HOME
Jinamizi la ajali za barabarani hadi lini?
Kwa muda mrefu sasa maisha ya Watanzania wengi
yamekuwa yakipotea na wengine wakibaki na ulemavu wa kudumu kutokana na
ajali za barabara.
Ni tatizo la muda mrefu ambalo, inavyoonekana ni
kama wenye mamlaka wamekosa ufumbuzi wake na wameamua kufunika kombe ili
mwanaharamu apite.
Tunasema hivi kwa sababu hatuoni hatua zozote za
maana zikichukuliwa zaidi ya kushuhudia ongezeko la hizi ajali, ambazo
nyingi zingeweza kuepukika.
Ajali nyingi zinazotokea zinasababishwa na uzembe
wa madereva. Mwendokasi wa madereva uliopitiliza mara nyingi
umeshutumiwa kuwa ni sababu kubwa ya ajali hizi.
Utaona dereva anachojua ni kupangua gia tu na
kuyapita magari mengine bila hata kuchukua tahadhari, matokeo yake ni
maafa kwa abiria wasio na hatia.
Baadhi ya barabara zetu huchangia ongezeko la ajali kutokana na ubovu uliokithiri na kukosa alama za barabarani.
Utakuta barabara ina mashimo au matuta ya hatari ambayo wenye mamlaka wanayaona, lakini hawachukui hatua zozote.
Matokeo yake dereva mgeni anapopita kwenye
barabara kama hii anaweza kupata ajali. Mfano mzuri ni barabara ya
Morogoro maeneo ya Ruvu na Chalinze.
Kwa Jiji la Dar es Salaam ndiyo usiseme, kwani
baadhi ya barabara, hasa zile za pembezoni, kwa kweli hazina hadhi ya
kuwa barabara za jiji.
Pia, moja ya sababu za ongezeko la ajali za
barabarani ni kuwa na idadi kubwa ya madereva wasio na sifa. Kuna
udhaifu mkubwa katika mfumo wetu wa utoaji wa leseni za udereva.
Leseni nyingi hasa za kuendesha magari madogo na
pikipiki zinatolewa kwa njia ya rushwa hali inayosababisha leseni hizi
kumilikiwa na madereva wasio na viwango na wasiojua sheria za usalama
barabarani. Mtu gani atakayepoteza muda wake kusomea udereva ikiwa
anajua kuwa akiwa na kiasi kidogo tu cha fedha atatafutiwa leseni na
kuletewa kokote aliko?
Kuna vishoka wanaoshirikiana na waliopewa dhamana
ya kutoa leseni hizi kuzisambaza kwa madereva hawa vihiyo na hivyo
kukwamisha juhudi za kupunguza ajali za barabarani. Wasioamini hili
wafanye utafiti na bila shaka watabaini uozo uliopo.
Kwenye upande wa pikipiki ndiyo balaa! Mengi yameshaongelewa
kuhusu tabia za vijana wetu kujifundisha kuendesha pikipiki asubuhi na
jioni yake kuanza kubeba abiria.
Madereva hawa wa bodaboda wengi wanachojali ni
hesabu tu, lakini kwenye usalama hakuna kitu. Mwendokasi ndiyo sifa yao
kubwa. Baadhi yao, hasa wale wanaokesha usiku kucha, hutumia sana pombe
aina kali na bangi ili kuwapa nguvu ya kufanya kazi. Staili yao ya
‘kanyaga twende’ katika kuendesha pikipiki zao, imekuwa kero kubwa kwa
watumiaji wengine wa barabara. Katika mazingira kama haya ajali
zitaendelea kutuandama tu.
Wakati wenye vyombo vya usafiri wanafidiwa vyombo
vyao na kampuni za bima abiria maskini hakuna anayewajali. Ni mara
chache sana kusikia kuna abiria aliyelipwa kutokana na madhara ya ajali
au familia iliyofidiwa kwa kupoteza ndugu yao katika ajali ya
barabarani.
Hili nalo ni jambo linalotakiwa liangaliwe kwa
makini na wenye mamlaka. Ikiwa kampuni hizi za bima zinakusanya
mamilioni kutoka kwa wachangiaji inakuwaje kuwe na utata katika kufidia
majeruhi na wafiwa baada ya ajali?
Si halali hata kidogo kushindwa kuwafidia watu waliosababishiwa madhara na wateja wa kampuni za bima.
Chapisha Maoni