Unknown Unknown Author
Title:
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
HOME Utegemezi umechangia kudhoofisha shilingi yetu Kwa vig...
HOME

Utegemezi umechangia kudhoofisha shilingi yetu




Kwa vigezo vyovyote vile vya kimataifa, uchumi wetu bado unaonekana haupo salama. Hali iko hivyo licha ya kuwepo kwa utajiri mkubwa wa rasilimali kama dhahabu na gesi asilia.
Hali kadhalika shilingi yetu imeendelea kusuasua miongoni mwa sarafu za kimataifa. Kwa mfano. kwa sasa shilingi moja ya Kenya ni wastani wa Sh18.
Uchumi wetu umeendelea kuambaa kwenye kingo za lindi refu la umaskini, licha ya kuwepo kwa uwezo wa kuondokana na adha hiyo, kwani tunazo rasilimali za kutosha kama nilivyoeleza.
Mikataba ya madini ambayo ungetarajia kuiona zama za kina Chifu Mangungo za kumruhusu “mwekezaji”, katika kila kilo kumi za dhahabu atakazo vuna, aondoke na kilo saba na wewe mmiliki wa utajiri huo kubakiwa na kilo tatu, bado inaendelea hadi sasa.
Japo marekebisho kidogo yamefanyika katika mirabaha ya mavuno bado marekebisho hayo hayaridhishi, ikilinganishwa na namna nchi nyinginezo duniani kama Botswana na Afrika ya Kusini zinavyofanya.
Utegemezi katika nyanja zote za uchumi, ndicho chanzo kikubwa cha umaskini na hali duni ya maisha ya watu wetu nchini.
Huwezi kuwa na uchumi imara au shilingi yenye nguvu, iwapo kwa miaka nenda rudi, sehemu kubwa ya mahitaji yako inatokana na bidhaa zinazotengenezwa na nchi nyingine duniani.
Huwezi kuwa na uwezo wa kudhibiti mfumuko wa bei ndani ya nchi, iwapo sehemu kubwa ya mahitaji yako ya msingi, inatokana na bidhaa zinazoagizwa nje ya nchi.
Pamoja na jitihada kubwa zilizofanyika nchini za kutokomeza umasikini uliokithiri, Tanzania bado inahesabika kuwa miongoni mwa nchi zilizo maskini zaidi duniani.
Mwaka 2012, kipato cha wastani cha Mtanzania mmoja kwa mwaka kilikadiriwa kuwa Dola 570 za Marekani. Taarifa hiyo ni kwa mujibu wa tathmini za Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani (IMF).
Kipato hicho ni wastani wa Dola 1.6 za Marekani kwa siku kwa mtu mmoja. Kipato kilichoifanya Tanzania ishike nafasi ya 176 miongoni mwa nchi 191 duniani.
Wakati huohuo, bado kuna Watanzania wasiopungua milioni 12 wanaokabiliwa na umaskini uliokithiri.
Novemba 2013, Serikali ilitangaza kwamba idadi ya Watanzania ambao bado wanaishi chini ya “mstari wa umaskini (below poverty line)”, imepungua hadi kufikia asilimia 28.2 ya Watanzania wote, kutoka kiwango cha asilimia 33.6 kilichokuwapo mwaka 2007.
Viashiria au vigezo mbalimbali vya maendeleo, bado vinaashiria kwamba hali ya uchumi wa Tanzania bado haijatengemaa kama baadhi ya taasisi za fedha za kimataifa zinavyojaribu kwa nguvu zote kutuaminisha.
Bado tuna kibarua pevu mbele yetu. Kuwa na utajiri wa maliasili na rasilimali lukuki ni kitu kimoja na kuwa na kiwango cha juu cha maendeleo ya kiuchumi na kiteknolojia ni kitu kingine.
Katika kigezo cha maendeleo ya watu au ustawi wa jamii (Human Development Index), Tanzania imeshika nafasi ya 152 miongoni mwa nchi 182 duniani.
Katika kigezo cha ubora wa mazingira ya kibiashara na uwekezaji au kufanya biashara (Business Environment), Tanzania imeshika nafasi ya 134 miongoni mwa nchi 185 duniani.
Katika kigezo cha uimara wa huduma bora za usimamizi wa Serikali au taasisi za umma (Government effectiveness), Tanzania imeshika nafasi ya 135 miongoni mwa nchi 212 duniani.

About Author

Advertisement

Chapisha Maoni

 
Top