasubiri kwa maelezo kuwa wakati wa mambo wanayoyataka yawemo
katika Katiba haujafika.
Mwananchi lamgusa JK
Katika hotuba hiyo, Kikwete alionyesha kuguswa na
kichwa kimojawapo cha habari katika gazeti hili kilichozungumzia kura
zilizopigwa na wajumbe wa Bunge la Katiba kupitisha Katiba
inayopendezwa.
Akizungumzia wasiwasi uliokuwa umetanda wa
kutopatikana theluthi mbili kutoka Zanzibar, Rais Kikwete alisema watu
wengi walidhani ungekuwapo ugumu kuipitisha lakini baadaye ilipita.
“Kwa hali ilivyokuwa watu walijua
haitawezekana…Kuna hadi gazeti moja nilikuwa nasoma nikakuta limeandika
kuwa Katiba yapitishwa kwa kura mbili tu.
“Mimi nilidhani wangeandika vinginevyo. Sijui kwa
nini wasingetumia ile ya wajumbe watano waliopiga kura ya ‘hapana’,
labda hiyo ndiyo ilikuwa inanoga zaidi,” alisema.
Ingawa hakulitaja gazeti hilo, Mwananchi ndilo liliandika kichwa
hicho cha habari, likimaanisha kuwa idadi ya kura zilizozidi kwenye
akidi ya kura 146 iliyokuwa inatakiwa kutoka Zanzibar zilikuwa mbili tu.
Shughuli ilivyokuwa
Katiba inayopendekezwa ilikabidhiwa kwa Rais
Kikwete mbele ya umati mkubwa wa watu uliofurika katika Uwanja wa
Jamhuri, chini ya ulinzi mkali wa polisi na vikosi vingine vya usalama.
Makundi ya watu na wageni waalikwa yalianza
kuingia uwanjani asubuhi kupitia milango mitatu, lakini hata hivyo
uwanja huo haukujaa kama ilivyotarajiwa.
Rais Kikwete aliingia katika uwanja huo saa 9:27
alasiri akitanguliwa na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein huku
viongozi wengine wakiwa wameshatangulia kufika uwanjani.
Waliohudhuria
Viongozi wengine waliohudhuria ni Makamu wa Rais,
Dk Mohamed Gharib Bilal, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Rais Mstaafu, Ali
Hassan Mwinyi na mawaziri wakuu wastaafu, Frederick Sumaye na Edward
Lowassa.
Wengine ni Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP),
Ernest Mangu, majaji wakuu wa Muungano na Zanzibar, wakuu wa mikoa na
baadhi ya viongozi wa dini ambao pia walianza kwa kutoa dua.
Baadhi ya viongozi wa dini waliokuwapo ni Sheikh
Mustapha Rajab Shaaban na Askofu Amos Mhagachi. Viongozi wengine
walikuwa ni mabalozi 26 wanaowakilisha nchi zao, wakiwamo kutoka
Ujerumani, Umoja wa Nchi za Ulaya, Norway, Nigeria, Sweden, Qatar,
Ireland na Zambia.
Wengine ni kutoka Afrika Kusini, Zimbabwe, DR
Congo, Algeria, Ufaransa, India, Indonesia, Kenya, Malawi, Rwanda,
Somalia, Falme za Kiarabu, Uganda, Vietnam, Yemen na Iran. Ndani na nje
ya uwanja, polisi wenye silaha walionekana kutanda wengine wakiwa juu ya
majengo kuimarisha ulinzi.
Kabla ya kuwasili kwa viongozi hao, wajumbe wa
lililokuwa Bunge la Katiba walisakata muziki wa mwambao huku wengi wao
na hasa wanawake, wakiwa wamevaa sare maalumu.
Nyimbo nyingi zilizokuwa zikiimbwa zililenga
kuwasifia wajumbe wa Bunge hilo na Rais Kikwete na zikiwaponda wajumbe
waliosusia vikao.
Wasanii waliotumbuiza katika sherehe hizo ni John Komba, Khadija
Kopa, Mrisho Mpoto na mwigizaji wa sauti, Steve Nyerere ambao wote
walilenga kuwahamasisha Watanzania waikubali Katiba inayopendekezwa.
Maoni ya watu
Baadhi ya watu waliohudhuria walitoa maoni yao
baadhi wakipongeza na wengine kuonyesha shaka kuhusu namna Katiba hiyo
iwapo itakubalika.
Mwenyekiti wa CCM, Wilaya ya Chamwino, Charles
Ulanga, aliisifia akisema ni nzuri lakini akaonyesha wasiwasi kuwa
juhudi za kuwaelimisha wananchi zisipofanyika itakuwa tabu kuipitisha.
Ulanga alisema uelewa wa wananchi ni mdogo kiasi
kwamba wanahitaji kufikishiwa elimu pamoja na Katiba yenyewe ili waisome
kabla ya kufanya uamuzi.
“Tatizo ni wale wanasiasa ambao walitoka, wamekuwa
wakiwaaminisha wananchi juu ya mambo mengi sana, sasa kama elimu
haitawafikia kikamilifu wananchi wanaweza kufanya uamuzi ambao si
mzuri,” alisema Ulanga.
Mkulima wa Kijiji cha Msalato, Andrew Mdumula
alisema Katiba hiyo imegusa masilahi mapana ya wakulima, likiwamo suala
la umiliki wa ardhi na jinsi ya kulipwa fidia.
Chapisha Maoni