HOME
Mwanasheria Mkuu ZNZ ametolewa kafara?
Bila shaka suala linalotawala gumzo na mijadala
mingi visiwani Zanzibar hivi sasa ni hatua ya juzi ya Rais wa Zanzibar,
Dk Ali Mohamed Shein kumfukuza kazi Mwanasheria Mkuu wa SMZ, Othman
Masoud Othman. Wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini walibashiri
kutimuliwa kwake alipopiga kura katika Bunge la Katiba wiki iliyopita na
kukataa ibara 22 za Rasimu ya Katiba inayopendekezwa. Hatua hiyo ilizua
mtafaruku mkubwa ndani ya Bunge na kuwafadhaisha wajumbe wa chama
tawala ambao tangu awali walitakiwa na chama hicho kupiga kura ya
‘ndiyo’ ili Rasimu ya Katiba iweze kupitishwa.
Mtafaruku ulioibuka bungeni siku hiyo
ulisababishwa na mambo matatu makubwa. Kwanza, wakati mwanasheria huyo
mkuu wa SMZ akipiga kura hiyo, yalikuwapo mazingira yaliyoonyesha kwamba
uwezekano wa kupatikana kwa theluthi mbili za wajumbe kutoka Zanzibar
ili kupitisha Rasimu hiyo ya Katiba ulikuwa mdogo sana. Hivyo, uongozi
wa Bunge na viongozi wa serikali kutoka pande mbili za Muungano walikuwa
katika wakati mgumu wakihaha kwa nguvu zote kupata akidi ya kura.
Pili, mwanasheria mkuu huyo alijitokeza dakika za
mwisho kabisa kupiga kura hiyo. Wajumbe, viongozi wa serikali na uongozi
wa Bunge waliamini kwamba ingekuwa kura ya turufu na ndiyo ingeamua
matokeo na mustakabali wa Rasimu hiyo ya Katiba. Pamoja na msimamo wake
wa kutoikubali Rasimu hiyo kujulikana mapema wakati alipojitoa katika
Kamati ya Uandishi ya Bunge, bado wajumbe wengi waliamini kwamba katika
nafasi yake kama mshauri mkuu wa SMZ katika masuala ya sheria,
angelazimika kupiga kura ya ‘ndiyo’ kuiepusha SMZ na aibu ya kuonekana
ikikwamisha Rasimu hiyo. Jambo la tatu lililosababisha mtafaruku huo ni
sarakasi zilizotawala upigaji kura na zoezi hilo kuonyeshwa moja kwa
moja kwenye runinga nchi nzima, kiasi cha kufanya wajumbe na viongozi wa
Zanzibar kuhofia kuonekana wasaliti kwa wenzao wa Tanzania Bara iwapo
Rasimu hiyo isingepitishwa.
Hivyo, hata kama hatimaye Rasimu hiyo ilipitishwa,
hasira za chama tawala, wajumbe wa chama hicho na viongozi wa Bunge
dhidi ya mwanasheria huyo mkuu, zilibaki palepale. Tulishuhudia baadhi
ya wajumbe wakionyesha hasira hizo kwa kumzomea na kumtishia maisha mara
tu alipopiga kura hiyo, na kulazimika kutoka nje ya Bunge kwa ulinzi
mkali na baadaye kurudi Zanzibar mara moja. Ndiyo maana tunasema hatua
ya Rais wa Zanzibar kumfuta kazi ilitarajiwa na wengi, hasa tukizingatia
kwamba hatua hiyo ya Rais Shein inatokana na mamlaka aliyopewa na
Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi wanasema
mwanasheria huyo mkuu ametolewa kafara. Hoja yao ya msingi ni kuwa, kama
SMZ tangu awali ilisema kupitia Baraza la Wawakilishi kwamba haikuwa na
msimamo wowote juu ya Rasimu hiyo ya Katiba, kwa maana kwamba wajumbe
kutoka Zanzibar wangekuwa huru bungeni kupiga kura au kufanya uamuzi
kadri watakavyoona inafaa, basi mwanasheria huyo mkuu hakufanya kosa
lolote kwa kupiga kura ya ‘hapana’.
Vinginevyo, hatua ya Rais Shein kumfukuza kazi
inajenga picha kwamba mawaziri na watumishi wa serikali na taasisi zake
waliokuwa bungeni, hawakuwa huru kufanya uamuzi kwa utashi wao, bali
walipaswa kufuata msimamo na maagizo ya serikali hizo mbili.
Chapisha Maoni