HOME
MWANASHERIA MKUU ZANZIBAR ALIYETIMULIWA ASEMA, IPO SIKU UKWELI UTAJULIKANA!
Mwanasheria
Mkuu wa Zanzibar aliyefukuzwa kazi, Othman Masoud Othman (mwenye
mkoba), siku alipopiga kura ya 'HAPANA' ambayo ndiyo imemponza.
Dar es Salaam. Kung’olewa
kwa aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman katika
nafasi hiyo ni kama kumewasha moto visiwani humo huku mwenyewe akisema:
‘Ipo siku ukweli utadhihirika.’
Othman licha
ya kutafutwa kutwa nzima ya jana, hakuwa tayari kuzungumzia kufukuzwa
kwake kazi na badala yake alituma ujumbe mfupi kupitia simu yake ya
kiganjani akisema: “Si wakati wake kulizungumza.”
Alipoulizwa
kwamba pengine anaweza kuwa tayari lini kuzungumzia suala hilo,
Mwanasheria huyo aliyepinga baadhi ya Ibara za Katiba zinazopendekezwa
kwa kuzipigia kura za hapana, alijibu pia kwa kifupi: “I have no idea
when (sifahamu ni lini), time will tell (ipo siku ukweli utadhihiri)”.
Kwa upande
mwingine, watu wa kada mbalimbali nchini wameelezea uamuzi wa Rais wa
Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kumtimua kazi kuwa ni uonevu kwa kuwa
alitumia haki yake ya kikatiba.
Mwalimu wa
Idara ya Lugha za Kigeni na Isimu wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM),
Faraja Christoms alisema, “Sidhani kama ni matumizi mazuri ya madaraka.
Othman katika maelezo yake alitamka wazi kuwa maoni yake si msimamo wa
Serikali ya Zanzibar. Alichokizungumza ndiyo msimamo wake binafsi na
jinsi anavyoona inafaa.”
Alisema
Mwanasheria huyo katika maoni yake alieleza wazi jinsi Katiba ya
Zanzibar inavyokinzana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano...
“Kilichomtokea ni tatizo la kutokuwapo kwa maridhiano tangu ulipoanza
mchakato wa kuandika Katiba Mpya.”
Mkurugenzi
Mtendaji wa shirika lisilokuwa la kiserikali linalojihusisha na masuala
ya kijamii (Fordia), Buberwa Kaiza alisema wajumbe wa Bunge la Katiba
walipiga kura kwa utashi wao na si ushawishi kutoka katika makundi
wanayotoka.
“Alichokizungumza
Othman si maoni ya Serikali za Zanzibar. Alipokuwa bungeni alikuwa sawa
na wajumbe wengine na si mwakilishi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Hii ni ishara mbaya kwa watendaji wa Serikali. Maana yake ni kwamba
watendaji wa chini wakifichua uovu unaofanywa na walio juu yao wanaweza
kufukuzwa kazi.”
Mtaalamu wa
Lugha ya Kiswahili, Dk Aldin Mutembei alisema: “Sasa watu wameanza
kuzuiwa kuamua mambo yao wao wenyewe. Othman alipiga kura kama yeye
binafsi na si Serikali ya Zanzibar tena akiwa na mawazo huru kabisa.
Kumfukuza kazi ni kutomtendea haki.”
Mwenyekiti
wa Chadema, Freeman Mbowe alisema: “Ubatili siku zote huzaa ubatili.
Nchi yetu sijui inakwenda wapi, maana watu wanazuiwa kufanya mambo yao
ambayo yapo kikatiba. Maandamano hakuna, ukisema ukweli unafukuzwa kazi?
“Watanzania
wataendelea kudai Katiba yenye maoni yao. Hii ni ishara ya kutaka
kuwafumba midomo wengine wanaopenda kueleza ukweli.
Mhadhiri wa
UDSM, Dk Benson Bana alikuwa tofauti na wenzake, akisema kilichomkuta
mwanasheria huyo alikitarajia kwa sababu kitendo chake cha kupiga kura
ya hapana kilimaanisha kuwa amekwenda tofauti na msimamo wa Serikali ya
Zanzibar.
“AG
anahudhuria vikao vya Baraza la Mawaziri la Zanzibar na ni lazima kuna
mambo ambayo wanakubaliana, ambayo unatakiwa uyapinge ukiwa nao na si
nje ya vikao vyenu.
“Alipokuwa
bungeni alikuwa amebeba msimamo wa Zanzibar na kitendo cha kupiga
‘hapana’ ni kinyume na miiko ya uwajibikaji wa pamoja,” alisema Dk Bana.
Waziri wa
Katiba na Sheria wa Zanzibar, Abubakar Khamis Abubakar (CUF), alisema
hafahamu sababu za kigogo huyo kuvuliwa wadhifa wake.
“Aliyemwondoa AG ni Rais wa Zanzibar, yeye ndiye atakuwa anajua sababu za kufuta uteuzi wake,” alisema Abubakar.
Hata hivyo,
Rais wa Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS), Awadh Ali Said alisema
haikuwa wakati mwafaka kwa Rais Shein kumvua wadhifa Othman wakati Taifa
bado halijakamilisha mchakato wa kupata Katiba ya Muungano na Zanzibar.
Alisema
alikuwa akitetea mambo hayo kwa kuweka mbele manufaa ya Zanzibar na
wananchi wake pamoja na vizazi vijavyo hasa kwa kuzingatia kuwa SMZ
haikuwa na msimamo wa pamoja katika suala la mabadiliko ya Katiba ya
Muungano tangu mwanzo.
Alisema
uamuzi wa kumvua wadhifa una madhara makubwa ikiwamo kuwajengea misingi
ya woga watendaji wakuu na kujikuta wakishindwa kujitokeza kutetea au
kupigania mambo ya msingi yenye manufaa kwa Zanzibar na wananchi wake.
Mwanasheria
Mkuu wa zamani, Hamid Mbwezeleni alisema kwamba Rais hajafanya kosa kwa
kumwondoa kwa sababu anatekeleza wajibu wake kwa mujibu wa Katiba na
sheria za nchi kama vile alivyomchagua na Katiba inampa haki ya
kumwondoa.
Naibu Katibu
Mkuu wa CUF na Waziri wa Biashara Viwanda na Masoko Zanzibar, Ahmed
Nassor Mazrui, alisema haikuwa busara kufukuzwa kazi wakati huu nchi
ikiwa katika mjadala mkubwa wa kutafuta Katiba Mpya.
Alisema AG
hakufanya makosa kutetea msimamo unaokwenda kinyume na ule wa CCM katika
kutafuta Katiba Mpya kwa kuwa alikuwa akitoa maoni yake kama wajumbe
wengine wa Bunge la Katiba.
Katibu
Mwenezi wa CCM Wilaya ya Mjini Unguja, Baraka Shamte alisema Othman
alitakiwa kujiuzulu wadhifa wake kabla ya kutimuliwa kazi kutokana na
kitendo chake cha kutetea mfumo wa Muungano wa Serikali tatu kinyume na
matakwa ya Serikali zote mbili ya Zanzibar na ile ya Muungano.
“AG ni
sehemu ya Serikali, hakupaswa kujitokeza hadharani kupinga mfumo wa
muungano wa Serikali mbili kinyume na mtazamo wa bosi wake anayetetea
serikali mbili katika mfumo wa Muungano,” alisema Shamte.
Chapisha Maoni