HOME
JK agusia ujana urais 2015
Tabora/Dar. Wakati mbio za
kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu 2015 zikianza kushika kasi nchini,
Rais Jakaya Kikwete amewataka vijana kumchagua mtu anayefanana na kijana
kurithi nafasi yake.
Kauli hiyo ya Rais Kikwete imekuja huku kukiwa na
makada kadhaa ndani ya chama chake ambao wametangaza nia ya kuwania
nafasi hiyo huku baadhi wakifungiwa kwa kuanza kampeni mapema na wengine
wakiendelea na mikakati ya chinichini kabla ya kujitangaza.
Rais Kikwete alisema hayo jana mjini Tabora
alipokuwa akihutubia wananchi waliohudhuria kumbukumbu ya Baba wa Taifa,
Mwalimu Julius Nyerere zilizokwenda sambamba na kilele cha Wiki ya
Vijana na hitimisho la Mbio za Mwenge wa Uhuru.
Alisema vijana ndiyo chachu ya maendeleo ya Taifa
lolote hivyo washiriki katika kugombea nafasi mbalimbali za uongozi na
kushiriki kupiga kura kumchagua rais anayefanana na kijana kama
alivyokuwa yeye wakati akigombea urais 2005, wakati huo akiwa na umri wa
miaka 55.
“Siyo kijana wa chini ya miaka 35, Katiba yetu
hairuhusu, lakini mtu ambaye anaonekana kijana kama nilivyokuwa mimi
wakati nagombea nafasi hiyo mwaka 2005,” alisema Rais Kikwete huku
akishangiliwa na umati mkubwa wa watu waliohudhuria uwanjani hapo.
Mgombea mwenye sifa zilizotajwa na Rais Kikwete
anaweza kutoka nje au katika kundi la wanaCCM wanaotajwa au kutangaza
nia ya kuwania nafasi hiyo ya juu.
Miongoni mwa wanaotajwa wamo makada sita waliopewa
onyo kali na chama hicho kwa kuanza kampeni mapema wakiwamo mawaziri
wakuu wa zamani, Edward Lowassa (61) na Frederick Sumaye (64) na Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe (61).
Wamo pia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano
na Uratibu), Stephen Wasira (69), Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi
na Teknolojia, January Makamba (40) na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati
na Madini, William Ngeleja (47).
Mbali na hao waliopewa onyo, wanaCCM wengine
wanaotajwa ni pamoja na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda (66), Waziri wa
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta (72), Mbunge wa Nzega, Dk
Hamis Kigwangalla (39), Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba (39) na
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya
(65).
Pia wamo Mbunge wa Songea Mjini, Dk Emmanuel
Nchimbi (43), Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein (66) na Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dk Mohamed Gharib Bilal (69).
Kauli hiyo ya Rais Kikwete ni kama ile iliyowahi
kutolewa na Rais mstaafu, Benjamin Mkapa mwaka 2005, kwa wajumbe wa
Mkutano Mkuu ambapo aliweka bayana kwamba wakati huo ulikuwa ni wa
vijana kuongoza nchi kwa kuwa tafiti ndivyo zilivyokuwa zikionyesha.
Baada ya Rais Mkapa kutoa kauli hiyo, wakati huo
Kikwete ndiye aliyepitishwa na CCM kugombea urais kwa kuwashinda wenzake
11 waliojitokeza ndani ya chama hicho kuwania uteuzi huo.
Rais Mkapa alisema pamoja na kuwa mgombea wa CCM anapaswa kuwa
na sifa 13 zilizoainishwa na NEC, yafaa pia kuwa na sifa za ziada ambazo
ni kuwa na mtu anayechagulika pande zote za Muungano, anayekubalika
katika kundi la vijana, ana historia iliyotukuka ndani ya chama na si
mtu aliyechipuka tu, anayeijua zaidi CCM, Muungano na Mapinduzi na
kwamba Tanzania chini yake itakuwa salama.
Pia awe ni mtu asiye na visasi, chuki, hasira na anayepima mambo kabla ya kufanya uamuzi.
