Unknown Unknown Author
Title:
Author: Unknown
Rating 5 of 5 Des:
HOME Kizungumkuti juu ya kura mbili zilizoipitisha rasimu inayopendekezwa chaanza kufukuta   Utata umezidi kugubika ...
HOME

Kizungumkuti juu ya kura mbili zilizoipitisha rasimu inayopendekezwa chaanza kufukuta

 




Utata umezidi kugubika kura mbili zilizowezesha kupitishwa kwa Katiba Inayopendekezwa ambayo wiki iliyopita ilikabidhiwa kwa Rais Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein mjini Dodoma.

Utata huo unatokana na kura za wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) upande wa visiwani, wajumbe waliokuwa Hijja, Saudi Arabia na zile za baadhi ya wajumbe wanaodaiwa kuhamishwa kinyemela kutoka Bara kwenda Zanzibar au kinyume chake.
Utata Saudia
Chanzo chetu kutoka Dodoma kilisema: “Kuna utata maana hakuna uhakika iwapo kweli mahujaji ambao ni wajumbe wa Bunge la Katiba walipiga kura maana kuna barua ilitoka ubalozini Saudi Arabia ikisema hilo lisingewezekana.”
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa Ubalozi wa Tanzania Riyadh, uliandika barua kwa Bunge Maalumu la Katiba ukieleza kwamba usingeweza kuratibu upigaji kura kutokana na mazingira halisi ya ibada ya Hijja.
Miongoni mwa sababu zilizotolewa na ofisi ya ubalozi huo ni kwamba mtu yeyote ambaye si hujaji hakuwa anaruhusiwa kuingia katika maeneo ya Hijja na Serikali ya Saudi Arabia ilikuwa imetoa vitambulisho maalumu kwa mahujaji tu.
Katibu wa Bunge Maalumu, Yahya Khamis Hamad alikiri kupokea barua kutoka Ubalozi wa Tanzania uliopo Riyadh, ukieleza kwamba mazingira yasingeruhusu wajumbe hao wanane kupiga kura, lakini akasema walitumia njia nyingine kufanikisha kazi hiyo.
“Tulipokea barua hiyo kweli na pengine niseme tu siyo moja, zilikuwa barua kama tatu au nne hivi, maana hata hapa foreign (Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa) Dar es Salaam walituandikia kuhusu ugumu wanaouona, lakini baada ya kuona hivyo tuliamua kutumia njia zetu wenyewe.
“Tulimtuma ofisa wetu kwenda Saudi Arabia na tulimkatia tiketi na kusema kweli wakati wote alikuwa akiwasiliana nasi, nakumbuka mtu wa kwanza kupiga kura alikuwa Raza (Mohamed, Mwakilishi wa Uzini) ambaye alikuwa Dubai na baada ya hapo alikwenda walikokuwa mahujaji wengine na walifanikisha vizuri sana,” alisema.