Akizungumzia umuhimu wa vijana jana, Rais Kikwete
alibainisha kuwa umetambuliwa katika Katiba Inayopendekezwa kwa kuundwa
kwa Baraza la Vijana litakalowaunganisha vijana wote nchini bila kujali
tofauti zao.
Alizitaka wizara zinazohusika kuhakikisha mifuko
ya maendeleo ya vijana pamoja na wanawake inakuwa na fedha za kutosha na
kuhakikisha zinawafikia walengwa.
“Pia naziagiza halmashauri zote nchini kuanza
kutoa taarifa za utekelezaji wa miradi ya maendeleo kila baada ya miezi
minne kuanzia Desemba mwaka huu,” alisema na kuongeza kuwa iwe mara ya
mwisho kwa halmashauri kufanya vibaya.
Kuhusu Nyerere
Rais Kikwete alimtaja Mwalimu Nyerere kuwa
kiongozi ambaye hana mfano nchini akieleza kuwa aliona umuhimu wa kuwa
na Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar, ndiyo maana Katiba
Inayopendekezwa inatambua Muungano wa serikali mbili.
Alielezea nadhiri aliyoiweka Mwalimu Nyerere juu
ya Mwenge wa Uhuru kwa kunukuu maneno yake, “Sisi watu wa Tanzania
tutaweka mwenge wa uhuru katika kilele cha Mlima Kilimanjaro ili uangaze
palipo na giza, ulete tumaini palipo na chuki na ulete umoja palipo na
utengano.”
Alimwelezea kiongozi huyo kama alama ya ukombozi
wa Bara la Afrika kwa kuwa alisaidia nchi nyingi kupata uhuru, zikiwamo
Namibia, Afrika Kusini na Msumbiji.
“Rais wa sasa wa Namibia (Hifikepunye Pohamba)
alikuja kuishi uhamishoni hapa Tanzania mara tu tulipopata uhuru.
Alikuwa anaishi kule Temeke, anaongea Kiswahili vizuri kama vijana wa
siku hizi.”
Apigia debe Katiba Inayopendekezwa
Rais Kikwete alisisitiza kuwa Katiba
Inayopendekezwa ambayo imepitishwa na Bunge la Katiba hivi karibuni ni
bora kuliko inayotumika sasa kwa sababu imetoa majawabu kwa changamoto
mbalimbali za kitaifa.
“Sherehe za kuzima Mwenge wa Uhuru zingeingia
dosari kama Bunge Maalumu la Katiba lingependekeza muundo wa serikali
tatu,” alisema Rais Kikwete.
Alisema Katiba hiyo imetambua haki za makundi
mbalimbali ya kijamii wakiwamo vijana, wanawake, watoto, wakulima,
wavuvi na wasanii. Hata hivyo, alisema Katiba hiyo ni matokeo ya
ushirikishwaji wa wananchi ndani na nje ya Bunge la Katiba.
“Ndugu zangu mjitokeze kupiga kura ya ‘ndiyo’ kwa
sababu Katiba hii ni bora, ni zaidi ya nzuri. Msikubali kutumiwa na
wanasiasa na wanaharakati kwa mambo ambayo hayana tija kwenu,” alisema.
Vita dhidi ya dawa za kulevya
Rais Kikwete alikiri kuwa vita dhidi ya dawa za
kulevya ni ngumu lakini Serikali imekuwa ikijitahidi kupambana na watu
wanaosafirisha dawa hizo ambazo zinawaharibu vijana wengi nchini.
Alisema vita inakuwa ngumu kwa sababu watu wanabuni mbinu mbalimbali za kusafirisha dawa hizo.
“Watu wanasafirisha dawa za kulevya kwenye malori
ya mafuta, wengine wanaficha katika sehemu ambazo hazistahili hata
kutajwa. Pamoja na mbinu zote hizo tumekuwa tukiwabaini,” alisema na
kuongeza kuwa watu 6,875 wamekamatwa na dawa hizo katika kuanzia Januari
– Oktoba mwaka huu.
Unataka niwe nakujuza kila kinachonifikia?mimi niko tayari lakini naomba ulike hapa>>>Facebook >>>Twitter
Unataka niwe nakujuza kila kinachonifikia?mimi niko tayari lakini naomba ulike hapa>>>Facebook >>>Twitter
Chapisha Maoni