Wajumbe wengine waliokuwa Uarabuni kwa mujibu wa orodha iliyotangazwa na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta ni pamoja na Dk Abdallah Kigoda, Sheikh Mussa Kundecha, Hamza Mustapha Njozi, Dk Maua Daftari, Shawana Bukheti Hassan, Asha Mtwangi, Amina Andrew Clement na Riziki Lulida.
Kauli ya Balozi
Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia, Profesa Abdilahi Omari alipoulizwa kuhusu suala hilo hakuwa tayari kutoa majibu ya moja kwa moja juu ya ofisi yake kushindwa kuratibu upigaji kura badala yake akataka watafutwe wasemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikano wa Kimataifa.
Alipoulizwa kuhusu ofisi yake kuandika barua kukataa jukumu la kuratibu kazi hiyo, alikiri kwamba ni kweli aliandika barua kuhusu suala hilo lakini barua hiyo haikuelekezwa kwa uongozi wa Bunge Maalumu, bali kwa Katibu Mkuu wa wizara yake.
“Kama kuandika barua tu, hiyo ndiyo kazi ya kila ubalozi, kwa hiyo barua naandika nyingi tu kila kukicha lakini haziendi kwingine zaidi ya pale wizarani kwa Katibu Mkuu ambaye ndiye msemaji mkuu wa wizara,” alisema Profesa Omari.
Msemaji Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mkumbwa Ally alikiri wizara hiyo kupokea barua kutoka kwa Balozi Omari na baadaye kuuandikia uongozi wa Bunge Maalumu kuhusu majibu ya Ubalozi wa Riyadh.
“Kimsingi siyo kwamba ubalozi wetu ulishindwa au ulikataa kufanya kazi hiyo, hapana; isipokuwa tatizo ni muda kwamba wakati suala hilo linapelekwa tayari muda ulikuwa umepita na suala la mahujaji lilikuwa mikononi mwa Serikali ya Saudi Arabia,” alisema Ally na kuongeza:
“Mahujaji wote wanakuwa chini ya Serikali na kuna wizara kabisa inayoshughulikia suala la Hijja, sasa muda ule wa kujiandikisha na mambo mengine ukishapita hakuna jinsi ambavyo ubalozi wetu ungeweza kusaidia.”
Mazingira ya Hijja
Mmoja wa waumini wa dini ya Kiislamu ambaye amekuwa akisafirisha mahujaji alisema wakati wa Hijja hufanyika ufuatiliaji wa hali ya juu kwa mahujaji ili kudhibiti idadi ya watu wanaotakiwa kuingia katika eneo hilo.
Muumini huyo aliyeomba jina lake lisiandikwe gazetini, alisema udhibiti huo hufanyika wakati wa kutoa viza.
“Kwa hiyo kama jina la mtu halimo kwenye orodha ya mahujaji ni vigumu kupenya kuingia Makka au Madina na kama akienda, basi ataishia maeneo mengine na siyo katika eneo la hijja,” alisema.

Hata hivyo, Naibu Katibu wa Bunge Maalumu, Dk Thomas Kashilila alisema ofisa aliyepelekwa Saudi Arabia aliwahi kuwa mtumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje akiwa katika eneo la Jumuiya ya Falme za Kiarabu (UAE), hivyo ilikuwa rahisi kwake kufanya kazi hiyo kwa ufanisi.
Kura za Zanzibar
Utata mwingine umeibuliwa na Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba (Jukata), Deus Kibamba kuwa Zakia Meghji alipiga kura kama mjumbe kutoka Zanzibar wakati jina lake liliingia bungeni akiwa ni mjumbe kutoka Bara.
Kibamba alisema katika Tangazo namba tano lililotolewa kwenye Gazeti la Serikali, Februari 7, mwaka huu likiwatangaza wajumbe wote, jina la Meghji lilikuwa linatoka Bara.
Hivyo, Kibamba alisema kura hiyo ni batili ikiungana na kura ya Makamu Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi (Zanzibar), Haji Ambar Khamis aliyekanusha kupiga kura licha ya kuorodheshwa.
Alipoulizwa kuhusu kura hiyo, Dk Kashilila alisema yupo nje ya ofisi na leo atakuwa kwenye mazishi mkoani Mwanza, hivyo atafutwe kesho. Hamad hakupatikana kupitia simu yake wakati ile ya Meghji ilikuwa ikiita bila kupokewa.
Utata kura za Ukawa
Eneo jingine ambalo limeacha maswali mengi kuhusu idadi ya kura ni idadi ya wajumbe wa Zanzibar ikilinganishwa na matokeo ya kura yaliyotangazwa na Dk Kashilila, huku majina ya wajumbe hao yakibakia kuwa siri hadi sasa.
Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, James Mbatia alisema hakuna mjumbe yeyote wa kundi hilo aliyepiga kura tofauti na madai ya uongozi wa Bunge kwamba kuna wajumbe wa Ukawa waliofanya hivyo.
“Sitta alisema wapo wajumbe wawili, lakini hajawahi kuwataja hadharani, kama kweli wapo si angewataja kwamba ni fulani na fulani, lakini kusema tu kwamba wapo waliopiga kura kupitisha Katiba kutoka Ukawa, si kweli na lengo ni kutaka kuhalalisha uchakachuaji wa kura walioufanya,” alisema Mbatia.
Tayari mjumbe wa kundi hilo kupitia NCCR-Mageuzi, Haji Ambar Khamis amekanusha kupiga kura licha ya jina lake kuwekwa karika orodha ya waliopiga kura za ‘ndiyo’, lakini uongozi wa Bunge ukajibu kuwa jina hilo liliwekwa kimakosa na haliathiri matokeo ya kura.
Katibu wa Bunge hilo, Hamad alisema wakati wakiandaa kupeleka karatasi ya kura kwa mjumbe wa Bunge hilo, Saada Mkuya Salum aliyekuwa Zanzibar, alipata taarifa kutoka kwa uongozi wa Bunge kwamba kulikuwa na wajumbe wengine wawili ambao walikuwa tayari kupiga kura.
“Majina yao siwezi kukutajia maana baada ya kupokea taarifa hizo niliwatafuta kwa simu na walisema wako tayari kupiga kura kwa masharti kwamba kura zao zitakuwa ni siri, hivyo hazitoandikwa majina,” alisema Hamad na kuongeza:
“Kwa hiyo maofisa wetu waliwapelekea ballot paper (karatasi za kura) na walipiga kura na wamesaini fomu za kuthibitisha kwamba wamepiga kura, wala hilo halina ubishi.”
Hamad alisema mpango wa kuwawezesha watu hao kupiga kura ulifanikishwa na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samia Suluhu Hassan na Mbunge wa Wawi (CUF), Hamad Rashid Mohamed.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Mohamed alikaririwa na gazeti hili akitamba kwamba yeye ndiye aliyefanikisha mpango huo.
Wajumbe waliowindwa
Habari ambazo zililifikia gazeti hili zinasema wajumbe wanne upande wa Zanzibar; mmoja kutoka NCCR-Mageuzi na watatu kutoka Chadema ndiyo walikuwa wamelengwa na mpango huo.
Wengine waliokuwa wakisakwa mbali na Ambar Khamis ni Zeudi Mvano Abdillahi, Maryam Msabaha na Mwanamrisho Taratibu Abama kutoka Chadema.
Zeudi alisema jitihada za kumtaka arejee bungeni hazikuanza wakati wa kupiga kura, bali tangu Ukawa waliposusia Bunge hilo, Aprili 16, mwaka huu.
“Wote walionifuata niliwaambia mchana kweupe na bila hata kumung’unya maneno kwamba siwezi kuisaliti nafsi yangu wala wananchi wa Zanzibar, kwa hiyo kama simu nilipata nyingi sana na hata wale walioniambia ana kwa ana nao niliwapa majibu hayo hayo,” alisema Zeudi.
Msabaha alisema: “Kweli nimesumbuliwa sana na watu ambao siwezi kuwataja na wananitaka nipige kura na wengine walifika mpaka nyumbani lakini mimi siwezi kushiriki upuuzi huo maana nikifanya hivyo dhamiri yangu itanishtaki.”
Abama alisema: “Nisingependa kuzungumzia kwa undani suala hili lakini ninachoweza kusema ni kwamba nimepewa alert (ilani) na viongozi wangu kwamba nasakwa, kwa hiyo nimekaa ndani tu wala sitoki maana sina uhakika hao wanaonisaka wana malengo gani.”
Je unataka niwe nakujuza kil kinachonifia?Mimi niko tayari kama utakuwa umelike katika Facebook Twitter 

About Author

Advertisement

Chapisha Maoni

 
Top